MABINGWA
watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara wanatarajia kushuka dimbani
jumapili ya wiki hii kuwakabili maafande wa JKT Ruvu kwenye uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam.
Kikosi
cha Yanga chini ya kocha mkuu, Mhoalanzi Hans Van der Pluijm kimeingia
kambini jana jioni katika Hoteli ya Kiromo, huku kikiendelea kufanya
mazoezi katika Uwanja wa Boko Beach Veterani.
Yanga
waliopo nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 46, pointi 7 nyuma ya
Azam fc wenye pointi 53, watakuwa wanacheza mechi ya raundi ya 23
jumapili, huku wakisubiri kiporo chao dhidi ya Kagera Sugar aprili 9
mwaka huu uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.Mechi iliyopita jijini Tanga, Yanga walipoteza mchezo kwa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao, Mgambo JKT na kuweka rehani ubingwa wao msimu huu.
Yanga
wamebakisha mechi nne na kama watashinda zote watafikisha pointi 58
ambazo Azam fc pekee ndio wataweza kuzifikia kama watashinda mechi zao
tatu zilizosalia.
Hata
hivyo taarifa njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa Mlinda mlango
Deoragtias Munish "Dida" aliyekuwa majeruhi kwa takribani wiki mbili,
ameshapona majeraha na ameungana na wenzake kambini tayari kwa
maandalizi ya mchezo huo.
Mlinda Mlango wa Yanga, Juma Kaseja hajasimamishwa
Katika
hatua nyingine, Yanga kupitia tovuti yao rasmi wamekanusha taarifa
zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba wachezaji wake,
kiungo, Athuman Idd, beki Kelvin Yondani na Mlinda mlango, Juma Kaseja
wamesimamishwa kutokana na timu kufungwa na Mgambo JKT.
“Taarifa
hizo hazina ukweli, wachezaji hao hawajafukuzwa na wapo wanaendelea na
mazoezi pamoja na wenzao”. Alifafanua taarifa ya Yanga.
Pia
Yanga wameviomba vyombo vya kutoa taarifa za ukweli na sio kupotosha
jamii na mwisho wa siku kuwapa usumbufu viongozi kufanya kazi ya
kukanusha.
Mchezo wa jumapili utakuwa mgumu kwa timu zote kutokana na kusimama maeneo mawili tofauti kwenye msimamo wa ligi kuu.
Yanga wapo nafasi ya pili na wanapambana kutetea ubingwa wao walioutwaa msimu huu.
Wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga JKT Ruvu mabao 4-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza mwaka jana.
Haitakuwa
kazi nyepesi kwa Yanga kumfunga aliyekuwa kocha wake msaidizi ambaye
kwasasa ni Kocha mkuu wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro.
Minziro na kikosi chake wapo nafasi ya 9 kwa kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 28 kibindoni.
Kiungo, Athumani Idd `Chuji` (wa pili kulia) hajasimamishwa
Maafande
hao wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa
mabao 3-1 mechi iliyopita dhidi ya Vibonde, Rhino Rangers kwenye uwanja
wa Azam Complex.
Mechi ya jumapili ni muhimu kwao kwasababu wanahitaji zaidi pointi ili kujiweka mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Uzoefu
unaonesha kuwa timu zilizopo katika hatari ya kushuka daraja huwa
zinacheza kwa kujituma zaidi, na ndio maana Mgambo JKT walipambana na
Yanga ndani ya dakika zote 90 na kushinda.
Kwa jicho la harakaharaka, unaweza kuwapa asilimia kubwa Yanga kuwa watashinda mchezo huo, kutokana na mazingira yao.
Kupoteza au kutoa sare kutazidi kuwaweka Yanga mazingira magumu zaidi ya kutetea ubingwa wao.
Matokeo yanayowafaa pekee ni ushindi, kwasababu moto wa Azam fc kueleka kutwaa ubingwa ni mkali sana.
Itakuwa mechi muhimu kwa Yanga, na kocha mkuu Pluijm atahitaji kutuliza akili zake kwani sasa matokeo hayatabiriki.
Haikuwa
rahisi kuamini kama Mgambo wangewafunga Yanga waliokamilika pale
Mkwakwani, lakini mpira una matokeo ya ajabu wakati fulani.
Yanga
wanatakiwa kuingia jumapili kwa tahadhari kubwa kwasababu kiwango cha
sasa cha JKT Ruvu si cha kubeza. Wanaweza kufanya lolote na kuwaharibia
zaidi wanajangwani.
0 comments :
Post a Comment