MMOJA wa wajumbe wa Zanzibar wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba
amembana na kumshika uwongo Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta,
akisema yeye hakupiga kura lakini mwenyekiti huyo na wenzake walichomeka
jina lake ili kulazimisha upatikanaji wa theluthi mbili ya Wazanzibari.
Mjumbe huyo ambaye ni Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi,
Haji Ambar Khamis, amesema kuwa ameshangaa kukuta jina lake kwenye
orodha ya majina ya wajumbe waliopiga kura kupitisha katiba
inayopendekezwa. Jina la Khamis ni nambari 39 katika ukurasa wa 209.Akizungumza na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya chama, Ilala, Dar es Salaam, huku akitokwa na machozi, Khamis alisema amesikitishwa na tukio hilo, na mpaka sasa hana amani, na anahofia maisha yake.
“Mimi sijashiriki kabisa bunge hilo tangu Aprili, na wala sijapiga kura. Sijui nini kinaendelea mpaka jina langu likawekwa,” alisema, halafu akakatiza, akaendelea kulia.
Wenzake walimtoa nje. Baadaye walieleza waandishi wa habari kuwa Khamis alipata mshtuko wa moyo, wakampeleka hospitali ya Amana.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisisitiza kuwa Khamis amewathibitishia kwa dhati kwamba hakuwahi kushiriki katika kuandaa wala kupitisha Katiba inayopendekezwa tangu BMK liliporejea kwa mara ya pili Agosti 5 mwaka huu.
“Kitendo cha kuandika jina la kiongozi wetu wa taifa katika katiba hiyo bila ridhaa wala ushiriki wake ni ulaghai uliokithiri kwa Watanzania na dunia kwa ujumla. Kitendo hicho ni udhalilishaji kwa ndugu Haji Ambar Khamis yeye binafsi, familia yake, chama chetu, viongozi na wanachama wote wa UKAWA pamoja Watanzania kwa ujumla wao,” alisema.
Mbatia alisema baada ya kupata nakala ya katiba hiyo inayopendekezwa, yeye na wenzake waligundua kuwa jina la kiongozi wao lilikuwa miongoni mwa wajumbe waliopiga kura kupitisha katiba hiyo.
Alisema walipomuuliza kuhusu ushiriki wake kwenye mchakato huo, alikanusha kwa kiapo.
Mbatia alisema pia kuna ushahidi wa kutosha kwamba muda wote tangu Aprili mwaka huu, Khamis hakushiriki katika vikao vya BMK.
Kwa mujibu wa Mbatia, chama chao kinaamini kuwa kitendo hicho kimefanywa kwa makusudi na viongozi wakuu wa BMK ili kukidhi haja zao binafsi na kulaghai umma wa Watanzania, na ni ishara hatarishi kwa usalama wa taifa kwani kinaweza kusababisha machafuko nchini.
Alisema uongozi wa chama umepokea Katiba inayopendekezwa kwa fedheha na mshtuko mkubwa na unaamini kuwa kuna mkakati mbaya na wa makusudi wa kusambaratisha chama chao.
“Imani hii inatokana na ukweli kwamba tangu mchakato wa kupata katiba umeanza, tayari tumeshapoteza viongozi wetu wawili kwa namna za kutatanisha, na hakuna majibu yanayoeleweka kutoka kwa vyombo vya dola,” alisema.
Alisema miongoni mwa viashiria hivyo ni mauaji ya kikatili na ya kinyama ya aliyekuwa kiongozi wa chama hicho Dk. Edmund Sengondo Mvungi yaliyotokea Novemba mwaka jana, na aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Mara, Stephen Sebeki yaliyotokea Julai mwaka huu.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, wana hofu kubwa juu ya usalama wa chama ngazi mbalimbali, wanachama wote wa chama hicho na wanasiasa wenzao wa UKAWA.
Alisema chama chake kitafanya utafiti wa kina na kuchukua hatua za kisheria. Wanajadiliana na jopo la wanasheria juu ya suala hilo.
Mbatia aliitaka serikali iwajibishe wote walioshiriki kubuni na kuandaa mkakati wa kuchomeka jina la Khamis katika orodha ya wajumbe wa Zanzibar.
Vile vile, alimtaka Sitta, amuombe radhi kiongozi wao huyo, familia yake, ndugu, rafiki zake, mashabiki wake, chama hicho, viongozi wenza wa vyama vinavyounda UKAWA pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa hujuma walizomfanyia.
“Kisha tunaitaka serikali itoe tamko la kuhakikisha usalama wa kutosha kwa kiongozi wetu, familia yake, viongozi wote wa NCCR pamoja na wanasiasa wote nchini na familia zao. Pia watuhakikishie kwamba matukio ya mauaji kama yaliyowahi kuwatokea viongozi wetu hao wawili hayatatokea tena,” alisema.
Bunge Maalum la Katiba lilimalizika Oktoba 4 mwaka huu, na kuikabidhi katiba hiyo inayopendekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete, Oktoba 8 mwaka huu.
Kumekuwapo na utata juu ya mfumo aliotumia Sitta kupata theluthi mbili ya wajumbe wa Zanzibar. Baadhi ya wachambuzi wamesisitiza mara kadhaa kwamba idadi ya wapiga kura kutoka Zanzibar ilighushiwa.
Utata ulitokana na kauli za Sitta mwenyewe, kwani awali alisema idadi ya wajumbe wote wa BMK ni 629 (Tanganyika 419 na Zanzibar 210). Idadi hiyo iliongezeka baadaye wakati wa kutangaza matokeo, ikawa 219 kwa wajumbe wa Zanzibar.
Theluthi mbili za wajumbe 210, ni 140. Wajumbe wa kundi linaloojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), akiwamo Khamis, walikuwa 67. Waliopiga kura za wazi za “hapana” walikuwa wanane, na kufikisha wajumbe 75. Kwa idadi hiyo tu, wapiga kura kutoka Zanzibar walibaki 135.
Kwa idadi ya wajumbe 219, theluthi mbili ingekuwa ni 146, lakini kwa kuzingatia kura za “hapana” zilizopigwa, idadi inayobaki ni 144. Kuibuka kwa mjumbe mpya na madai haya, kunaongeza utata juu ya theluthi mbili iliyotangazwa na Sitta juu ya idadi ya wajumbe waliopitisha katiba hiyo.
Sitta alipotafutwa ili atoe ufafanuzi, simu yake iliita lakini hakupokea. Baadaye, mwandishi alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno -fyanda lina maana ya –bana, -finya. Hiki ni kibano kipya kwa Sitta, ambaye kwa siku kadhaa amekuwa katika mzozo na viongozi wa dini na wanasiasa wenzake, hasa wa upinzani na makundi kadhaa katika jamii.
source: FURAHIA MAISHA BLOG
0 comments :
Post a Comment