-->

MKUU WA WILAYA YA MBULU AWAPIGIA GOTI WANANCHI WAKE

Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya, amesema kuwa aliwapigia magoti wananchi wa Kijiji cha Hydom, ili kuonyesha unyenyekevu kwa wananchi hao aliodai walionekana kujazwa maneno ya uchochezi na wanasiasa ili wavuruge amani . 


Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya akiwa amewapigia wananchi magoti kwa maana ya kuonyesha unyenyekevu. 

Alisema kutokana fujo zilizofanywa na baadhi ya wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika majuzi, kwa nafasi yake angeweza kuagiza hata Jeshi la Polisi kuwadhibiti watu, lakini misingi ya dini yake haimruhusu kumdhuru mtu zaidi ya kumwonyesha unyenyekevu.
Alisema hali hiyo ndiyo iliyomfanya kuamua kupiga magoti na kumshtakia Mungu.
“Mimi ni mkristo, unyenyekevu ndiyo nguzo pekee ya kuonyesha upendo na kudumisha amani. Ningeweza kuagiza polisi wawadhibiti, lakini sioni sababu kwa kuwa hiyo siyo misingi ya utawala. Ndiyo maana nikaona bora nitumie njia nyingine ya kumshirikisha Mungu mbele yao,”alisema Choya na kuongeza:
“Wanasiasa wamekuwa wakipandikiza chuki kwa wananchi kwa makusudi kwa lengo la kuvuruga amani lakini kwa kumweka Mungu mbele nina imani tutafanikiwa ili siku moja tusije tukaingia kwenye mkumbo wa Syria na Misri”
Choya alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na Mwananchi Jumapili, siku chache baada ya kitendo chake cha kupiga magoti mbeye ya wananchi kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Haydom.
Mkuu huyo wa wilaya alidaiwa pia kuwalaani baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Haydom kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kumdharau na kutofuata maagizo yake, wakati yeye amewasaidia katika kutatua migogoro mbalimbali waliyokuwa nayo.
Tukio hilo la kusikitisha lilijitokeza baada ya wananchi wa kijiji hicho kupinga agizo la Choya, lililowataka kufanya uchaguzi wa kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho, kabla ya kufanya uchaguzi mdogo, ambapo walipinga kwa kudai kuwa hakuna sheria hiyo.
Mmoja wa wananchi hao alilumbana na mkuu huyo wa wilaya mbapo Choya alijibu; “Nami nitarudi kwetu." Naye Tikin akasema tena: “Unasema utarudi kwenu Biharamulo wakati hawakutaki kwani ulifukuzwa ubunge?”
Maneno hayo yalionyesha kumkwaza Choya ambapo alipiga magoti huku machozi yakimlenga na kumwomba Mungu afanye jambo kwa watu wa Haydom kwani wanamdharau kabla ya kujitokeza wazee watatu wa Haydom na kumwomba msamaha mkuu huyo wa wilaya.
Mwananchi
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment