aadhi
ya wamiliki wa blogu nchini Tanzania wameonyesha wasiwasi baada ya wito
kutolewa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo wa kuwataka wafanye kazi
chini ya jumuia inayotambulika.
Wito
huo umetolewa katika warsha maalumu iliyoandaliwa na taasisi hiyo
ambayo ilikuwa na lengo la kuwafunda wamiliki wa blogu nchini humo ikiwa
ni sehemu moja wapo ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao. Baadhi wanahisi kwamba utaratibu huo huenda ukawathibiti katika kupata mapato hayo.
Warsha
hii imejumuisha zaidi ya mabloga mia mbili kutoka sehemu mbalimbali
nchini Tanzania. Licha ya kukuwa kwa kasi kwa tasnia hii na kuwa sehemu
muhimu ya kupasha habari jamii, imefahamika kwamba, baadhi ya wamiliki
wa blogu hawana utaalamu wa uandishi.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo ambayo imeonekana kuwa ndio chanzo
cha ukiukaji wa maadili ya uandishi, Mamlaka ya Mawasiliano nchini
Tanzania TCRA imetoa fursa kwa wamiliki hao kuanzisha jumuia itakayotoa
muongozo.
"TCRA tunashughulika na mawasiliano kwa ujumla wake, lakini mtandao ni
muhimu sana. Kwa hiyo katika Intanet tumeona kwamba hawa bloggers ni
wadau muhimu sana lakini hamna mtu ambae amewaunganisha, kwa hiyo sisi
tumefanya kikao ili bloggers wakutane ili tuwape taarifa ambazo
zinasaidia katika utaalamu wao. Kimoja ambacho kimekubaliwa ni kwamba
waanzishe jumuia yao, sisi hatutakwepo kwenye uongozi wao bali tunataka
tuwe chachu," amefafanua Profesa John Nkoma ambae ni mkurugenzi mkuu wa
TCRA.
Blogs nyingi nchini Tanzania zinamilikiwa na vijana ambao kutokana na
matatizo ya ajira, wameona hii ni fursa pekee ya kujipatia ajira na
kujiongezea kipato. Hata hivyo, hofu tayari imeanza kutawala miongoni
mwao kwamba mabadiliko yatakayofanyika yanaweza kuathiri kipato chao.
Habiba Chagamba ambae ni mmiliki wa blogu ya Tayojo amemwambia mwandishi
wa BBC Aboubakar Famau kwamba wanahofia mabadiliko yoyote
yatakayofanyika yanaweza kuathiri kipato chao.
"Vijana wengi wameona soko la ajira ni la taabu, hivyo wameona hii ndio
njia ya kujikwamua kiuchumi. Kwa mfano mimi blogu yangu inaniingizia
dola za kimarekani kuanzia 300 hadi 400 kwa mwezi, hii si haba kwa
mtanzania.
Lakini iwapo serikali itataka kukata kodi katika hayo mapato, basi hapo
ndio kutakuwa na utata, kwa sababu hatujui tutakula wapi. Ndio maana
tunasema jamani fanyeni mnavyofanya lakini tuangalie na sisi tunakula
wapi, lakini katika suala la kodi, kila mtu lazima alipe kodi," amesema
Habiba.
Kikubwa pia kilichotawala katika warsha hiyo lilikuwa ni suala zima la
maadili ya uandishi hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea
kwenye kura ya maoni ya katiba iliyopendekezwa na uchaguzi mkuu ambavyo
vyote vinatarajiwa kufanyika mwakani katika vipindi tofauti.
Assah Mwambene ni msemaji wa serikali ya Tanzania.
"Kiutaratibu sisi kama serikali hatudhibiti mitandao ya kijamii.
Tunachotaka sisi ni kuwatambua, tuwajue wako wapi, wanafanya nini,
lakini la pili walau tunaweza kuwaambia, jamani hapa tunaona mmekwenda
vibaya au vizuri sana," amesema Assah Mwambene ambaye ni msemaji wa
serikali ya Tanzania na kuongeza, "hatuwezi kukataa kwamba vyombo hivi
ni muhimu na ni mchakato muhimu wao kushiriki lakini wakiwa na uelewa
mpana wao wenyewe kwa sababu wana wajibu mkubwa katika jamii
wanayoifanyia kazi."
Tanzania ina blogu zaidi ya elfu mbili lakini ni wachache ambao wameweza
kujinyakulia umaarufu wa ndani ya nchi na nje kupitia kazi zao za blogu
kama vile Issa Muhiddin Michuzi na Father Kidevu.
0 comments :
Post a Comment