Shamra
shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani
City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete
alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu
ingawa uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni
waalikwa. Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga
mitambo ndani na nje ya ukumbi huo.
Ulinzi
katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita kiasi ambapo hakuna yeyote
aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi maalumu, hata angeomba kwa
kupiga magoti.
“Hata
sisi tumetoka Bagamoyo hadi hapa tuna undugu kabisa na mkubwa (Rais
Kikwete), lakini wametunyima kwa sababu hatuna kadi,” alilalamika
mwanamke mmoja aliyeongozana na wanaume wawili.
Hakuna
waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo, isipokuwa
waandishi na wapiga picha maalumu wa Serikali ambao walipewa
vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine walioonekana wakipiga picha ni
wanafamilia ambapo watoto wa kiume wa Rais Kikwete, walionekana wakiwa
na kamera huku wamevalia kanzu nadhifu.
Mfanyakazi mmoja wa Ikulu alipomwona
Mwandishi wa gazeti hili, alimfuata na kumwambia kuwa sherehe hiyo ni ya
kibinafsi na haruhusiwi mwandishi yeyote kufanya kitu chochote.
“Tumenyimwa
kuruhusu waandishi kwenye sherehe hii, sawa wewe ni mwandishi lakini
hii ni sherehe binafsi na ya kifamilia, huruhusiwi kupiga picha yeyote,”
alisema mfanyakazi huyo, jina linahifadhiwa.
Hata
hivyo, mwandishi alitumia mbinu kupata picha za maharusi hao pamoja na
matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea ukumbini hapo.
0 comments :
Post a Comment