Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, kimeshindwa kufanyika baada ya kuzuka mabishano makali baina ya mstahiki meya na madiwani wa CHADEMA.
Tukio hilo lilitokea Alhamisi asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, baada ya meya, Henry Matata, kuwataka madiwani watatu anaodai kufukuzwa watoke nje kwa maelezo kwamba si wajumbe halali wa baraza hilo.
Madiwani wanaodaiwa kufukuzwa na Matata ni Marietha Chenyenge wa Kata ya Ilemela, Abubakar Kapera wa Kata ya Nyamanoro pamoja na wa Kata ya Kirumba, Dany Kahungu wa CHADEMA watoke.
Kutokana na amri hiyo ya Matata, madiwani hao waligoma kutoka nje ya ukumbi huo, kwa madai kwamba wao ni halali kwa Baraza la Halmashauri ya Manispaa hiyo na kwamba walifukuzwa kinyume cha taratibu na sheria za nchi.
Matata aliyechaguliwa na madiwani sita kati ya 14 wa manispaa hiyo, hivyo kushindwa kukidhi akidi ya theluthi mbili za wajumbe halali, alitangaza kuwafukuza madiwani hao miezi tisa iliyopita kwa tuhuma za kutohudhuria vikao vitatu mfululizo vya baraza bila taarifa.
Malumbano hayo makali baina ya meya na madiwani Chenyenge na Kapera, yalizuka kabla ya kikao kufunguliwa.
Matata aliomba msaada wa askari polisi kuwatoa madiwani hao, lakini hawakuweza kutekeleza amri hiyo.
Baada ya kuona askari polisi wameshindwa kuchukua hatua hiyo, Matata alieleza kutoridhishwa kwake na hatua hiyo, huku akitishia kuwatumia vijana wake mabaunsa ili kuwaondoa madiwani hao ukumbini.
Wakati hayo yakijiri, tayari madiwani hao walikuwa wameshavaa majoho yao ya kushiriki kikao cha Baraza la Madiwani na kuketi kwenye viti miongoni mwa madiwani wengine kadhaa.
Katika maelezo yake, Matata alisema: “Madiwani hawa hawana uhalali wa kushiriki kikao hiki kwa kuwa nilishawafukuza. Na kitendo cha kulazimisha kushikiri ni sawa na kufanya vurugu.”
Baada ya mabishano yaliyodumu kwa takribani dakika 20, Matata alisimama na kufungua kikao hicho, na muda huo huo akakiahirisha akidai hakiwezi kufanyika bila madiwani hao kuondolewa ukumbini.
Wakizungumzia hali hiyo, madiwani hao walisema wamelazimika kuhudhuria kikao hicho bila mwaliko, baada ya kuona wamesimamishwa muda mrefu kinyume cha kanuni za uendeshaji wa serikali za mitaa, huku maendeleo ya wananchi yakidhoofika katika kata zao kutokana na kukosa usimamizi wao..
0 comments :
Post a Comment