-->

HALI AFRIKA KATI YAENDELEA KUWA TETE

Hali imeanza kutulia kidogo katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika kati-Bangui,baada ya mapigano ya umwagaji damu kati ya makundi ya imani tofauti za kidini.Hata hivyo jeshi la Ufaransa linasema hali bado inatisha.
Wanajeshi wa Ufaransa wapiga doria mjini Bangui
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema mpango wa kuwapokonya silaha wafuasi wa makundi tofauti ya wanamgambo unaanza hii leo.Ameonya jeshi la Ufaransa linaweza kutumia nguvu kuwalazimisha wanamgambo wazisalimishe silaha zao.Katika mahojiano na kituo cha matangazo cha RTL waziri huyo wa ulinzi wa Ufaransa amesema baadhi ya makundi ya wanamgambo wameanza kuchanganyika na raia wa kawaida na kusababisha "vurugu".
Wakaazi wa mji mkuu Bangui wamezungumzia kuhusu milio ya hapa na pale ya risasi katika baadhi ya mitaa ya mji huo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa shirika la haki za binaadamu la Jamhuri ya Afrika kati,Joseph Bindoumi,wanamgambo wa Seleka ambao wengi wao ni waislam,bado wangalipo mjini B angui.
"Hali ni tulivu lakini inatisha" amesema msemaji wa jeshi la Ufaransa kanali Gilles Jaron akiwa mjini Paris.Ufaransa imeamua kutuma jumla ya wanajeshi 1600 katika Jamhuri ya Afrika kati,1200 kati yao mjini Bangui.
Uchaguzi uitishwe haraka
Rais wa Ufaransa Francois Hollande akitangaza lengo la wanajeshi wa nchi yake katika jamhuri ya Afrika kati
Akitangaza jukumu la wanajeshi wa Ufaransa katika jamhuri ya Afrika kati,rais Francois Hollande amezungumzia kuhusu"Opereshini itakayofanyika haraka,itakayoleta tija na ambayo itabidi itekelezwe kwa ushirikiano pamoja na vikosi vya Afrika ili kuyavunja nguvu makundi yanayomiliki silaha,kurejesha utulivu na kurahisisha, wakati ukiwadia, kuitisha uchaguzi huru na wa vyama vingi katika nchi hiyo."
Mjini Bangui kwenyewe wanajeshi wa Ufaransa wanaendelea kupiga doria katika kila pembe ya mji huo,wakifuatana kwa mguu na baadhi ya wanajeshi wa kikosi cha nchi za Afrika Misca watakaoongezwa toka 2500 hivi sasa hadi kufikia wanajeshi 6000.
Wanajeshi wa Ufaransa wamewekwa pia katika maeneo ya kaskazini na magharibi ya Jamhuri ya Afrika kati.
Rais wa mpito Michel Djotodia anaelaumiwa kwa kushindwa kuwadhibiti wanamgambo wa kiislam wanaosemekana kuwahujumu wakristo ambao ndio walio wengi nchini humo ametangaza siku tatu za maombolezo na kuahidi kuitisha uchaguzi mwakani badala ya mwaka 2015.
Mshikamano badala ya Mtengano
Wananchi walioyapa kisogo maskani yao wakikimbia mapigano katika jamhuri ya Afrika kati
Waumini wa kikristo walikusanyika makanisani jana kuwakumbuka wahanga wa mapigano ya siku za nyuma kati ya makundi ya wanamgambo wakikristo na waislamu."Tunabidi tuugeuze mkondo wa matumizi ya nguvu na vita uwe mkondo wa amani na mshikamanao" amesema askofu mkuu wa Bangui Dieudonné Nzapalainga katika misa iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini mjini Bangui.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
CHANZO:DW SWAHILI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment