Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba tano Assumpter Mshama akiwasilisha maoni ya wajumbe wa Kamati yake leo mjini Dodoma juu ya uchambuzi wa sura ya kwanza na sita ya wa rasimu ya Katiba mpya.
KAMATI za Bunge Maalumu la Katiba zimeanza kuwasilisha bungeni maoni yake, kuhusu mijadala ya sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba mpya, huku wengi wakikataa muundo wa serikali tatu, kwa kusema utaibua hisia za ubaguzi kwa wananchi wa taifa moja.
Miongoni mwa kamati zilizowasilisha maoni jana bungeni ni Kamati Namba Tano, ambayo Makamu Mwenyekiti wake, Assumpter Mshama, alisema muundo wa serikali tatu ukipita, utaibua hisia hizo, ambazo hazipati nafasi katika mfumo uliopo wa serikali mbili.
Assumpter alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyesema; “Nje ya Muungano, hakuna Wazanzibari, kuna wao Wapemba na sisi Waunguja…dhambi hii haitaacha kuitafuna Tanganyika ambayo ina makabila mengi.”
Mbali na ubaguzi, walio wengi katika kamati hiyo walielezea hatari nyingine ya muundo unaopendekezwa, utajenga mazingira ya kulisambaratisha Taifa.
“Sura ya 17 ya rasimu inathibitisha kitakachotokea endapo muundo unaopendekezwa utakubaliwa. Mojawapo ya mambo yanayozungumziwa na sura hii ni masuala ya kugawana rasilimali, kugawana watumishi wa umma, madeni na mambo mengine.
“Mambo haya badala ya kuwaleta karibu, inawatenganisha wananchi wa pande mbili za Muungano…kwa mnasaba huu, muundo wa serikali mbili ndio ulioafikiwa na wajumbe wengi kuwa unalifaa taifa letu kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama ya wananchi wa pande mbili,” alisema.
Kuhusu kero za Muungano zinazodaiwa kudumu kwa miaka 50 na kuwa kichocheo cha kupendekezwa kwa serikali tatu, walio wengi katika Kamati hiyo walisema changamoto hizo wanazitambua na jitihada zinafanyika kuzikabili.
“Walio wengi wanaamini kuwa muundo wa serikali tatu hautakuwa suluhisho badala yake utaibua changamoto nyingine nyingi. Mchakato huu ni fursa kubwa na ya pekee kuzishughulikia changamoto hizi kwa mapana yake. “Mapendekezo yaliyotolewa na walio wengi, yanalenga kuzipa jitihada hizi kinga za kikatiba na kisheria ili ufumbuzi wake uwe endelevu,” alisema Assumpter.
Kutokana na hoja hizo, Assumpter alisema walio wengi wanapendekeza katika Sura ya Sita, Ibara ya 60 (1), irekebishwe na kusomeka “Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa serikali mbili ambazo ni: “Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wajumbe wengi pia katika Kamati hiyo, wamependekeza kuwepo kwa viongozi wakuu wenye mamlaka ya utendaji katika Jamuhuri ya Muungano waliotajwa katika Ibara ndogo ya (3), ambao watawajibika kila mmoja wao katika kutekeleza madaraka waliyopewa kuhakikisha wanalinda, wanaimarisha na kudumisha Muungano.
Viongozi wakuu hao ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tanganyika kufufuliwa?
Kamati hiyo Namba Tano, walio wengi wamependekeza kabla ya Rasimu ya Katiba kupitisha muundo wa serikali tatu, ni lazima nchi inayoitwa Tanganyika iwepo kwanza na kupewa mamlaka yake, kisha iamue inataka Muungano wa aina gani.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mshama alisema rasimu ya Katiba inapendekeza muundo wa serikali tatu zitakazotokana na Muungano wa nchi mbili, lakini hivi sasa Tanganyika inayopendekezwa kama nchi mshirika haipo.
Alifafanua Tanganyika haipo kwa kuwa mamlaka, uendeshaji na masuala yake yote yalikwishakabidhiwa kikatiba na kisheria katika nchi inayoitwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1964.
