WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya 
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameweka wazi utetezi wa Tanzania katika 
mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Malawi.
Akizungumza na wahariri wa habari 
katika semina ya ardhi Dar es Salaam jana, Profesa Tibaijuka alisema 
tayari Rais Jakaya Kikwete ametoa ushahidi wa mpaka huo katika Kamati ya
 Marais Wastaafu, Festus Mogae wa Botswana, Joachim Chisano wa Msumbiji 
na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.
Katika ushahidi huo, kwa mujibu wa 
Profesa Tibaijuka, Tanzania ilitumia zaidi historia ya ugawaji mipaka 
ilivyokuwa na kutumia ushahidi wa nyaraka za serikali za kikoloni, 
zilizoshiriki kugawa mipaka ya Afrika.
Profesa Tibaijuka alisema mipaka ya nchi 
iliwekwa mwaka 1890 katika Mkataba wa Wajerumani waliokuwa wakitawala 
Tanganyika kwa kutumia hadithi za wagunduzi waliotangulia Afrika, kabla 
ya Wakoloni kuanza kugawana bara hilo.
Wakati huo kwa mujibu wa Profesa 
Tibaijuka, mpaka kati ya Tanganyika na Kongo na hata Malawi, ulikuwa 
Mashariki ya Ziwa na hivyo hata Ziwa Tanganyika, lilipaswa kuwa Kongo.
Alifafanua kuwa katika upimaji, baada ya 
kufanya uamuzi huo wa watawala, hatua ya pili ilikuwa kuunda tume kwenda
 kuhakiki mpaka huo kwa kuzungumza na wenyeji, na kuurekebisha kwa 
kufuata taarifa za wenyeji. Mwaka 1898 tume hizo zikaundwa, na matokeo 
yake mipaka Ziwa Tanganyika, Mto Songwe na hata Ziwa Victoria ikawekwa 
katikati.
Kwa bahati mbaya, mwaka 1914 Vita ya 
Kwanza ya Dunia iliibuka na kusababisha tume hizo kusimama kazi kabla ya
 kupita na kuthibitisha mpaka katika Ziwa Nyasa. Profesa Tibaijuka 
aliendelea kuanika ushahidi huo, kwamba baada ya vita ya dunia, 
Ujerumani ilishindwa na kupoteza makoloni yake ambayo yalichukuliwa na 
League of Nations ikiwamo Tanganyika ambayo ilitolewa kwa Uingereza kama
 mwangalizi.
Tanzania imethibitisha katika ushahidi 
wake kuwa, kitendo cha Uingereza kupewa Tanganyika kuwa mwangalizi huku 
Malawi ikiwa koloni lake, kilisababisha tume hiyo kutoendelea na kazi, 
kwa kuwa hakukuwa na umuhimu wa mpaka, wakati mtawala wa Malawi na 
Tanganyika akiwa mmoja.
Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, 
Uingereza ilikuwa ikipeleka taarifa za uangalizi mara kwa mara League of
 Nations na kabla ya uhuru miaka ya 1950, Gavana wa Tanganyika alipeleka
 taarifa kutaka tume ifanye kazi yake kuhusu mpaka.
Profesa Tibaijuka alisema taarifa hizo 
ziko Geneva, Umoja wa Mataifa, na ujumbe wa Tanzania ulilazimika kwenda 
kupekua katika maktaba ya Umoja huo kupata vielelezo vya taarifa za 
Uingereza kuhusu mpaka, ambazo zimetumika katika ushahidi.
Ushahidi mwingine Ushahidi mwingine ambao
 Profesa Tibaijuka alisema utaisaidia Tanzania ni makubaliano ya 
kimataifa yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa kuhusu kugawana eneo la maji.
Alisema kwa kufuata makubaliano hayo, haiwezekani watu wa Mbamba Bay, waombe kunywa maji ya Ziwa Nyasa kutoka Malawi.
Source: Habarileo
 
0 comments :
Post a Comment