Bunge la Katiba leo linatarajiwa kuwaka moto upya wakati taarifa za Kamati zitakapoanza kuwasilishwa, huku mvutano mkubwa ukitarajiwa kuwa juu ya muundo wa Muungano.
Katika taarifa hizo, wakati kundi la walio wengi hasa kutoka CCM wakionekana kupania kuifumua Rasimu ya Katiba na kuingiza maudhui ya Serikali mbili katika Sura ya Kwanza na ya Sita zinazohusu Muungano, walio wachache wanaitetea Rasimu na kuchambua kasoro lukuki za Muungano.
Habari kutoka katika kamati hizo, zinabainisha kundi la walio wachache limeandaa hoja nyingi kuliko za walio wengi kwa mfano, katika Kamati Namba Nne inayoongozwa na Christopher Ole Sendeka taarifa ya wengi ina kurasa 13 wakati taarifa za wachache iliyoandaliwa na Tundu Lissu ina kurasa 50.
Uchunguzi umebaini kuwa, taarifa mbalimbali zilizoandaliwa na walio wengi zimejikita katika mapendekezo juu ya Serikali mbili, katika Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba kinyume na mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika mapendekezo hayo, kamati hizo zinaeleza manufaa ya mfumo uliopo, faida zilizopo na athari za kuingia katika mfumo mwingine wa Muungano.
Hata hivyo, wajumbe wa makundi hayo hawakuwa tayari kuzungumzia taarifa zao kwa kina kwa kuwa bado zilikuwa hazijawasilishwa bungeni.
Katika taarifa kinzani, uchunguzi umebainisha kuwa zimeonyesha vielelezo kadhaa, ikiwamo Sheria ya Muungano kutowahi kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali la Mapinduzi Zanzibar.
Gazeti la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar la Januari 25, 1964 halikuwa na taarifa yoyote ya maridhiano ya Muungano tofauti na Gazeti la Tanganyika katika siku hiyo.
Taarifa hiyo pia inataja vielelezo vya tume mbalimbali ambavyo vinapendekeza muundo wa Serikali tatu.
Habari za ndani ya kundi hilo zinadai kuwa, mapendekezo ya kubadili muundo wa Muungano yaliyotolewa na tume mbalimbali za kikatiba pamoja na rasimu yanathibitisha kwamba Muungano umekuwa na migogoro isiyokwisha na ambayo haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa.
Vilevile, kundi la walio wachache linadai kuwa miongoni mwa sababu za usiri katika Muungano ni watawala wa nchi za Afrika Mashariki, hususan waasisi wa Muungano kuwa na hofu ya tawala zao kupinduliwa kutokana na mfano wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Habari zinasema kuwa, kundi hilo la walio wachache linadai kuwa Baraza la Mapinduzi lililokuwa linatawala Zanzibar wakati wa Muungano, lilikataa pendekezo la Muungano na pia halikutunga sheria ya kuridhia Hati za Makubaliano ya Muungano baada ya Sheikh Abeid Karume kuamua kuunganisha Zanzibar na Tanganyika bila ridhaa ya Baraza la Mapinduzi.
Chanzo chetu kinadokeza kuwa, Bunge la Tanganyika liliitishwa kwa dharura siku tatu baada ya kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya Muungano na kutakiwa kupitisha Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar siku hiyohiyo kwa kutumia hati ya dharura.
Kundi hilo linadai kuwa sehemu nyingine kubwa ya migogoro ya Muungano imetokana siyo kwa sababu ya namna ulivyozaliwa, bali na utekelezaji wa masharti ya Hati za Makubaliano ya Muungano.
“Hii ni kwa sababu wakati Muungano umetukuzwa katika majukwaa ya kisiasa, umekuwa ukikiukwa kwa vitendo - hasahasa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakati wote wa historia yake ya karibu miaka 50,” kinaeleza.
Imeandikwa na Mussa Juma, Sharon Sauwa na Editha Majura.
CHANZO NI MWANANCHI
About Omari Makoo
0 comments :
Post a Comment