HOTUBA YA MH ZITTO KABWE (MBUNGE KIGOMA KASKAZINI) ILIYOTOLEWA TAREHE 15 MACHI 2015
Asanteni sana Kigoma Kaskazini
Mwanamapinduzi na Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara alisema kuwa ili kuleta mabadiliko ya kimapinduzi ni lazima kuwa na hali fulani ya uendawazimu. Ila tusiufikirie uendawazimu huu wa kuokota makopo bali ule ukichaa mzuri wa kuamini katika mambo au misingi fulani na kuisimamia kwa dhati pamoja na changamoto nyingi.
Kwa kuamini kwa dhati katika mabadiliko haya na kutaka kuboresha maisha ya wanakigoma, mwaka 2005 nilikuja kwenu kuwaomba ridhaa ya kuwatumikia kama mwakilishi wenu Dodoma. Nikiwa na umri wa miaka 29 tu. Labda ulikuwa ni msukumo wa matumaini yangu makubwa yanayoambatana na ujana yaliyowashawishi, kwani mliniamini na kunipa kazi hiyo ya heshima kubwa ya kuwawakilisha.
Mwaka 2010 mliniamini tena, naamini kutokana na utekelezaji wangu mzuri wa kazi na mafanikio tuliyoyaweza kuyapata katika jimbo letu. Hivyo kwa miaka kumi tumekuwa bega kwa bega katika safari hii ya pamoja ya kujenga na kuiendeleza jimbo letu, na leo nimekuja kuwashukuru kwa fursa mliyonipa kwani safari yetu inafikia mwisho. Fursa mliyonipa ni ya kipekee kwani ilikuwa fursa si tu ya kuwatumikia ninyi bali kulitumikia Taifa langu.
Katika miaka kumi hii kuna mambo makubwa tumeyafanya pamoja na kufanikiwa; na kuna mambo ambayo hatukuweza kuyafanya. Kwa yale ambayo hatukuweza kuyafanya naomba radhi. Kwa yale ambayo tumeweza kuyafanya naomba kuwapongeza sana kwa kufanikisha. Kwani kama Mwalimu Nyerere alivyotuambia kuhusu Uhuru na Maendeleo: “Uongozi ni kuongea na kujadili na wananchi, kuwaelewesha na kuwashawishi. Uongozi ni kufanya kazi pamoja na wananchi na kuonyesha kwa vitendo mnachotaka kufikia. Uongozi ni kuwa mmoja wa wananchi na kutambua kuwa mko sawa…. Wananchi hawawezi kuendelezwa bali wanajiendeleza.” Na ndivyo tulivyofanya kwa miaka kumi, na kwa ushirikiano wenu tumeweza kufanikisha miradi mikubwa katika Jimbo letu.
Mwaka 2005 tulikuwa hatuna barabara ya lami hata moja. Leo hii, ninapoongea nanyi tuna barabara za lami zenye zaidi ya kilomita 100 kuunganisha Jimbo letu na majimbo mengine kwa pande zote za nchi kavu. Vilevile tuna mradi mkubwa wa kuunganisha vijiji vya ufukweni mwa Ziwa Tanganyika kwa barabara. Kiujumla kwa mkoa wa Kigoma tumefanikiwa kumaliza daraja la Malagarasi na hivyo kuunganisha mkoa wetu na mkoa wa Tabora kwa lami jambo ambalo lilikuwa kilio chetu cha muda mrefu sana tokea enzi na enzi. Muhimu zaidi ni kuwa barabara hizi zinatumika na wananchi, wafanyabiashara na wakulima ili kuwasiliana, kufanya biashara na kupanua masoko.
Tumefanikiwa kuongeza huduma ya Nishati ya Umeme kwa kuunganisha vijiji zaidi ya 16 hivi sasa.
Changamoto kubwa iliyobakia mkoani kwetu ni uzalishaji mdogo wa umeme na wenye gharama kubwa sana. Suluhisho la kudumu ni kufanikisha mradi wa Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha 44MW ambao utakuwa nafuu na kuwezesha pia kusambaza umeme mikoa jirani ya Katavi na Tabora, na hata kuuza nchi jirani ya Burundi. Viongozi wa kisiasa wa mkoa wa Kigoma watakaoingia kwenye uongozi baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015 hawana budi kuweka kipaumbele kikubwa kwa mradi huu. Bila ya umeme wa uhakika na nafuu hatuwezi kupiga hatua ya kuongeza thamani ya mazao yetu kwa kujenga viwanda vya usindikaji na kuongeza ajira ya vijana wetu.
Tumefanikiwa kuanza miradi ya Bandari na Soko kubwa kijiji cha Kagunga. Lengo likiwa ni kukuza biashara ya bidhaa kati yetu na nchi ya Burundi. Kigoma ni mji wa biashara kiasili na biashara ilichukua nafasi kubwa ya uchumi wa mkoa huu kwa miaka mingi sana. Kuimarishwa kwa miundombinu ya Biashara ni sehemu ya miradi ya kimkakati katika kuuweka mkoa kuchukua nafasi yake ya kiuchumi katika nchi yetu. Katika muktadha huo ndio maana tunaendelea na miradi ya Bandari Kibirizi na Bandari ya Nchi Kavu Katosho. Ndio maana tunaendelea na mradi wa Kituo cha Usafirishaji Mwandiga ( Mwandiga International Transportation Terminal ) na eneo maalumu la kiuchumi Ujiji. Haya yote tuliyaanzisha kwa pamoja nanyi ili kuhakikisha kuwa uchumi wetu unazalisha ajira kwa watu.
Tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekondari kwa kuwa na shule katika kata na baadhi ya kata tumejenga shule kila kijiji. Hata hivyo, tuna changamoto kubwa sana ya ubora wa elimu katika mkoa wetu. Katika jimbo la Kigoma Kaskazini zaidi ya 90% ya watahiniwa wa Kidato cha Nne wanapata madaraja ya mawili ya chini, wakati ule daraja la nne na daraja la sifuri. Tumeanzisha mradi wa majaribio ya kutoa motisha kwa Walimu ili kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha elimu inaboreshwa. Shirika la Twaweza linaendesha mradi mkubwa wa motisha kwa walimu na baada ya mwaka huu tutakuwa tumejifunza njia bora za kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wetu. Bila Elimu bora miradi yote niliyoeleza hapo awali haina maana yeyote. Serikali imetoa Sera mpya ya Elimu, ni wajibu wetu kuona namna ya kuitekeleza katika ngazi yetu ili kupata mafanikio. Hata hivyo, uongozi wa kisiasa utakaoingia baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu hauna budi kujielekeza vya kutosha katika elimu ya ufundi ili kujenga stadi za kazi kwa vijana waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Tumefanikiwa kupanua huduma ya Afya kwa kuboresha Zahanati zetu chache zilizokuwepo na kujenga zahanati kadhaa mpya na miradi ya vituo vya afya vya Mahembe na Nyarubanda. Hata hivyo nasisitiza sana umuhimu wa kinga kuliko tiba kwani gharama za afya zimekuwa kubwa sana. Ndiyo maana tulipojadili hili suala, ilionekana kuwa suluhisho linatakiwa lipatikane kwa kufanya kile ambacho hatujawahi kufanya ili kuleta maendeleo ya kweli. Na mniruhusu hapa kunukuu wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipotuasi kuwa “Maendeleo ni maendeleo ya watu. Barabara, Majengo, kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na masuala mengi kama haya si maendeleo, bali ni vitendea kazi tu vya maendeleo” Ndiyo maana kulikuwa na umuhimu wa kutafuta njia mpya na mbadala kuboresha maisha ya mwananchi, hususan kwa upande wa afya. Uthibitisho wa ubunifu wetu ni kuwa katika kipindi hiki cha miaka 10 tumefanikiwa kuanzisha hifadhi ya jamii kwa wakulima. Tulianza na Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wa RUMAKU ambapo wananchi walijiunga na NSSF na hivyo kupata mikopo ya muda mfupi, huduma za afya bure na kujiwekea akiba kwa ajili ya mafao ya muda mrefu. Mafanikio makubwa yaliyopatikana yamewezesha wazo hili kusambaa nchi nzima na hivi sasa wakulima wa Korosho, Chai, Pamba, Tumbaku wanafuata nyayo za Wakulima wa Ushirika wa RUMAKU. Hapa Kigoma wazo hili sasa linatekelezwa kwa wavuvi wa mwambao mwa Ziwa Tanganyika. Ndoto yetu ni wananchi zaidi ya theluthi moja kwenye nguvu kazi wawe na Hifadhi ya Jamii. Natoa wito kwa wananchi wengine wenye uwezo wa kuchangia hifadhi ya jamii wajiunge na vikundi vya ushirika na kuchangia ili kufaidika na mafao ya muda mrefu kama pensheni lakini pia yale ya muda mfupi kama bima ya afya, mikopo kupitia SACCOS na mengine yatakayoanzishwa kama bima ya mazao.
Tumefanikiwa kujenga heshima ya watu wa Kigoma hapa nchini. Hivi sasa watu wa Kigoma tunatembea kifua mbele bila woga kuliko hapo awali. Kujiamini na kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano ni wajibu wetu kama raia. Changamoto za kujiona raia wa daraja la pili zimeondoka na zinaendelea kutokomezwa. Juhudi zetu ni silaha kubwa katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya Jamhuri yetu katika kila Nyanja za maisha yetu. Nafurahi kupata fursa ya kushiriki nanyi katika kujenga heshima hiyo ya Mkoa wetu. Nitaendelea kushiriki katika kudumisha heshima hiyo.
Nimejifunza mengi sana katika safari hii ya utumishi kwenu. Kama nilivyosema hapo awali, mliamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa ya nchi yetu kwa kunipa jukumu hili nikiwa kijana mdogo. Naamini kuwa ule ukichaa wangu mzuri wa kusimamia misingi ya kuleta maendeleo kwa wananchi wangu na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia nimezipigania. Na katika safari hii nimejenga marafiki wengi sana na pengine hata maadui ingawa hao ni wachache. Lakini haijalishi kwani mi binafsi sina uhasama na binadamu mwenzangu.
Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inaendeshwa. Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na mengine ni makosa. Mliniruhusu kufanya mak osa na kuyarekebisha makosa hayo kwa hiyo kukomaa zaidi. Shukrani za dhati ziwaendee wazee wangu ambao mliniongoza mpaka hapa tulipofika na kunishauri hata kunionya pale palipohitajika. Kwa ujumla nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndio maana hamkunisikia tu kutetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii kama Wakulima, Wafanyakazi, Wasanii, Wavuvi, Wana michezo na wana habari.
Katika safari hii ya miaka 10 kuna watu nimewafurahisha na kuna watu nimewaudhi. Kwa wale niliowaudhi ninaomba radhi. Kwa wale niliowafurahisha ninaomba wasiache kuniongoza na kunishauri kila wakati. Haikuwa safari rahisi na sikutegemea iwe rahisi. Kiuhalisia ilikuwa safari ngumu yenye mafunzo makubwa kwangu. Ilikuwa ni safari yangu kama kiongozi na pia safari yangu binafsi ya kupevuka kifikra na kupata mafunzo kuhusu maisha. Ukifika ulikokuwa unakwenda katika safari, unaweza kutathmini mengi kuhusu safari hiyo, lakini mwisho wa siku unatakiwa ujue kama safari hii ilikuwa njema ama la. Ninajivunia safari hii na ninasema kwa dhati kabisa ilikuwa ni safari njema.
Ni wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza Jimbo letu. Kushika kijiti pale ninapoishia. Kurekebisha pale nilipokosea. Kuimarisha pale nilipofikia.
Sitakuwa mbunge wenu baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba lakini nitaendelea kutetea maslahi ya Mkoa wa Kigoma na Taifa letu kwa njia nyingine.
Sitaacha ule uendawazimu mzuri aliyoizungumzia Thomas Sankara unaoleta maendeleo ya kimapinduzi. Na misingi ni ileile na maadui ni walewale ambao mwasisi wetu Mwalimu Nyerere aliyokuwa anasema tupambane nao, yaani umaskini, ujinga, maradhi na sasa tumeongeza ufisadi. Kizazi chetu kina jukumu la kipekee kuendeleza mapambano haya na nitaendelea kuhakikisha tunafanya mapinduzi na kuwa na Taifa lenye misingi madhubuti ya uwajibikaji ili kuondoa kila aina ya ufisadi na kutumia rasilimali za nchi kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.
Asanteni sana Kigoma Kaskazini!
0 comments :
Post a Comment