-->

KILIMANJARO YACHAFUKA KWA MABOMU YA MACHOZI


Hai: Vurugu kubwa jana ziliibuka wilayani Hai Kilimanjaro na kulilazimu Jeshi la Polisi kufyatua mabomu ya machozi katika jitihada za kuzima vurugu hizo.
Hata hivyo, hali iliendelea kuwa tete ilipofika saa 10:00 alasiri na kulazimu Jeshi la Polisi kuongeza nguvu kwa kuwatuma askari zaidi wa kutuliza ghasia (FFU) kutoka Moshi Mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alilithibitishia gazeti hili kuibuka kwa vurugu hizo zilizoanza saa 6:00 mchana katika Kijiji cha Kwansera huko Masama.
“Ni kweli kuna vurugu kati ya Wananchi wa hicho kijiji na mwekezaji anayemiliki shamba kubwa la kahawa na migomba ndiyo vijana wetu wa FFU wameelekea huko,” alisema.
Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio zilisema Polisi wenye sare kutoka Kituo cha Bomang’ombe wilayani Hai ndio wa kwanza kufika eneo la tukio na kujaribu kudhibiti vurugu bila mafanikio.
“Mabomu ya kutosha yameshafyatuliwa hapa tangu saa 6:00 mchana, lakini hali siyo nzuri wananchi wanataka kuchoma moto majengo ya mwekezaji,” kilidokeza chanzo chetu.
Kiini cha mgogoro huo ni uhasama uliojengeka kati ya wananchi hao na mwekezaji huyo Mtanzania kutokana na mwekezaji kuhodhi eneo kubwa huku wananchi wakiwa hawana ardhi.
SOURCE:MWANANCHI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment