Watahiniwa 3,000 wa kujitegemea wako hatarini
kutofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu kutokana na kile
kilichoelezwa kuwa ni Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutokuwa na
taarifa zao za kulipia karo za mtihani huo pamoja na zile za usajili.
Licha ya maelezo hayo ya Necta, taarifa
zinaonyesha kuwa watahiniwa hao walishalipa ada za mtihani huo kupitia
njia mbalimbali za kielektroniki zilizoainishwa na baraza hilo, ikiwamo
benki na kampuni za simu za mkononi.
Watahiniwa walipaswa kulipa Sh35,000 ikiwa ni ada za mtihani huo kupitia wakala mbalimbali walioteuliwa na Necta.
Gazeti hili lilifanikiwa kuona barua ya Necta
kwenda kwa mmoja wa wanafunzi waliojisajili kufanya mtihani huo kwa
mwaka 2013 ikimweleza kuwa, hataweza tena kufanya mtihani huo kwa kuwa
hakulipa karo ya mtihani huo.
Barua hiyo ilieleza kuwa, kumbukumbu za Necta
zinaonyesha kuwa wanafunzi hao wamejiandikisha kufanya mtihani, lakini
hawajawasilisha fomu za usajili wala kulipa karo za mtihani huo.
“Hivyo kwa barua hii, unafahamishwa kuwa
umeondolewa kuwa mtahiniwa mwaka 2013,” ilisema sehemu ya barua hiyo
zilizosambazwa kwa watahiniwa hao.
Kutokana na kuwepo hali hiyo, baadhi ya watahiniwa
kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameanza kufuatilia Necta kujua hatima
yao wakiwa na vielelezo vya malipo yao.
Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani Tanzania
(Necta), John Nchimbi alithibitisha kuwa baraza hilo liliandika barua
kwenda kwa watahiniwa takriban 3,000 waliokuwa wamejiandikisha kama
watahiniwa binafsi na kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani huo kwa mwaka
huu.
Alifafanua kuwa, baadhi yao walifika Necta wakiwa
na stakabadhi zilizothibitisha kuwa wamelipa karo hiyo na hivyo
kurudishwa kwenye kundi la watakaofanya mtihani huo mwaka huu.
“Necta hatupokei fedha moja kwa moja, tuna
mawakala, kilichotokea ni kuwa baadhi ya watu walilipa karo za mitihani,
lakini kwenye mfumo wetu tulikuwa hatuoni kama walilipa,” alisema na
kuongeza:
“Kwa hiyo watu wote walioandikiwa hizo barua ni
wale ambao kwenye mfumo wetu hawaonekani kama wamelipa, lakini wengi wa
hawa walikuja na risiti zikionyesha kuwa walikuwa wamelipa na
wakarudishwa kwenye mfumo,” alisema. MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment