SASA WAUZA MADAWA JELA MIAKA 30 NA FAINI YA SHILINGI BILIONI MOJA
BUNGE limepitisha rasmi Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya wa mwaka 2014, huku adhabu ya kifo kwa watakaokutwa na dawa hizo, ikishindikana kuingizwa kwenye muswada huo, isipokuwa mapapa na vigogo wa biashara hiyo, wameongezewa adhabu ya faini ya Sh bilioni moja na kifungo cha maisha.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge bado wameendelea kung’ang’ania kuwa sheria hiyo ijumuishe adhabu hiyo kali ya kifo kwa wafanyabiashara, mapapa au vigogo wanofadhili biashara hiyo, kwa kuwa madhara ya dawa hizo ni makubwa na yanaathiri zaidi vijana ambao ni nguvukazi ya nchi.
Akitoa majumuisho ya michango ya wabunge kuhusu hoja ya muswada huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama, alisema adhabu ya kifo haiwezekani kuingizwa kwenye sheria hiyo, kwa kuwa adhabu hiyo nchini iko kwenye makosa mawili pekee.
“Ni kweli Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo bado zinatoa adhabu ya kifo, lakini kwa mujibu wa sera iliyopo, adhabu ya kifo imeingizwa na kubainishwa kwenye makosa ya uhaini na mauaji pekee,” alisema Mhagama.
Alisema makosa hayo ndiyo yaliyotafsiriwa kwenye sera hiyo na kwamba hadi sasa, Tanzania haijafanya mchakato wowote wa kuingiza makosa mengine katika adhabu hiyo ya kifo kwa kunyongwa hadi kufa.
Aidha alisema kwa muda mrefu nchini kumekuwepo na mijadala juu ya kuwepo kwa adhabu hiyo kutoka kwa wanaharakati kwamba inastahili iwepo au la.
“Itakuwa ngumu mimi leo kukubali adhabu hii iingizwe kwenye sheria bila kufuatwa kwa mchakato wa kuongeza dawa za kulevya kwenye sera.”
Alisisitiza kuwa adhabu iliyopendekezwa katika muswada huo ya kifungo cha maisha ni kubwa.
“Ila naomba tuendelee kuwa wakali,wabunge na wananchi wanaodai wana orodha za wauza unga zipelekeni kwenye vyombo husika ni kosa kukaa na orodha hizo.”
Katika kupitishwa vifungu vya muswada, baadhi ya wabunge walipendekeza eneo la adhabu kwa wanaofadhili biashara hiyo ya dawa za kulevya, liongezewe zaidi adhabu ambayo ni faini ya Sh bilioni moja na kifungo cha maisha badala ya kutozwa faini ya Sh bilioni moja au kifungo cha miaka 30 kama ilivyokua awali kwenye muswada huo.
Waziri asiye na Wizara Maalumu, Mark Mwandosya, alisema wafadhili wa dawa hizo, ndio wafanyabiashara wakubwa wanaojulikana kama mapapa hivyo faini ya Sh bilioni moja ni sawa na fedha ya mboga kwao hivyo adhabu ya kifungo cha maisha ndio inayostahili kwao.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya, ambaye awali alipendekeza mapapa hao wanyongwe, alisisitiza ni vyema wakapewa adhabu ya kifungo na faini ya Sh bilioni moja ili iwe fundisho kwa wengine.HABARILEO
0 comments :
Post a Comment