-->

HII NDIO SABABU YA BUNGE JANA KUVUNJIKA MNAMO SAA TANO USIKU

Dar/Dodoma. Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana usiku kilivunjika baada ya vurugu kutawala ukumbini humo.
Vurugu hizo zilianza saa 04:42 usiku hadi saa 04:49 usiku wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha Bunge hadi leo saa tatu asubuhi.
Chanzo cha vurugu ni kutokana na ugumu wa kutokukubaliana na azimio la tisa, lililolenga kumwajibisha moja kwa moja Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Azimio la PAC lilitaka Waziri Muhongo aadhibiwe kwa kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma zilizokuwa zinazomkabili ikiwamo kulidanganya Bunge.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wengi wakiwa wa CCM walitaka waziri huyo asiadhibiwe na Bunge bali achukuliwe hatua na mamlaka iliyomteua.
Wakati ubishani huo ukiendelea, ikiwa imefika saa 4.42 usiku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisimama na Spika Makinda alimruhusu kuzungumza.
“Bunge kufikisha saa tano kasoro ni historia, lakini leo (jana) kuna uzito wa kiti na uzito wa wabunge kwa mamlaka ambayo yako ndani yao. Panaonekana kuna maamuzi mengine ya kulinda watu. Kwa nini leo tuna kigugumizi. Tunapata wakati mgumu kuendelea kushiriki kikao cha kulindana. Kwanini mnalinda wezi,” ilikuwa ni kauli ya Mbowe.
Mara baada ya kutoa kauli hiyo, wabunge wote wa upinzani walisimama na kuanza kupiga kelele kwamba wezi waondoke…tunataka fedha zirudi…tunataka fedha zirudi…vijana msilale…vijana msilale.
Wakati wabunge hao wakiendelea kuimba, wabunge wa CCM wao walikuwa wakizunguka zunguka huku wengine wakitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Hata hivyo, wabunge wa upinzani waliendelea kusimama, kuimba na kupiga makofi, huku wabunge wa CCM wakimpongeza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kwa kuruka kihunzi alichokuwa amewekewa na kamati ya PAC.
Kutokana na hali hiyo wabunge wengine walisimama vikundi vikundi, huku Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, na Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka walikuwa wakiwasihi wabunge wa upinzani wasiondoke bungeni.
Spika Makinda alisimama na kusema, “Mheshimiwa Mbowe kuondoka mapema ni mambo ya kitoto, semeni mnataka Bunge lifanye nini.”

Hata hivyo, kauli hiyo ya Makinda haikuwafanya wabunge hao kuacha walichokuwa wakikifanya, bali walibaki ndani ya ukumbi wakiwa wamesimama hadi ilipofika Saa 04:49 usiku wakati Spika Makinda aliposimama na kusema, “Waheshimiwa wabunge naahirisha kikao cha bunge hadi pale tutakaposhauriana.”
Kuvunjika kwa kikao hicho kinaweka njia panda hatima ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema ambao Bunge lilikuwa halijafikia kufanya maazimio ya hatima yao.
Hoja ya baadhi ya wabunge wa CCM walikuwa wakitaka mapendekezo yaliyotolewa na Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge kuhusu hatima ya Pinda na Werema yapite.
Chenge alipendekeza kuwa, “Kuhusu suala la Waziri wa Nishati na Madini lifikishwe kwa mamlaka ya uteuzi kwa hatua zaidi (wakimaanisha Rais).”
Pendekezo ambalo lilipingwa na upinzani kwa kile walichoeleza kuwa Bunge linaweza kuwawajibisha kama ambavyo limewahi fanya hivyo. Spika Makinda akijibu hoja ya Bunge kuwawajibisha alisema; “Mnajua waheshimiwa wabunge huko nyuma mawaziri walikubali wenyewe, lakini hawa wamekataa ndiyo maana tunaona haya yanatokea.”
Awali, Bunge hilo limemwachia Rais Jakaya Kikwete kufanya uamuzi wa kuwawajibisha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi baada ya kuadhimia kuwa suala lake lifikishwe kwa Rais kwa hatua zaidi.
Mjadala wa kuchukuliwa hatua kwa Maswi uliwagawa wabunge na kuwafanya kujadili kwa zaidi ya dakika 30, kufikia uamuzi huo ambao hata hivyo ulipingwa na baadhi ya wabunge.
Hata hivyo, Bunge limemwokoa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kwa kuona kuwa kauli yake aliyoitoa haikuwa na madhara yoyote hivyo hahusiki kwa vyovyote vile kwenye sakata hilo.
Hatua ya kuwashughulikia viongozi hao na wengine kuokolewa ilifikiwa baada ya mvutano mkali wa pande mbili ndani ya Bunge katika kukubaliana na mapendekezo ya kamati ya PAC.
Baada ya muda wabunge na mawaziri walioanza kuingia kwenye magari yao na kuondoka bila kujua nini kitaendelea leo.
Hata hivyo, Spika Makinda ambaye alikuwa amezungukwa na askari wa usalama akisindikizwa ofisini kwake alisikika akiwaambia baadhi ya wabunge kuwa kikao kitaendelea leo saa tatu.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Bunge zimeeleza kuwa kikao cha Bunge kitaendelea leo.
Awali, Bunge lilikubali mapendekezo ya PAC kwamba viongozi wa umma waliofaidika na fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wachukuliwe hatua za kinidhamu ya kuvuliwa nyadhifa zao.
Wengine ni Naibu wake Stephen Masele na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakimu Maswi nao wawajibishwe.
PAC ilieleza kuwa wakati Jaji Werema ameonekana kutoishauri vizuri Serikali na pia kuagiza fedha hizo zitolewe kwenye akaunti hiyo, mwenzake Profesa Muhongo hakuchukua hatua wakati akijua kuwapo kwa sakata hilo, huku Naibu wake, Stephen Masele akitiwa hatiani kwa kulidanganya Bunge.
Vilevile, Bunge limependekeza kuwa viongozi wa umma waliopewa fedha zitokanazo na Akaunti ya Tegeta Escrow na hawakutangaza kupokea zawadi kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma nao wachukuliwe hatua akiwamo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Viongozi wengine wanaotajwa kupewa fedha hizo ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na baadhi ya majaji na watumishi wa Serikali.
BOFYA HAPA KUSOMA HABARI NYINGINE ZA SIASA
                            UWANJA WA SIASA
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment