PROFESA Ibrahim Lipumba-Mwenyekiti wa
Chama cha Wananchi (CUF), ni miongoni mwa wasomi wa ndani na nje ya nchi
walioalikwa kutoa mada katika uzinduzi wa Chama cha ACT-Tanzania tarehe
29 Machi mwa huu. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa habari wa
ACT, Abdallah Khamis uzinduzi huo utaanza saa tisa alasiri, ambapo
Prof. Lipumba, atazungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani nchini kuhusu
‘kwanini Tanzania bado ni nchi masikini na nini cha kufanya kuondoa
umasikini’.
Khamis anasema, “pia viongozi wote wa
vyama vya siasa nchini, mabalozi wa nchi mbalimbali na wakuu wa asasi
zisizo za kiserikali wamealikwa”.
Viongozi wengine walioalikwa ni Samia
Nkrumah, Kiongozi wa Chama cha CPP cha Ghana na mtoto wa Rais wa kwanza
wa Ghana Osagyefo Kwame Nkrumah, Ababu Namwamba-Katibu Mkuu wa Chama cha
ODM cha Kenya na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wa
Jamhuri ya Kenya.
“Vile vile ACT – Tanzania inatarajiwa
kupata wageni kutoka vyama rafiki vya Ujerumani Die Linke na Umoja wa
vyama vya mrengo wa kushoto Progressive Alliance.
“ACT-Tanzania kitafanya mkutano wake mkuu
na uzinduzi wa chama mnamo tarehe 28 na 29 Machi 2015. Katika mkutano
Mkuu chama kitapitisha katiba mpya ya chama na kufanya uchaguzi,”
amesema.
Khamis ameongeza kuwa, viongozi
watakaochaguliwa ni Kiongozi wa chama, Mwenyekiti, Makamu wenyeviti,
Katibu Mkuu na Manaibu makatibu wakuu. Pia chama kitachagua wajumbe wa
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
“Baada ya uzinduzi, ACT- Tanzania
itafanya mikutano ya hadhara nchi nzima kwa kuanzia na mikoa ya Arusha,
Shinyanga, Tabora, Kigoma na Mbeya,” amesema Khamis.
0 comments :
Post a Comment