-->

DONDOO ZA AFYA:ZIFAHAMU TIBA YA SARATANI YA TEZI DUME

TIBA YA SARATANI YA TEZI DUME
Je Saratani ya tezi dume inatibika?
Ndiyo! Kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika.
Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi, wakati kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri kumfuatilia mgonjwa kwa ukaribu bila kumfanyia upasuaji au bila kumpatia tiba ya mionzi.
Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu (hormonal therapy), au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).
1.Upasuaji
Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa walio katika hatua za awali za ugonjwa (stage I na stage II) ingawa pia hufanywa kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu yaani stage III na stage IV. Upasuaji unaofanywa ni ule wa kuondoa tezi dume pamoja na baadhi ya tishu zinazozunguka tezi hiyo.
2.Tiba ya Mionzi
Hii ni aina ya tiba inayotumia mionzi kuua seli zenye saratani. Tiba ya mionzi hutumika kutibu saratani ya tezi dume ambayo haijasambaa kwenye sehemu nyingine za mwili. Aidha inaweza pia kutumika kuua masalia ya tishu zenye saratani mara baada ya kufanyika kwa upasuaji.
Kwa wagonjwa walio katika hatua ya mwisho ya saratani yaani wale ambao saratani tayari imeshasambaa mwilini, mionzi hutumika kupunguza maumivu makali ya mifupa.
Madhara anayoweza kupata mgonjwa kutokana na aina hii ya tiba ni pamoja na kushindwa kusimamisha uume au uhanithi, kukosa hamu ya kula, uchovu, ngozi kubabuka, kuharisha na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.
3.Tiba ya Homoni
Hii ni aina ya tiba inayotumia dawa zinazopunguza kiwango au ufanyakazi wa homoni ya testosterone mwilini. Testosterone ni homoni ya kiume inayochochea ukuaji wa tezi dume, hivyo basi matumizi ya dawa hizi husaidia kupunguza ukuaji huu na kusambaa kwa seli za saratani
SOURCE:MZIZIMA24
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment