Maombi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ya kuomba ufutiwa shtaka la
kukiuka uamuzi wa mahakama, yamebaki njiapanda baada ya Jamhuri
kuyawekea pingamizi la kisheria, ikiiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam iyatupilie mbali.
Sheikh Ponda, kupitia kwa Wakili wake Juma
Nassoro, aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya marejeo, akiiomba
mahakama hiyo ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Morogoro.
Maombi hayo yalitarajiwa kuanza kusikilizwa jana
lakini, Serikali iliwasilisha pingamizi hilo la awali na hivyo mahakama
hiyo ikalazimika kuanza kusikiliza pingamizi hilo kabla ya kuendelea na
maombi ya msingi. Pingamizi hili liliwasilishwa na Wakili wa Serikali
Mkuu (PSA), Bernard Kongola.
Wakili alidai kuwa hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ni batili kwa kuwa ina kasoro za kisheria.
Alibainisha kasoro hiyo kuwa ni kutokuwa na tarehe
ambayo kiapo hicho kilitolewa na kwamba hakuna mahali panapoonyesha
kuwa msimamizi wa kiapo alikuwa akimjua mla kiapo na wala kueleza kuwa
mla kiapo alitambulishwa kwake na nani.
Wakili Kongola alieleza kuwa hata kwenye hati ya
kiapo iliyoko katika jalada lililoko mahakamani inaonyesha kuwa kuna
kasoro hizo na kwamba walijiridhisha hivyo baaada ya kudurusu katika
jalada hilo la mahakamani.
“Mheshimiwa Jaji, dosari hizi haziwezi kurekebishika, kwa hiyo maombi yote ni batili,” alisema Wakili Kongola.
Hata hivyo, Wakili wa Ponda, Nassoro alisema kiapo
hicho ni sahihi na kimetimiza matakwa ya kisheria kwa kuwa nakala
aliyonayo inaonyesha kiapo hicho kilitolewa na Oktoba 8, 2013 na kwamba,
msimamizi wa kiapo alikuwa akimfahamu mla kiapo, ambaye ni Ubaidi
Hamidu.
Pia wakili Nassoro alisema Serikali haijatoa
ushahidi mahakamni kuonyesha kuwa kweli ilidurusu jalada la mahakama na
kubaini kuwa hati hiyo iliyoko mahakamani ina dosari hizo wala kueleza
ni lini alifanya hivyo hivyo.
Akijibu hoja hiyo Wakili Kongola alisisitiza kuwa
kiapo hicho ni batili kama walivyojiridhisha kwenye jalada la mahakama,
Novemba 21, 2013, na kwamba wanao ushahidi wa kutosha katika hilo. Baada
ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Rose Teemba anayesikiliza maombi hayo
aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 11
Blogger Comment
Facebook Comment