KATIKA hali isiyo ya kawaida mwanaume
mmoja mkazi wa mtaa wa Pangani kata ya Makorongoni katika Manispaa ya
Iringa Hamis Said maarufu kwa jina la Mwarabu amemuua kinyama mtoto
Raymond Ben Mangungu (2) kutoka na ugomvi wa kimapenzi kati yake na
mama wa mtoto huyo ambae kwake ni mpenzi wake.
Imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo wa
mauaji ya mtoto huyo alikuwa amelewa pombe kupita kiasi na si mara ya
kwanza kulewa kiasi hicho na kutishia kufanya mauaji dhidi ya mtoto
huyo wa kambo kwa kile alichokuwa akidai kuwa ni fedhea kwake kuishi na
mwanamke ambaye ana watoto wawili ambao si damu yake.
Wakizungumzia juu ya tukio hilo
mashuhuda wa tukio hilo kwa sharti la kutotaja majina yao walisema
kuwa imekuwa ni kawaida kwa Mwarabu kumpiga mwanamke huyo na familia
yake kwa madai kuwa hataki kuwaona watoto hao wakiendelea kuishi katika
nyumba hiyo ambayo ameipanga yeye.
"Huyu bwana Mwarabu alikuwa akifanya
kazi ya kuuza korosho mitaani na akirudi usiku amekuwa mkali kwa
mwanamke huyo ambae alikuwa akidai kuwa bado amekuwa na mahusiano na
baba wa watoto hao wawili .....hata hivyo sisi kama majirani
tumekuwa tukishindwa kuwaamua kutokana na mwanaume kuwa na tabia ya
kulewa pombe kupita kiasi na hata tukio hili tulijua ni kawaida yao"
Mtoto Tinito Mangungu (6) ambae ni kaka
na marehemu alisema kuwa baba yao huyo mdogo alifika usiku na kuwataka
wote kuamka kitandani na kuwa hakuna mtu atakayelala katika chumba
hicho kama si damu yake.
"Baba mdogo (Mwarabu) alirudi usiku
akiwa amelewa na kusema hakuna mtu kulala kitandani na kuanza kumpiga
mama kwa meza na viti huku sisi tukilia kumtaka asimpige mama
yetu....baada ya hapo alimchukua mdogo wangu na kuanza kumkaba shingo
na kumwacha kitandani akiwa amelala bila kuamka hadi sasa mama anasema
amekufa"
Akielezea juu ya mkasa huo
uliosababisha mauaji ya mtoto Raymond mama mzazi wa mtoto huyo Bi Kudra
Kahemela (23) alisema kuwa kwa upande wake baada ya kutishiwa kuuawa
kwa kipigo alifanikiwa kukimbia katika chumba hicho na kwenda
kujificha nje na baada ya muda mwanaume huyo alianza kutapika na pale
alipoingia kutaka kumsaidia ndipo alipopigwa na kuamua kukimbia kwenda
kulala nje ya nyumba hiyo kwa kujiegesha katika nguzo ya umeme iliyopo
nyumba ya pili karibu na nyumba ya shekhe wa mkoa Juma Alli Tagalile
Alisema kuwa asubuhi aliingia katika
chumba hicho baada ya mwanaume huyo kutoka kwenda katika kilabu cha
pombe za kienyeji cha Tulivu kuendelea kunywa pombe na kumkuta mtoto
huyo akiwa amelala bila kutikisika
"Mimi nilijua kama mtoto amelala tu ama
amezimia ila baada ya kuwaita watu wazima akiwemo mama yangu mzazi
ndipo nilipobaini kuwa mtoto wangu Ray amefariki dunia na ndipo
nilipomfuata na kumweleza juu ya tukio hilo ila bado aliendelea kunywa
pombe na kudai kuwa mtoto huyo amezimia kwa kelele za usiku"
Alisema baada ya hapo mwanaume huyo
alikimbia hadi Ilala kwa wakwe zake na kuomba msamaha na kusuruhishwa
ugomvi wao ila wakati huo mtego wa kukamatwa ukiwekwa ndipo alipokimbia
kusikojulikana.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia
mtoto huyo akiwa amekufa katika kitanda cha wazazi wake huku chini ya
chumba hicho thamani mbali mbali pamoja na vyombo vikiwa vimevunjika
kutokana na ugomvi huo
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo wa
Pangani kata ya Makorongini Bw. Salum Kibaya amethibitisha juu ya kifo
cha mtoto huyo na kuwa baada ya tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa
kuamkia leo Jumamosi Desemba 14 mwaka huu alilazimika kwenda kituo cha
polisi cha stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani na kuwajulisha juu ya
tukio hilo na kufika eneo la tukio.
Bw Kibaya alithibitisha pia kuwa
ugomvi kati ya wapenzi hao si wa kwanza kutokea japo kwa maelezo ya
mwanamke huyo alikuwa mbioni kuolewa na mwanaume huyo na hivyo kuwa na
wanaume wawili akiwemo mzazi mwenzake ambae kwa sasa anaishi eneo la Don
Bosco mjini hapa.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa huku jeshi la polisi likiwahoji
mama wa mtoto huyo, kaka wa mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye ni mkazi
wa Mlandizi Kibaha Jijini Dar es Salaam na mama mzazi wa mtoto
aliyepoteza maisha.
0 comments :
Post a Comment