Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na
Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI)
wamefutiwa mashitaka na
mahakama ya wilaya ya
Mwanakwerekwe dhidi ya kesi ya
kufanya mkusanyiko bila ya kibali
iliofunguliwa Mei mwaka jana
visiwani Zanzibar.
Uamuzi huo umetolewa na Hakim
Ame Msaraka Pinja baada ya
kukamilika kusikilizwa kesi hiyo na
washitakiwa kuonekana hawana
hatia katika mashitaka yaliokuwa
yamefunguliwa na Mkurugenzi wa
Mashitaka Zanzibar, mwezi Mei
mwaka jana.
Hakimu Pinja amesema kwa
kuzingatia mashahidi wanne upande
wa mashitaka pamoja na
washitakiwa wenyewe
waliithibitishia mahakama kwamba
katika mkusanyiko wao hawakuwa
wakizungumzia mambo ya dini
isipokuwa Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar.
Amesema kwa msingi huo
washitakiwa hawakuhitaji kuwa na
kibali chochote cha kisheria kabla
ya kuandaa mkusanyiko huo kwa
vile walikuwa wakizungumzia
mambo ya Muungano na kwa msingi
huo hakuna shitaka linalowatia
hatiani na mahakama imetupilia
mbali dai hilo.
Amesema baada ya mahakama
kupitia jalada la kesi hiyo,
imeonekana washitakiwa hawana
hatia, “ninawaachia huru kwa
sababu kosa waliloshitakiwa
halikuhitaji kibali cha Mufti kabla ya
kuandaa mkusanyiko huo,” alisema
Hakimu Pinja.
Hata hivyo Hakimu huyo alisema
upande wa mashitaka wa Serikali
kama haujaridhika na uamuzi wa
mahakama hiyo unaweza kukata
rufaa mahakama ya mkoa ndani ya
siku 30 tangu kutolewa kwa uamuzi
huo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni
Farid Hadiy Ahmed Mussa Juma
Issa, Haji Sadif Haji, Suleima Juma
Suleiman, Fikirini Mjawaliwa
Fikirini na Abdallah Said Ali.
Washitakiwa walifunguliwa
mashitaka kwa kufanya mihadhara
ya Kiislam bila kibali cha Mufti
kinyume cha kifungu cha 6(1)(2)
cha kanuni za kuidhinisha na
kuratibu mihadhara
zinazotengenezwa chini ya kifungu
15(1) ya sheria Namba 9 ya mwaka
2001, kifungu cha 10(1)© na kifungu
cha 14(2) ya sheria namba 9 ya
mwaka 2001.
Ilidawa bila ya halali, Mei 26 mwaka
jana majira ya saa 3:30 huko katika
viwanja vya Lumumba wilaya ya
Mjini Unguja, washitakaiwa
walifanya mihadhara ya Kiislam bila
ya kuomba kibali cha Mufti wa
Zanzibar.
0 comments :
Post a Comment