Wabunge
wawili nchini Libya walipigwa risasi na kuumizwa baada ya kundi la
waandamanaji kuwashambulia bungeni katika mji mkuu wa Tripoli.
Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa wawili hao walipigwa risasi walipojaribu kutoroka kutoka katika eneo hilo.
Waandamanaji
hao waliokuwa na ghadhabu walilishambulia bunge hilo, huku wakitaka
bunge lifungwe na tarehe mpya ya uchaguzi wa mapema itangazwe.
Kumekuwa
na wimbi la maandamano nchini humo kutokana na uamuzi wa bunge la nchi
hiyo kuahirisha tarehe ya uchaguzi hadi baadaye mwakani.
Waliolishambulia
bunge siku ya Jumapili walisema kuwa walighadhabishwa pia na “kutekwa
nyara” kwa waandamanaji waliokuwa na kikao nje ya bunge.
Walisema kuwa waliohusika na utekaji nyara huo walikuwa chini ya uongozi wa waasi wanaotumikia amri ya bunge.
Waandamanaji
hao ambao wengi wao ni vijana walijihami kwa visu na
vijiti,wakalishambulia bunge huku wakiwa na ujumbe kwa wabunge kwa
kuimba “jiuzulu,jiuzulu”, kwa mujibu wa taarifa ya ashirika la habari la
AFP.
Bunge la nchi ya Libya limeshambuliwa mara kadhaa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Nuri
Abu Sahmein ambaye ni spika wa bunge hilo aliambia kituo cha
televisheni cha Al-Nabaa kuwa maandamano yaliyokuwa ya amani,
yalivurugwa na watu waliojihami.
"Wabunge wawili walipigwa risasi pale walipojaribu kutoweka mahali hapo kwa kutumia magari yao,” alisema.
Haikuwezakana kubaini papo hapo idadi ya wabunge walioumia.
Picha
zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha waandamanaji
wakivuta kile kilichokusudiwa kuwa kiti cha Spika wa bunge hilo nje ya
bunge na kukichoma.
Mwandishi
wa BBC Rana Jawad ambaye yuko Tripoli anasema kuwa bunge la Libya
limeshambuliwa mara kadhaa na makundi tofauti, yakiwemo makundi ya waasi
katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Uchaguzi
uliokuwa wa amani ulifanywa na nchi ya Libya katika mwezi wa Julai
mwaka jana, ila bado nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ingali
inang’ang’ana kupata utulivu, miaka mitatu baadaye tangu kufurushwa
kutoka maamlakani kwa aliyekuwa rais, hayati Muammar Gaddafi.
-BBC

0 comments :
Post a Comment