-->

YANGA WAMSHUSHIA KIPIGO CHA BAO 3 KWA BILA RHINO MKOANI TABORA

Na Baraka 
LIGI kuu soka Tanzania bara imeendelea leo  kwa mitanange miwili ya vuta nikuvute iliyopigwa katika miji miwili tofauti hapa nchini.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Young African walialikwa na maafande wa JWTZ, Rhino Rangers kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mbeya City walikuwa wageni wa JKT Ruvu wanaonolewa na kocha Fredy Ferlix Minziro, katika uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, nje kidogo ya jiji la  Dar es salaam.
Yanga waliuanza mchezo wa leo kwa lengo moja la kuibuka na ushindi ili kuwasogelea Azam fc kileleni.
Haikuwa rahisi kwao kuwafunga Rhino kwa dakika 28 za kwanza, lakini dakika ya 29, mshambuliaji aliyekalia benchi kwa muda mrefu, Jeryson Tegete aliandika bao la kuongoza.
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Rhino ambapo mara kadhaa Tegete alijaribu kuzitafuta nyavu za wapinzani wao, lakini mabeki wa Rhino walikuwa makini.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Yanga walitoka kifua mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili  kilianza kwa Yanga kuendelea kulishambulia lango la Rhino.
Dakika ya 68, Yanga walipata bao la pili baada ya mlinzi wa Rhino kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa winga machachari, Saimon Msuva.
Dakika ya 75, kocha Pluijm alimtoa Tegete na kumuingiza mshambuliaji Hussein Javu.
Hakika nyota ya Yanga iliendelea kung`ara ambapo dakika ya 90, Hussein Javu aliandika bao la tatu kwa Yanga na kulizamisha zaidi jahazi la Rhino.
Dakika 90 za mchezo huo zimemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Safari ya Rhino Rangers kuelekea ligi daraja la kwanza imezidi 
kuiva kwasababu wamebakiwa na michezo minne tu.

Huko Azam complex, Chamazi, nje kidogo ya jijini la Dar es salaam, JKT Ruvu walikuwa wenyeji wa Mbeya City.

Mchezo huo umemalizika kwa wagonga nyundo wa Mbeya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mabao yoye mawili ya Mbeya City yamefungwa na Sady Kipanga.
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ameuambia mtandao huu kuwa mechi ilikuwa nzuri, na walijitahidi kutumia nafasi walizotengeneza.

“JKT Ruvu walicheza vizuri. Sisi tulikuwa wazuri zaidi. Tumepata nafasi na kutumia. Mashabiji wetu wazidi kutuamini kwani safari ya ubingwa bado ipo”. Alisema Maka.

Kwa matokeo hayo, Mbeya City wanafikisha pointi 42 katika nafasi ya tatu, pointi moja nyuma ya Yanga wenye pointi 43 baada ya kushinda leo mabao 3-0 mjini Tabora.

Utofauti wa pointi moja unaonesha jinsi ambavyo timu za ligi kuu hasa za juu zinaendelea kupambana kutafuta taji msimu huu.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi nne ambapo Simba itacheza na Coastal Union katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex. Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam Tv.

 Mechi nyingine za kesho Jumapili ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment