-->

NDEGE WA AJABU WATOKEA BUKOBA,UWEPO WAO WALETA MAAFA MKOANI HAPO


Ndege wa ajabu wakiwa juu ya miti katika Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Ndege hao wamezua hofu kwa wakazi kutokana na kinyesii chao kudhuru mifugo na ndege. Picha na Mtandao wa Jamii Forums


BUKOBA.

NDEGE wa ajabu wanaosadikiwa kutoa kinyesi chenye sumu kali, wamevamia Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba na kusababisha vifo vya mifugo na ndege wafugwao, huku ukali wa sumu hiyo ukisababisha kutoboka mabati ya nyumba zilizopo kisiwani humo.
Ndege hao wanaoaminika kuvamia kisiwa hicho mwezi mmoja uliopita tayari wameshasababisha vifo vya kuku 516 na mbuzi 12 wanaodaiwa kugusa au kula kinyesi chao. Hata hivyo, bado haijafahamika ndege hao wanatokea nchi gani.


Akithibitisha habari hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Massawe alisema Serikali ilipata taarifa hizo kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na baadaye kuundwa timu ya kutafuta taarifa za awali za tatizo hilo.


Massawe alisema ndege hao, pamoja na kusababisha vifo vya mifugo na ndege wafugwao pia baadhi ya miti katika kisiwa hicho imekauka na mabati kutoboka inapotokea kinyesi chao kitaangukia kwenye paa za nyumba zao.


Pia Massawe alisema kuwa, taarifa ya kuwapo kwa ndege hao katika Kisiwa cha Musira, ilifikishwa kwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kebwe Stephene Kebwe aliyekuwa mkoani humo wiki iliyopita na kuwa suala la kuwapo kwa ndege hao siyo la ghafla kwa kuwa walikuwapo hapo awali.


Dk. Kebwe alisema wizara imetuma wataalamu kuchunguza tatizo hilo na kuwa wizara hiyo itaangalia ukubwa wa tatizo hilo linavyoweza kuwaathiri wananchi.


Hata hivyo, alisema suala hilo pia linahitaji ufuatiliaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Dk. Munda Elias alikwishawasili kwa ajili ya uchunguzi na kuthibitisha kuwa tayari kinyesi cha ndege hao kimepelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi na Mkoa unasubiri matokeo ya utafiti huo.


Naye Ofisa Tarafa wa Rwamishenye, Abdon Kahwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Ziporah Pangani alisema tayari Serikali imechukua hatua za kupiga marufuku kupeleka au kusafirisha mifugo kutoka kisiwani humo kwenda maeneo mengine kwa hofu ya kusambaa kwa sumu hiyo.


Pia alisema ndege hao wameleta hofu kwa wakazi wa kisiwa hicho, kwani kinyesi chao kinapodondoka kwenye bati hupata kutu na kutoboka, huku kukiwa na hofu nyingine kwamba huenda mifugo nayo imeathiriwa.MWANANCHI
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment