KONGAMANO LA KISWAHILI KANDA YA TANZANIA LAFANA 19/03/2014
Ø Pendekezo kuhusu Marehemu Shaaban
Robert kutunukiwa Shahada ya heshima ya Uzamivu laungwa mkono
Ø Kiswahili lugha ya pili Barani
Afrika kwa idadi ya Wazungumzaji
Kongamano la Sita la
Lugha ya Kiswahili kwa upande wa Kanda ya Tanzania, limemalizika mwanzoni mwa
Mwezi huu baada ya kufanyika kwa muda wa takribani Siku nne, toka pale tarehe,
26/02/ hadi 01/03/2014. Kongamano hilo lilifanyika Jijini Tanga katika Chuo
Kikuu cha Eckernford, ambapo Wadau Wanafunzi na Wahadhiri toka sehemu
mbalimbali nchini walihudhuria, Vyuo zaidi ya kumi (10) vilishiriki katika
Kongamano hilo. Lengo la Kongamano hilo lilikuwa ni kuwaleta karibu Wadau wa
Lugha hii adhimu ya Kiswahili sambamba na kujadili changamoto na matatizo
mbalimbali yanayoikabili lugha hii. Mada mbalimbali ziliwasilishwa, Mada hizo
ni pamoja na; Kiswahili ni bidhaa adhimu,
jadili, Shaaban Robert kama Baba wa Fasihi
je, mchango wake unatambuliwa? Uchangamani wa asili ya Kiswahili na Mswahili,
Mchango na changamoto za vyombo vya habari katika kukuza lugha ya Kiswahili.Michango
na maoni mbalimbali ya Wadau hao wa lugha yalitolewa mara baada ya kuwasilishwa
kwa Mada hizo.
Wadau mbalimbali wa Kiswahili wakifuatilia
kwa umakini mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa Kongamano hilo
Mgeni rasmi katika
Kongamano hilo alikuwa ni Profesa Mwansoko, huyu ni Mtaalamu wa uundaji wa
Istilahi na kauli mbiu mbalimbali katika nyanja zote, Kiuchumi, Kisiasa, Afya
na nyinginezo, baadhi ya Istilahi alizozitunga ni pamoja na;VVU-Virusi vya
UKIMWI”, na kauli mbiu isemayo, “MALARIA HAIKUBALIKI” , sambamba na hilo pia ndiye
Mkurugenzi wa BAKITA. Katika utoaji wa nasaa zake yeye (Prof. Mwansoko) alianza
kwa kueleza historia ya CHAWAKAMA sambamba na wazo la kuanzishwa kwake, kikao
kilichofanyika kule Mkoani Arusha Mwaka 2005, baada ya Watu (Wadau) takribani
Saba toka Nchi za Afrika Mashariki kukutana. Kwa upande mwingine Prof. Mwansoko
alijuza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo mbioni kuanzisha Kamisheni ya
Kiswahili, ambapo Makao yake Makuu yatakuwa Nchini Tanzania – Zanzibar, hivyo
basi Watanzania hawana budi kuchangamkia hilo. Prof. Mwansoko alikwenda mbali
zaidi na kusema kuwa, lugha ya Kiswahili hivi sasa ni lugha ya pili kwa idadi
ya Wazungumzaji Barani Afrika, na ni lugha inayokua kwa kasi katika Nchi za
Afrika ya Kusini, Gaboni, Zimbabwe, Namibia.
Kuhusu
Wenyeji na Hotuba ya Makamu Mkuu wa Chuo.
Kongamano
hilo lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Eckernford-Tanga, kilichopo chini ya
Prof. Kiango ambaye ndiye Makamu Mkuu wa Chuo, na Prof. Madumulla ambaye ni
Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, pamoja na Wanafunzi wasomao katika Chuo hicho.
Katika hotuba yake ya kufunga Kongamano
hilo, Prof. Kiango alizungumzia kwa upana,mfungamano na uwiano uliopo baina ya
lugha na maarifa husika, alisema, “Maarifa huingia kichwani mwa Mtu kupitia
lugha , hasa ile unayoifahamu” aliendelea kusema,” kupitia lugha ndipo
uchakataji wa taarifa hufanyika na hatimaye kupata lile (lengo)
lililokusudiwa”,mwishoni alitoa rai kwa Wadau na Wanafunzi kuipa nafasi lugha
ya Kiswahili ili kujenga msingi imara wa maendeleo ya taifa hili.
Kushoto
ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Eckernford Prof. Kiango (Mwenye suti) akichangia
wakati wa Kongamano hilo.
CHAWAKAMA-TANZANIA,
yabariki Marehemu Shaaban Robert kutunukiwa Shahada ya heshima ya Uzamivu (PhD)
Hilo lilikuwa ni moja
ya wazo muhimu sana alililotolewa wakati Kongamano hilo. Lilikuwa ni Pendekezo
lililowasilishwa na Bwana Athuman Ponera, Mhadhiri toka Chuo Kikuu cha Dodoma.
Katika uwasilishaji wake huo, Bwana Ponera alimtaja na kumuelezea kwa
upana sana marehemu Shaaban Robert na
kusema kuwa kutokana na kazi zake nyingi kuigusa jamii moja kwa moja katika
kila nyanja, kisiasa, kijamii na kiutamaduni lakini bado ameendelea kusahauliwa
na kutotambuliwa mchango wake kwa vitendo, hivyo basi fursa pekee ni hiyo ya
kumpa tunzo ya heshima ya Shahada ya Uzamivu. Kazi zake nyingi zilijikita
katika kupinga uonevu, na dhuluma lakini kikubwa zaidi, aliamini katika usawa
baina ya Watu wote.
Historia
fupi kuhusu Marehemu Shaaban Robert
Shabaan Robert
alizaliwa Mwaka 1909 kule Vibambani- Machuwi, Mkoani Tanga na kufariki Mwaka
1962 na kuzikwa huko huko Tanga. Elimu yake alipata katika Shule ya Msingi Kichelewe (Siku hizi Uhuru Mchanganyiko)
Dar es Salaam, kuanzia darasa la kwanza hadi la Sita pale Mwaka 1922-1926,
baadhi ya kazi zake ni pamoja na; Utu
bora Mkulima, Adili na nduguze, Maisha yangu na baada ya Miaka Hamsini,
Kusadikika,Wasifu wa Siti bint Saadi, Kufikirika, Siku ya Watenzi wote.
Chini ni Nyumba ambayo
Marehemu Shaaban Robert aliwahikuishi enzi za uhai wake, iliyopo Tanga mjini
Mjukuu
wa Shaaban Robert (mwenye kofia) akitoa maelezo kwa baadhi ya Wanachawakama huko
Vibambani Machuwi
Washiriki
walipata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za kihistoria
Pamoja na kuyatazama na kuyajadili kwa kina masuala
mbalimbali yahusuyo Kiswahili, lakini pia Washiriki hao walipata fursa ya
kwenda kutembelea sehemu za kihistoria kama vile; Mapango ya Amboni, na kule Machuwi
sehemu ambayo Marehemu Shaaban Robert alizaliwa, akalelewa na kuzikwa huko.
Imeandaliwa na, Adam Matimbwa
Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu-BAED,
maoni/ushauri-0654 051209
0 comments :
Post a Comment