TAMKO LA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA WA KUNDI LA “TANZANIA KWANZA”
23 Machi 2014
Sisi
Wajumbe Wa Bunge Maalum la Katiba tunaotoka makundi mbalimbali na pia
tunaoamini katika kauli mbiu isemayo “TANZANIA KWANZA”, tunapenda kutoa
tamko rasmi la kuunga mkono hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais alipokuwa
akihutubia Bunge Maalum la Katiba Tarehe 20/03/2014 kama ifuatavyo:
Kwanza,
tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete, kwa hotuba yake aliyoitoa wakati akizundua Bunge Maalum
la Katiba tarehe 20 Machi 2014. Tunaamini Rais, kama Mkuu wa Nchi,
alikuwa na haki na wajibu wa kutoa mwelekeo na maono yake kuhusu Rasimu
ya Katiba na hatua hii tuliyonayo sasa ya kuipitia Rasimu kwenye Bunge
la Katiba. Tunafarijika kwamba hotuba hiyo imepokelewa vizuri na
Watanzania wengi kwenye kila kona ya nchi yetu na wengi wao wamekuwa
wakitutumia ujumbe wakituhimiza kuizingatia hotuba hiyo katika kutimiza
wajibu wetu.
Pili,
tunamshukuru Rais kwa uchambuzi wake wa kina wa Rasimu na ushauri wake
kwetu kuhusu haja ya kuweka taifa mbele, kushawishiana kwa hoja kuliko
kulazimisha hoja na haja ya kutunga Katiba itakayoliimarisha taifa letu
na kuendeleza umoja na ustawi wa Watanzania. Sisi wana TANZANIA KWANZA
tutaendelea kushawishi kwa hoja na wala hatutalazimisha.
Tatu,
tumeshangazwa na hamaki iliyoonyeshwa na baadhi ya wajumbe wenzetu
kuhusu hotuba ya Rais. Tunasikitishwa na kauli zao zenye mwelekeo wa
kuhujumu mchakato wa kupata Katiba mpya. Viongozi hawahawa wanaotoa
kauli hizi walionekana wakishangilia hotuba ya Rais pale aliposema yale
waliyokuwa wanakubaliana nayo. Iweje watishie vurugu na kususia kisa tu
Rais kasema baadhi ya mambo wasiyokubaliana nayo. Ustahamilivu wa
kidemokrasia, ustaarabu na hekima ya uongozi na utu uzima hautaki
hivyo.Hotuba ya Rais imeweka wazi faida na hasara za mifumo yote ya
Muungano wa Nchi yetu kwa hoja ili Watanzania wawe na fursa pana zaidi
ya kutafakari na mwisho kuamua. Mheshimiwa Rais ametimiza kauli yake ya
kushawishi kwa hoja na si kwa kulazimisha.
Nne, Hotuba
ya Mheshimiwa Rais haikuvuruga wala kuingilia mchakato uliopo mbele
yetu. Rais hakuingilia kanuni za Bunge maalum tulizozipitisha, Rais
hakubadilisha Sheria ya mabadiliko ya Katiba, Rais hakupiga kura kwenye
vifungu vya Katiba, Rais ameanza kwa kuipongeza Tume ya Mh. Jaji Warioba
na kuipongeza kw uwasilishaji wake. Alichokifanya Mheshimiwa Rais kama
kiongozi mkuu wa Nchi mwenye hekima na busara na uchungu wa Nchi yake na
kutambua dhamana aliyopewa na Watanzania wote bila kujali makundi
ameelezea faida na hasara za mifumo ya Serikali iliyowasilishwa kwenye
hotuba ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume. Rais katupa moyo na kutuhimiza
tumalize kazi haraka na tuifanye kwa weledi huku tukiweka maslahi ya
Taifa mbele. Hata pale alipotoa maoni na ushauri kuhusu baadhi ya
vifungu bado Mh.Rais alisisitiza kwamba uamuzi wa mwisho ni wetu sisi
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Tano,
dhana ya kuichambua na kuikosoa rasimu maana yake si kumdhalilisha
Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe wake. Msingi mzima wa kutolewa Rasimu hii
ni kwamba Wananchi tuichambue, tuikosoe, tuirekebishe, tuiboreshe na
hata ikibidi tuibadilishe na mwisho tutaipigia kura sote kwa pamoja.
Rasimu haikuletwa kama Msahafu wala Biblia na ndiyo maana zimewekwa
hatua mbili baada ya kazi ya tume kukamilika: BUNGE MAALUM LA KATIBA na
KURA YA MAONI YA WANANCHI. Rais akiwa mkuu wa Nchi, naye ana nafasi yake
katika mchakato wa Katiba. Sisi wana TANZANIA KWANZA, tunashukuru
kwamba Mh. Rais alitutanabahisha kuhusu maeneo muhimu ya kuzingatia
ambayo Tume haikuyaainisha kwa upana wake ikiwemo mipaka ya Nchi yetu.
Tunawapongeza Wajumbe wa tume kwa kazi waliyoifanya na kuikamilisha.
Kazi inayofuatia sasa ni uchambuzi wa Rasimu waliyoiwasilisha. Katika
hatua hii ya sasa ya Bunge la Katiba, Rasimu hii inaweza ikakosolewa na
hata inaweza kubadilishwa sana. Tunawasihi Wajumbe wa Tume waondokane na
dhana kwamba kazi yao inapojadiliwa tofauti na mapendekezo yao siyo
udhalilishaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sita,
Sisi Wajumbe wa Bunge Maalum, wana TANZANIA KWANZA ambao idadi yetu ni
zaidi ya Wajumbe 400 na ambao orodha yetu tutaitoa hivi karibuni kwa
wingi wetu na umoja wetu tunayo dhamira ya kutimiza wajibu wetu kwa
mujibu wa Sheria na kwa kuzingatia matarajio ya Watanzania. Tunawasihi
wale wenzetu ambao hawakuipenda hotuba ya Mheshimiwa Rais watulie,
waondoe hamaki na sote tushirikiane kuifanya kazi hii, kama wapo ambao
kitendo cha Rais kuja kuhutubia na kutoa uchambuzi wake kuhusu Rasimu,
kinawafanya wasitake tena kushiriki katika mchakato huu, basi uamuzi wao
huo waufanye kwa namna ambayo haitatukwaza au kutuzuia sisi wengine
tunaotaka kuendelea na shughuli hii ya mchakato wa Katiba. Tunawasihi
viongozi wa Bunge Maalum wasivumilie wala kuendekeza vitendo vya vurugu
za makusudi vitakavyozuia uendeshaji wa Bunge. Tunawasihi msiruhusu watu
wachache wakaliweka rehani Bunge Maalum ili kutengeneza mtaji wa
kisiasa. Tunawasihi Watanzania wawaone na kuwahukumu wale watakaotaka
kuvuruga au kukwamisha mchakato adhimu wa kupata Katiba mpya kisa
tu Mh. Rais kaja kuhutubia Bungeni.
Mwisho,
tunapenda kusisitiza kuhusu umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari katika
mchakato huu. Hiki ni kipindi muhimu sana katika uhai wa Taifa letu.
Wananchi wengi wanafuatilia mchakato huu kupitia vyombo vya habari.
Tunawasihi wamiliki, wahariri na waandishi wa habari wazingatie weledi
wa hali ya juu sana katika kuripoti mchakato huu. Wananchi wanapenda
kusikia, kuona na kusoma yanayojiri wala sio propaganda za wanasiasa au
makundi mbalimbali. Tunapenda kuvisihi vyombo vya habari
viwaunganishe Watanzania wote katika kipindi hiki muhimu na cha
kihistoria. Hata hivyo tunatoa shukrani zetu za dhati kwa vyombo vya
habari na wanahabari wote kwa ushiriki wao katika mchakato huu wa
Katiba. Tunazidi kuwasihi waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa,
kutokufanya kazi kwa kufuata propaganda za kisiasa au kufuata makundi,
kutoa mizania sawa kwa maoni tofauti bila kuegemea maoni ya kundi moja
au matakwa ya makundi fulani kwa kuwa mwisho wa siku sisi sote tuna
jukumu kubwa la kuhakikisha tunakuwa na Tanzania moja.
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Libariki Bunge Maalum la Katiba
“TANZANIA KWANZA”
Tunawashukuru kwa kutusikiliza.
0 comments :
Post a Comment