-->

HII HAPA HOTUBA YA ZITTO KABWE ALIYOISOMA KWENYE UZINDUZI WA CHAMA CHA ACT TANZANIA


 katika uzinduzi wa ACT Tanzania.29.03.2015
Watanzania wenzangu, wageni waalikwa
Nawashukuru kwa kuwa pamoja nasi siku hii ya kihistoria.
Karibu Miaka 54 iliyopita tulipopata uhuru, Muasisi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 39, mwenye matumaini makubwa na taifa jipya na alikuwa na ndoto! Ndoto yake ilikuwa imejikita katika kuhakikisha taifa letu litakuwa taifa lisilo na umaskini, dhiki, ufukara; taifa lisilo na tofauti kubwa kati ya maskini na tajiri; taifa lenye usawa, haki na maendeleo, ambapo watoto wote wanasoma shule bila kujali kipato cha mzazi; taifa ambalo wananchi wake wanamiliki uchumi wao.
Ndoto hii aliiamini kwa dhati na wananchi wote walikubali na kuota nae ndoto hii. Alilisimamia kwa maneno na vitendo kupitia Azimio la Arusha, sera zake na uongozi wake wa kizalendo. Mpaka mauti ilipomkuta aliamini katika misingi hii aliyojitahidi kuturithisha. Lakini miaka 16 baada ya kifo chake, ndoto yake imeyeyuka!
Tulilonalo ni jinamizi alilolihofu Nyerere.
Leo hii:
Watanzania wachache wameondoka katika unyonge na dhiki.
Watanzania wengi bado wapo katika hali ya dhiki.
Watanzania wachache wameshikilia uchumi: Warasimu, Wanasiasa na Matajiri wachache wenye mitaji.
Watanzania wengi bado kama Mwalimu Nyerere alivyosema “wananyonywa kiasi cha kutosha; wanapuuzwa kiasi cha kutosha”.
Ndoto ya Mwalimu Nyerere bado haijawafikia wananchi.
Sasa ndio wakati wa mabadiliko ya kimapinduzi.
Sasa ndio wakati wa kujenga Uchumi shirikishi ambao utaruhusu kila mwananchi kupata fursa ya kuboresha maisha yake;
Sasa ndio wakati dola imara ipate nafasi ya kusimamia uchumi;
Sasa ndio wakati kwa wananchi kuwa na uhuru wa kweli wa mawazo, fikra, kushirikiana, kuabudu;
Sasa ndio wakati wananchi kuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao;
Sasa ndio wakati wetu watanzania kujirithisha upya nchi yetu!
Huu ndio wakati wa kubomoa uchumi wa kinyonyaji na kifisadi na kujenga uchumi wa wananchi. Haya ndio mabadiliko ya kimapinduzi tunayoyataka. Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere, na muda umefika wananchi turejeshe nchi mikononi mwetu!
Haya yamekuwa mawazo yangu kwa muda mrefu kwa sababu mimi ni zao la ndoto ya Mwalimu Nyerere. Nililelewa na mama yangu mzazi pekee mwenye ulemavu; nimeanza kusoma shule ya msingi nikiwa naenda peku. Lakini kutokana na kufaulu mitihani vizuri, sikuhitaji kuwa tajiri kusoma mpaka chuo kikuu. Leo hii kutokana na elimu bora niliyoipata bure, nimesafiri na kufika katika nchi zaidi ya 70; nikiwa kama kiongozi nimekutana na kubadilishana mawazo na watu muhimu duniani kama vile wakuu wa nchi. Sio mimi peke yangu bali tupo maelfu tuliofaidika na mfumo huu. Lakini muhimu kupita yote, nimeweza kutumikia wananchi wa Kigoma na watanzania bungeni kwa miaka 10. Kama hii si ndoto iliyokuja kuwa kweli, ni nini?
Zitto Zuberi Kabwe angezaliwa mwaka 2000, angekuwa kijana ambaye hajakamilisha elimu yake, haelewi lugha za kigeni kama kiingereza, hana ujuzi wowote na kama Mungu angeendelea kuninyima kipaji cha kuimba kama sasa ningeshindwa hata kutoka kama Diamond na Mwana FA! Mwalimu Nyerere asingepigania ndoto yake miaka ya 60 na 70, ningekuwa kama mamilioni ya vijana leo ambao wanahangaika kutafuta ajira na kipato bila ujuzi na elimu.
Na ndiyo maana siku ya leo ni muhimu kwangu. Nina furaha na heshima kubwa kuwa katika familia yangu mpya ya kisiasa. Familia inayoaamini katika itikadi, misingi na tunu ninazoziamini.
Nimezungumza mara kadhaa kuhusu sababu za kujiunga na chama hiki. Chama cha Wazalendo ACT- Tanzania inaongozwa na misingi ya Uzalendo, Demokarsia, Uhuru wa fikra na matendo, Utu, Usawa, Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji na Umoja katika kila kitu. Chama hiki ni cha wananchi si wenyenchi wa sasa waliojimilikisha taifa. Chama hiki ni cha watanzania wote bila kujali kabila, dini, jinsia, rangi ya ngozi au hali ya ulemavu!
Tunapojadili wananchi kujimilikisha upya nchi yetu ni kupitia usimamizi wa sheria utakaohakikisha kuwa kuna uwazi na uwajibikaji wa viongozi. Uwazi tunaouamini ni ule utakaohakikisha kila mwananchi anapata taarifa za fedha zao, mikataba ambayo Serikali inaingia kwa niaba yao na taarifa za maslahi, mali na madeni ya viongozi wao. Tunataka uwazi katika uendeshaji wa Serikali na sisi tutaanza na uwazi katika uendeshaji wa chama chetu. Tunataka wananchi sio tu wajione kuwa sehemu ya uendeshaji wa nchi yao, bali pia wawe sehemu ya uendeshaji wa nchi yao.
Tunataka uwazi utakaoruhusu uhuru wa mawazo na uhuru wa wananchi kujieleza bila kuhofu Serikali kuwachukulia hatua kwa kutoa mawazo yao. Ndio maana ACT Wazalendo tunapinga vikali miswada ya sheria ambayo Serikali ya CCM imeiwasilisha bungeni katika mkutano unaoendelea. Miswada hii kama vile muswada wa Haki ya kupata taarifa, vyombo vya habari na ule wa makosa ya mtandao, inalenga kuminya na kunyima haki za wananchi kuwasiliana kwa uhuru na kutoa mawazo yao kama inavyoainishwa katika katiba ya nchi.
Tunapojadili wananchi kurejesha taifa mikononi mwao tunazungumzia uwajibikaji. Ripoti ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ilieleza moja ya sababu kubwa ya kushamiri rushwa, ufisadi na ubadhirifu nchini ni nanukuu ‘kukosekana kwa mfumo madhubuti wa uwajibikaji’ nchini kwetu. Sababu kubwa ya ACT Wazalendo kupinga Katiba inayopendekezwa ni kwamba Katiba hiyo imechakachua nia hii ya kuweka mfumo wa uwajibikaji. Ndio maana tunawaambia wananchi waikatae Katiba hiyo kwa nguvu zao zote! Katiba inayoepndekezwa inastahili kadi nyekundu, tuikatae na kura ya hapana!
Iwapo wananchi hawawezi kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao hatuwezi kujenga jamii ya watu wanaoheshimiana na kutii sheria za nchi.
Kila Mtanzania bila ya kujali cheo chake ni lazima awe chini ya sheria. Uwajibikaji ni lazima uanze na viongozi. Mnajua kuwa katika maisha yangu ya kisiasa hili ndio limekuwa jukwaa langu. Kwa bahati mbaya tunaishi katika kipindi ambacho wanasiasa wengi wamekuwa wakikumbwa na kashfa mbalimbali za kifisadi na matokeo yake inajengwa picha kuwa kila mwanasiasa ni fisadi. Mfumo wa Uwajibikaji wenye uwazi utasaidia wananchi kutofautisha wanasiasa wanaosimamia maslahi ya umma na wale wanaosimamia maslahi yao binafsi na vyama vyao vya siasa.
