Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Zanzibar (CUF), Ismail Jussa Landu amesema ikiwa kweli serikali ya umoja ya kitaifa inataka kuonekana kuwa inaheshimu utawala bora na haki za binaadamu itende haki kwa kuwapa dhamana na kuwaachia Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) waliowekwa ndani zaidi mwaka sasa.
Masheikh hao waliwekwa ndani tokea mwezi wa 10 mwaka 2012 bila ya kupewa dhamana kwa madai ya kuhatarisha usalama wa taifa ambapo Mkurugenzi wa Mshtaka Zanzibar (DPP) alitumia kifungu cha sheria ya usalama wa taifa katika kujenga hoja ya kuwanyima dhamana watuhumiwa hayo 10.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliofanyika huko Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Jussa alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimesaini mkataba wa kimataifa wa kuheshimu haki za binaadamu na hivyo inapaswa kuheshimu haki hizo bila ya kubagua.
Alisema katika katiba zote mbili ya Tanzania na ile ya Zanzibar katika kifungu cha 18 cha katiba hizo kinampa mtu uhuru wa kutoa maoni yake na kupokea kwa mujibu wa sheria bila ya kuadhibiwa.
Jussa ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa alisema Masheikh wa Uamsho wamewekwa ndani zaidi ya mwaka sasa bila ya kupewa dhamana wakati sheria inaipa mahakama uwezo wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa wa makosa yote isipokuwa mauaji na uhaini.
“Ikiwa Zanzibar inataka ionekane kwamba inaheshimu haki za binaadamu basi iwape dhamana Masheikh hawa maana hata huko kuwaweka ndani bila hata kuwapa dhamana ni kinyume na haki za binaadamu muda umeshakuwa mwingi wamewekwa ndani bila ya kuzingatia athari za huku katika jamii” alisisitiza Jussa na kuungwa mkono wa wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.
Katika kitu ambacho kinaonekana kuitia doa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Jussa alisema ni huko kuendelea kuwaweka ndani Masheikh hao na kuwanyima dhamana bila wakati sheria inasema huwezi kutiwa hatiani mpaka kuwepo na ushahidi uliokamilika hivyo kuendelea kuwaweka ni kwenda kinyume na sheria ambazo Zanzibar wamezipitisha wenyewe.
“Tunasema wapo watu ambao wanaiba na ushahidi upo lakini hawakamatwi wala hawawekwi ndani na wala hakuna sheria iliyowagusa wapo nje wanatembea bila ya kuchukuliwa hatua yoyote sasa tunasema mahakimu wa mwisho ni wazanzibari wenyewe wakiona hakuna haki inayotendeka kwa Masheikh wao basi wazanzibari wataamua ifikapo 2015” alisema na kushangiriwa na wananchi wengi kwa kupigiwa makofi.
Kauli hiyo ya Jussa imeungwa mkono na aliyekuwa Mkereketwa wa Chama Cha Mapinduzi Mohammed Ahmed Sultan (Eddy Riamy) ambaye ametoa wito kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwapa dhamana Masheikh kwani imekuwa kero kubwa kwa wananchi kila unapopita mitaani.
Mkereketwa huyo ambaye alifuatana na Kamati ya watu sita ya Maridhiano iliyoongozwa na Mzee Hassan Nassor Moyo, alisema kwamba mbali ya kukosekana darsa na kusalisha kwa Masheikh hao lakini pia familia zao zimeathirika kiuchumi na kisaikolojia kutokana na kuwa waume ndio waliokuwa wakitizama familia na sasa kuwekwa ndani kumeathiri familia hizo.
Kauli za kutetewa Masheikh hao zimeonekana kuvuta hisia za wananchi wengi ambapo baadhi yao wlaikuwa wakisema ni wakati mwafaka sasa Serikali kushughulikia kama ni kuwatia hatiani au kuwapa dhamana lakini kuendelea kuwaweka rumande kunawanyima haki zao kikatiba na hakuwatendei haki wao na familia zao.
CHANZO:MUNIRA MADRASA
0 comments :
Post a Comment