Hii ni njia ambayo mwanamke anaweza kutumia kupanga uzazi bila kutumia dawa au kitu cha aina yoyote. Njia hii inategemea kuchagua kwa makini siku za kufanya tendo la ndoa kutegemeana na ufahamu wa kipindi chote cha hedhi cha mwanamke. Njia hii ina faida yake, lakini yeyote anayeitumia lazima awe makini sana, kwa sababu lazima ajue lini anategemea kupata damu ya hedhi tena. Ni rahisi sana kufanya makosa kwa kutumia njia hii.
Nani anaweza kutumia njia ya kalenda Wanawake walioko tayari kuchukua miezi 3 hadi 6 kupima vipindi vyao vya hedhi kabla ya kutumia njia hiyo. Wanawake walio na mzunguko wa hedhi ambayo urefu wake haubadiliki. Wanawake wanaojua hisabati vizuri sana.
Kwa hiyo, kabla ya kutumia njia hiyo, ni vyema kwa mwanamke kuandaa kalenda inayoonesha siku yake ya kwanza kutoa damu ya hedhi kila mwezi kwa kipindi cha miezi 3 hadi 6. Hii itamsaidia kujua lini mayai yake yalipevuka.
Njia hii inamsaidia zaidi mwanamke aliye na mzunguko wa hedhi wa siku 28, na hutegemea kufahamu kuwa yai la mwanamke hupevuka siku 14 kabla hajaingina kwenye hedhi.
Kwa mfano; 1) Kama unaanza kuingia katika hedhi tarehe 1 Juni (na una mzunguko wa hedhi wa siku 28), basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya cha hedhi tarehe 29 Juni. Kwa hiyo yai lako litapevuka siku 14 kabla kwenye tarehe 15 Juni. Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe kupata mimba kama unafanya mapenzi karibu na tarehe hii, kuanzia tarehe 14 Juni hadi 16 Juni. Kwa hiyo kuepukana na kupata mimba, usifanye mapenzi kati ya tarehe hizo. Lakini lazima ukumbuke kuwa mbegu za kiume zinaweza kuishi ndani ya mwili wa mwanamke kwa siku 7, kwa hiyo ili kuwa na uhakika zaidiya kuepukana na kupata mimba, unatakiwa kutokufanya mapenzi kuanzia tarehe 8 hadi 16 Juni.
2) Katika mfano mwingine, kama unaanza kuingia katika hedhi tarehe 13 Juni (na una mzunguko wa hedhi wa siku 28), basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya cha hedhi tarehe 11 Julai. Kwa hiyo yai lako litapevuka siku 14 kabla kwenye tarehe 28 Juni. Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe kupata mimba kama unafanya mapenzi kati ya tarehe 27 Juni na 29 Juni. Ili kuepukana na kupata mimba, usifanye mapenzi kati ya tarehe hizo. Kwa usalama zaidi, usifanye mapenzi kuanzia 21 hadi 29 Juni.
3) Katika mfano mwingine, kama baada ya kuandaa kalenda kuonesha mzunguko wako wa hedhi wa miezi 3 hadi 6 iliyopita, unagundua kuwa mzunguko wako ni wa siku 33 badala ya siku 28, basi kifuatacho ni kweli: kama unaanza kuingia katika hedhi tarehe 1 Juni basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya cha hedhi tarehe 4 Julai. Kwa hiyo yai lako litapevuka kwenye tarehe 20 Juni (Siku 14 kabla ya tarehe 4 Julai). Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe kupata mimba kama unafanya mapenzi kati ya tarehe 19 na 21 Juni. Ili kuepukana na kupata mimba, usifanye mapenzi kati ya tarehe hizo. Kwa usalama zaidi, usifanye mapenzi kuanzia 13 hadi 21 Juni.
4) Katika mfano mwingine, kama baada ya kuandaa kalenda kuonesha mzunguko wako wa hedhi wa miezi 3 hadi 6 iliyopita, unagundua kuwa mzunguko wako ni wa siku 26 badala ya siku 28, basi kifuatacho ni kweli: kama unaanza kuingia katika hedhi tarehe 1 Juni basi kuna uwezekano mkubwa utaingia kwenye kipindi kipya cha hedhi tarehe 27 Juni. Kwa hiyo yai lako kitapevuka kwenye tarehe 13 Juni (Siku 14 kabla ya tarehe 27 Juni). Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kwako wewe kupata mimba kama unafanya mapenzi kati ya tarehe 12 na 14 Juni. Ili kuepukana na kupata mimba, usifanye mapenzi kati ya tarehe hizo. Kwa usalama zaidi, usifanye mapenzi kuanzia 6 hadi 14 Juni.
Faida ya kutumia njia hiyo •Haina madhara yeyote ya kimwili.
Matatizo yanayoweza kujitokeza •Njia ya kalenda si kinga dhidi ya virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.
•Njia hii ni ngumu na inahitaji wanawake kuwa wastadi katika hisabati, na kuwa waangalifu sana kuandika au kukumbuka tarehe ya kuanza kipindi chao cha hedhi cha mwisho.
•Huchukua muda mrefu (miezi 3 hadi 6) kufahamu urefu wa mzunguko cha hedhi.
•Mzunguko wa hedhi huweza kubadilika wakati wowote kufuatana na mabadiliko katika mwili. Hii huweza kusababisha tarehe ya yai kupevuka kuwahi au kuchelewa, kwa hiyo mwanamke huweza kujiweka katika hatari ya kupata mimba bila kufahamu.
•Ili njia hii iwe na uhakika, mwanamke hawezi kufanya mapenzi katika siku zake 9 kila mwezi ambapo kuna uwezekano wa yeye kupata mimba. Kwa hiyo njia hii inahitaji uwezo mkubwa wa kujidhibiti na hufanya kazi vizuri iwapo mwanaume namwanamke wamekubaliana kufanya hivyo kwa pamoja, na mwanaume anamsaidia mwanamke kuhesabu au kuandika urefu wa mzunguko wake wa hedhi.
•Kwa sababu urefu wa mzunguko wa hedhi wa mwanamke huweza kubadilika ghafla bila kutegemea, hata kama inatumika inavyotakiwa, njia hii si nzuri kama njia nyingine zilizotajwa kuzuia mimba na kupanga uzazi.
0 comments :
Post a Comment