Wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari
matombo katika wilaya ya morogoro wamejeruhiwa, na wengine watatu
kunusurika, baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu,
wakati wakitoka shuleni.
Wanafunzi hao waliojeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao
ni Luciani Juma (14) na Anthonia Charles (15), wakazi wa kijiji cha
Konde, Tarafa ya Matombo wilayani Morogoro, ambapo Luciani aliyelazwa
katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu, ameiambia
itv kuwa walipatwa na tukio hilo wakati wakitokea shuleni, ambapo njiani
walikutana na kitu mfano wa balbu ya tochi ambacho hata asubuhi wakati
wa kwenda shule walikiona na kukipuuza, na mmoja wawanafunzi
alikirushia ganda la muwa aliokuwa akila, na kililipuka na kutoa mshindo
mkubwa.
Daktari anayemtibu Lucien katika wadi namba moja ya hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Morogoro, aliyejulikana kwa jina moja Dk. Francis
amesema majeruhi huyo anaendelea vizuri, na amepata majeraha katika
sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo sehemu za siri, kwenye paja na
sehemu ya nyonga na kwamba katika maeneo hayo walifanikiwa kutoa vitu
mfano wa chuma.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro John Laswai, amethibitisha
kujeruhiwa kwa wanafunzi hao, ambapo majeruhi Anthonia ametibiwa na
kuruhusiwa na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini kitu
kilichowajeruhi wanafunzi hao, ambacho kilitoa mshindo mkubwa na
mtawanyiko wa vyuma, kama kilikuwa ni bomu ama vinginevyo.
SOURCE:ITV
0 comments :
Post a Comment