“Hivyo kama kuna shirikisho linapendekezwa basi ni lazima kwanza nchi hiyo inayoitwa Tanganyika iwepo, iwe na Katiba yake na vyombo vyote vya utawala ili iweze kuwa na mamlaka ya kuamua kama inataka Muungano. “Muungano wenyewe wa aina gani na kama ni shirikisho, basi Tanganyika iamue kwa msingi wa kuyakubali masharti ya shirikisho linalopendekezwa. Hilo likifanyika Hati ya Makubaliano iliyopo na ambayo ndiyo inayotajwa na Rasimu ya Katiba, itabaki kuwa waraka wa kihistoria,” alisema Assumpter.
Kamati Namba 2
Mwenyekiti wa Kamati Namba Mbili, Dk Shamsi Vuai Nahodha, alisema katika ibara ya kwanza inayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe walikuwa na mjadala mkali kuhusu maana ya maneno Muungano na Shirikisho, ambayo ufafanuzi wake ulitolewa.
Alisema Muungano ni makubaliano ya zaidi ya nchi moja, kuunda dola moja yenye nguvu, ambapo majukumu ya msingi ya nchi hizo yanakabidhiwa kwenye Serikali ya Muungano.
Alisisitiza Muungano wa Tanzania ni makubaliano kati ya Tanganyika na Zanzibar, ambapo Tanganyika ilikabidhi madaraka yake yote kwa serikali ya Muungano na Zanzibar ilikasimu baadhi ya madaraka yake kwa serikali ya Muungano.
Kwa upande wa Shirikisho, Dk Nahodha alisema Shirikisho ni makubaliano ya nchi mbili au zaidi, zinazounda Serikali moja chini ya kiongozi mmoja, lakini kwa muktadha wa rasimu ya Katiba iliyopo, Shirikisho linalozungumziwa litakuwa na serikali tatu na Marais watatu.
Alisema baada ya ufafanuzi wa kina, wajumbe walifanya uamuzi katika Ibara ya Kwanza wajumbe wengi ambao hawakufikia theluthi mbili walipendekeza neno Shirikisho lifutwe kwa sababu tatu; Kwanza, hati ya makubaliano ya Muungano inazungumzia kuwepo kwa serikali mbili yaani serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Hata Rasimu ya Katiba katika Ibara 1 (3) inatambua hati ya Muungano kama msingi na mwendelezo wa makubaliano hayo,” alisema Nahodha.
Alisema sababu ya pili ni Hati hiyo ya Muungano mpaka sasa haijafutwa na wala haijabadilishwa na tatu, Shirikisho la Serikali tatu linalopendekezwa katika rasimu, litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa eneo la Bahari ya Hindi lenye rasilimali nyingi ambazo mataifa makubwa wanaziwania.
“Udhaifu huu utayapa mwanya mataifa hayo kuzirubuni nchi washirika zisichangie gharama za kuendesha serikali ya shirikisho hasa tukizingatia kuwa serikali ya Shirikisho haina vyanzo vya uhakika vya mapato na endapo jambo hili litatokea Shirikisho litadhoofika na hatimaye kuvunjika.”
Msingi wa Muungano
Akizungumzia Sura ya Sita, inayozungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano alisema wajumbe walijadili na kuchambua na kukubaliana kwamba Muundo wa Serikali Mbili, kama ulivyoanishwa katika hati ya Muungano, ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema hata hivyo baada ya kupiga kura kwa ajili ya kupata uamuzi, theluthi mbili ya upande wa Tanzania Bara haikupatikana. Alisema ingawa theluthi mbili haikupatikana, wajumbe wengi kutoka pande zote, walipendekeza kwamba Ibara hiyo ifanyiwe marekebisho.
Alisema kutokana na marekebisho hayo; Ibara ya 60 (1), itasomeka; “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa serikali mbili ambazo ni (a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano na (b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ibara ya 60 (2) sasa itasomeka kwamba “Shughuli za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitatekelezwa na kusimamiwa na (a) vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, (b) vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na (c) vyombo viwili vyenye mamlaka ya utoaji haki. Hoja kinzani Akisoma maoni kinzani, Dk Nahodha alisema katika mjadala huo baadhi ya wajumbe walikuwa na mtazamo hasi hususani neno Shirikisho lilipotumika.
Kwa mujibu wa Nahodha, baadhi walisema wajumbe walio wengi walidhamiria kwa kiwango kikubwa kuleta marekebisho ama nakala ya rasimu yao ya siri ili kubadili kiini cha rasimu rasmi, ambayo kimsingi ni maoni na mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
0 comments :
Post a Comment