Hali imeendelea kuwa
tete ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), huku
jumuiya hiyo ikitengua uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao
walikataliwa na Baraza Kuu la chombo hicho lililokutana hivi karibuni,
Visiwani Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea
kuna na taarifa kwamba kumekuwa na mwendelezo wa harakati za kuandaa
mkakati wa kumwondoa madarakani mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sadifa Juma
Khamis na kwamba vikao vya kupanga mkakati huo vilianza mara tu baada ya
mkutano wa Zanzibar.(P.T)
Watendaji
waliosimamishwa ni Wakuu wa Idara za Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege,
Fedha na Uchumi, Omary Suleiman na yule wa Idara ya Chipukizi na
Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu Mkuu wa UVCCM,
Sixtus Mapunda alilithibitishia gazeti hili kung'olewa kwa watendaji hao
na kwamba kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo
watathibitishwa na Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma
Oktoba mwaka huu.
"Sisi tuliomba hawa
wathibitishwe kwenye kikao kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo mkanganyiko
wajumbe wakataka tujadili suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita
lakini kwa kuwa tulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu
tukaomba suala hili lisogezwe mbele," alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari
watendaji hao walikuwa wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni
kujikanganya, wameona ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano
ujao.
"Kuna kanuni inayotoa
mamlaka kwa Kamati ya Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo
inabidi sasa tuweke kwanza mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba,
hawa watathibishwa," alisema.
Hata hivyo habari ambazo
zimelifikia gazeti hili zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara
kurejea kwenye nafasi zao, kwani kitendo cha wajumbe kuwakataa katika
kikao cha Zanzibar kinathibitisha kwamba hawana imani nao.
"Kama wajumbe wa Baraza
Kuu wangekuwa wanawaamini, shinikizo lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini
sisi wajumbe ni kwamba hatuwataki. Inabidi Sadifa na kamati yake ya
utekelezaji watuteulie watu wengine," alisema mmoja wa viongozi wa UVCCM
wa mikoa ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi wa wakuu
wa idara za UVCCM pia ni mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya,
Mapunda ambaye mara baada ya kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro
katika taasisi ambayo yeye ni mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa
vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo,
Mapunda anaweza kujikuta katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa
Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha majina ya watu walewale waliong'olewa ili
wapigiwe kura kwa ajili ya kuthibitishwa.
Vikao vya Siri
Habari kutoka katika
mkutano wa Zanzibar zilisema kuwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya
baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Kinana alinukuliwa
akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara hivyo
alishauri suala hilo lipangwe kuzungumzwa katika mkutano wa Oktoba
utakaofanyika Dodoma.
Baada ya mkutano wa
Baraza Kuu, baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wa mikoa, waliripotiwa
kuendesha vikao vya siri katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es
Salaam, huku kundi kubwa likitajwa kupanga mikakati ya kuhakikisha
Sadifa anang'oka.
Miongoni mwa hoja
zinazojengwa dhidi ya mwenyekiti huyo ni pamoja na hiyo ya ukiukwaji wa
kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara, hasa Ibara ya 91 ya toleo la nane la
Kanuni za Umoja huo kwa kuwatangaza kabla ya kuundwa kwa Kamati ya
Utekelezaji ambayo alipaswa kushirikiana nayo, kabla ya kuridhiwa na
Baraza Kuu.
Wajumbe wengi watatumia
kusimama kazi kwa watumishi hao kama hoja ya kuthibitisha kuwapo kwa
makosa ya kiutendaji, hivyo watahoji iwapo kuna sababu za UVCCM
"kuendelea kuwa na mwenyekiti ambaye hawezi kuzingatia kanuni na
miongozo katika utendaji wake".
Tuhuma nyingine ambazo
zimekuwa zikizungumzwa dhidi ya Sadifa ni matumizi mabaya ya fedha za
Umoja huo pamoja na kukodi walinzi binafsi watano; wawili Tanzania Bara
na watatu Zanzibar, ambao wamekuwa wakilipwa na UVCCM.
Jana Sadifa alipotafutwa
kuzungumzia tuhuma hizo mpya alisema: "Hayo masuala mimi bwana
siyataki, chochote unachopewa wewe andika unavyojua".
Aliongeza:"Ukiwa na
issue (suala) yoyote inayohusu Umoja wa Vijana, wewe mtafute Katibu
Mkuu, hata kama hayo mambo yananihusu mimi, wewe usinitafute mimi,
mtafute Katibu Mkuu yeye nimempa mamlaka ya kuwa msemaji mkuu."
Naye Mapunda alipoulizwa
kuhusu tuhuma dhidi ya bosi wake alisema hawezi kuzungumzia matumizi
mabaya ya fedha kwani hana taarifa.
"Tangu niteuliwe
sijamaliza hata siku saba, kwa hiyo niwe muwazi tu kuwa sina taarifa
nayo na sasa siwezi kusema fedha zilivyotumika," alisema Mapunda.
Kuhusu suala la walinzi
(mabaunsa),Mapunda alisema hao si sehemu ya watumishi aliokabidhiwa na
kwamba jumuiya hiyo haina waajiriwa wa aina hiyo.
Chanzo:mwananchi
0 comments :
Post a Comment