Mwungwana ni vitendo; nimewajibisha watu kwenye Buzwagi na mikataba ya madini, kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma na juzi juzi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Lakini matukio haya machache hayatoshi kujenga mfumo madhubuti wa Uwajibikaji. Ni lazima kufanya mapinduzi ya mfumo mzima wa uchumi wa nchi yetu na kujenga mfumo mpya unaohudumia kila Mtanzania na ambao kila Mtanzania anajivunia kuujenga. Hatuwezi kuwa Taifa linaloshikiliwa na vikundi vya wafanyabishara wachache na wanasiasa wanaofadhiliwa na wafanyabishara hao.
ACT Wazalendo inataka kujenga Taifa ambalo viongozi wake wanawajibika kwa wananchi. Hii ndio fikra tunayotaka kurejesha. Hizi ndizo siasa zilizoasisi Taifa letu. Hatuna budi, ni lazima kurudi kwenye misingi na kuanza upya!
Kwa sababu ACT Wazalendo imejikita kwenye misingi hii, tumelihuisha Azimio la Arusha.
Sio tu tumeweka miiko ya uongozi lakini pia tumetunga kanuni za kutekeleza miiko hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya Katiba ya chama chetu. Hitaji moja kubwa la Kanuni zetu za Maadili ni kutaka kila Kiongozi wa ACT Wazalendo kuweka hadharani Maslahi yake, Mali na Madeni yake.
Katika chama hiki huo ndio utamaduni wa kisiasa tunaotaka kuujenga. Kutenda tunachohubiri hata kabla ya kuingia kwenye uongozi wa Dola.
Chama cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila Kiongozi wa chama lazima atangaze Mali zake na Madeni yake. Kila Kiongozi lazima aweke wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala husika. Viongozi wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze matakwa haya ya kikanuni.
Fomu hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye Miiko ya Uongozi inamtaja anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015. Tunapopinga Viongozi wa Umma kufanya Biashara na Serikali na hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga Viongozi wa Chama chetu kufanya Biashara na Chama. Ni Marufuku Serikali kugeuzwa kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za Umma. Uadilifu tunaoutaka Serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.
Tutafanya haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu wananchi; Wakulima, Wafanyakazi, Wafanyabiashara ndogo ndogo, Vijana, Wanawake na Wazee wetu.
Tunataka kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi. Sio kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao wenyewe.
Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi.
Tanzania inapoteza 15% ya makusanyo katika forodha kwa sababu ya ukwepaji wa kodi. Hii ni sawa na tshs 490 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zingeweza kuchangia wananchi milioni 4 kwenye hifadhi ya Jamii. Tanzania inapoteza takribani tshs 2 trilioni kila mwaka kwenye misamaha ya kodi. Hii ni fedha ambayo ingeweza kujenga reli mpya ya kati ya kisasa kutoka Dar mpaka Mwanza na Kigoma ndani ya miaka mitatu. Ili kuondoa upotevu huu ni lazima kupanua wigo wa kodi, kurahisisha kodi, kupunguza baadhi ya kodi kama ( PAYE) na kutumia teknolojia kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.
Vile vile ni muhimu kuimarisha mfumo wetu wa kodi za kimataifa ili kuzuia utoroshaji mkubwa unaofanywa na makampuni ya kigeni. Ili tujitegemee kama Taifa ni lazima kukusanya mapato ya ndani ya kutosha. Ili kukusanya mapato ya ndani ya kutosha ni lazima kuweka mazingira mazuri ya biashara hasa kwa wafanyabishara ndogo ndogo kwani ndio wazalishaji wakubwa wa ajira.
Kwa Vijana, Taifa hili ni lenu. Asilimia 75 ya Watanzania wapo chini ya miaka 40. Asilimia 65 ya wapiga kura wapo chini ya miaka 40. Nusu ya Watanzania ni watoto chini ya miaka 18. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kujenga maisha yenu. Haikubaliki Vijana kuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu tu uchumi hauzalishi ajira za kutosha. ACT Wazalendo ndio jukwaa lenu la kufanya mapinduzi ya mfumo wa uchumi ili kujenga uchumi shirikishi unaozalisha ajira. ACT Wazalendo inataka kuwajengea mfumo wa hifadhi ya jamii ambapo mtakapokuwa Wazee msipate tabu za pensheni na matibabu wanazopata Wazee wetu hivi sasa. Shiriki kujijengea Taifa litakalohakikisha maisha yako ya sasa nay a baadae na ya kizazi kijacho.
Kwa Wanawake, Ninyi ndio mhimili wa Taifa hili, wazalishaji wakuu na walezi wa Taifa letu. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kutambua nafasi yenu stahili katika jamii. Nikiwa nimelelewa na Mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za wananchi walio pembezoni, sina namna kutoa heshima yangu zaidi ya kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke. Msitarajie watu wengine kuwapigania mnapaswa kuchukua hatua kupitia jukwaa hili la ACT Wazalendo.
Kwa wafanyabishara, ninyi ndio mnachochea shughuli za Uchumi na kuzalisha ajira. Kuanzia kwa wamiliki wa maduka madogo mitaani mpaka kwa mameneja wa maduka makubwa; kutoka kwa wachuuzi na mama lishe mpaka kwa wamiliki wa viwanda na biashara; mnaamka kila siku asubuhi kujenga Taifa hili kwa kuzalisha mali na huduma. Baadhi yenu ambao mnamiliki viwanda, mashirika makubwa na kutoa ajira kwa maelfu ya wananchi, mmeanza mkiwa mnashona viatu na sare za shule, au mkitengeneza na kuuza mkate. Mmepata utajiri wenu na mali zenu kwa juhudi na jasho lenu na kutokana na fursa za kiuchumi zilizokuwepo kipindi hicho ambacho hakikuangalia dini, kabila, uwezo wa kifedha au rangi ya ngozi. ACT Wazalendo inataka kuwawekea mazingira bora ya biashara halali lakini pia kuhakikisha mnalipa kodi zenu na kutonyonya wafanyakazi wenu. Tunataka kuwawekea mfumo rahisi wa kodi, wenye kueleweka na unaowapa motisha kuzalisha zaidi ili kuongeza ajira zaidi na kupanua Pato la Taifa. Msipotimiza wajibu wenu biashara zenu hazitashamiri. Kurudi kwenye misingi ya Taifa hili ni kurejesha maadili katika biashara zenu.
Kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, ninyi ndio mnaolilisha Taifa letu na kuleta fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo nje. Kwa miongo mitatu sera za nchi zimewaweka pembeni na hivyo uchumi wenu kusinyaa. Viwanda vyote vya kusindika mazao yenu vimeuzwa kwa bei ya kutupwa licha ya kwamba jasho lenu ndio lilitumika kuvijenga. Miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano haiwafikii ili muweze kupata masoko. Hamna hifadhi ya jamii wala bima ya mazao yenu. Ardhi yenu wamepewa wawekezaji na mnakodishiwa, mnapanga kwenye ardhi yenu wenyewe. Mmeachwa mkijihangaikia. Kurejesha nchi kwenye misingi kutawarudishia heshima yenu katika nchi yetu. ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi kwenu kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi shirikishi ambao mtafaidika na jasho lenu. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya kinyonyaji.
Kwa Watanzania wote mnaonisikiliza leo, katika ukumbi huu na popote mlipo kupitia vyombo vya habari, mnamo mwaka 1978 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya nduli Idi Amini na kusema;
“Tutampiga. Sababu za kumpiga tunazo, nia tunayo, uwezo wa kumpiga tunao”.
Tanzania ipo katika vita hivi sasa.
Vita dhidi ya Ufisadi,
vita dhidi ya uporaji wa rasilimali zetu,
vita dhidi ya Siasa chafu.
Vita dhidi ya Uchumi wa kinyonyaji.
Vita dhidi ya kuporomoka kwa Utaifa wetu.
Tunapaswa kufanya jambo moja tu, nalo ni kupigana vita hizi. Ni vita kwa ajili ya kurejesha ndoto tuliyoota miaka 54 iliyopita na Muasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere. Tunataka kurejesha nchi kwa wananchi, tunataka kujimilikisha nchi yetu. Wananchi wawe WENYE nchi! Tutimize ndoto yetu ya kuona;
Tanzania yenye Dola madhubuti,
Tanzania yenye Wananchi wenye mwamko,
Tanzania yenye sekta binafsi iliyochangamka,
Tanzania yenye uchumi unaonufaisha watu wote.
Sababu tunazo, nia tunayo na uwezo tunao. Twendeni tukajenge Chama kitakachorejesha misingi ya Taifa letu.
Asanteni sana
Mzalendo Zitto Kabwe
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment