-->

VIJANA WA KIZANZIBAR WASIFIWA KWA KUCHELEWA KUJIHUSHA NA MAHUSIANO YA KIMAPENZI

VIJANA waishio visiwani Zanzibar huchelewa kujihusisha na vitendo vya ngono ikilinganishwa na Bara.

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) nchini, Mariam Khan, katika uzinduzi wa ripoti ya hali ya idadi ya watu duniani ya mwaka 2012.

Alisema utafiti huo unaonyesha asilimia 17 ya wasichana na asilimia 10 ya wanaume wa kati ya miaka 18 hadi 24 walijamiiana kabla ya kufikisha miaka 18.

Takwimu hizo zinaonyesha asilimia 57 ya wasichana na asilimia 37 ya wavulana visiwani humo wenye miaka kati ya 15 hadi 24 hawana uelewa na mahali inapouzwa mipira (kondomu) ya kike au ya kiume.

“Utafiti wa viashiria vya VVU na malaria nchini (THMIS), uliofanyika hivi karibuni, unaonyesha mwaka jana asilimia 6 ya wasichana ambao hawajaolewa na asilimia 15 ya wavulana wasiooa wenye miaka kati ya 15 hadi 24 waliwahi kujamiiana kabla ya ndoa na bila kutumia kinga,” alisema.

Katika masuala ya uzazi, alisema utafiti huo unaonyesha wasichana waishio Zanzibar hawatumii njia za kisasa za uzazi wa mpango ikilinganisha na Bara ambako matumizi yake ni asilimia 17.

Alisema wasichana wengi nchini wanapata ujauzito kutokana na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi, wazazi kutengana au kukata tamaa.

Khan alisema ripoti hiyo imeonyesha msichana mmoja kati ya wanne, anajifungua akiwa na umri wa miaka 19.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Edward Mbanga, alisema jamii inapaswa kuwalinda watoto wa kike hasa walio na umri mdogo, ili kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuwasababishia wapate ujauzito.

“Tatizo la wasichana kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo sio tatizo la nchi hii pekee, bali lipo hata maeneo mengine,” alisema.

CHANZO:MUNIRA MADRASA
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment