-->

ACT TANZANIA WATOA TAARIFA KWA UMMA


TAARIFA KWA UMMA

Maazimio ya Mkutano wa Tatu wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Tanzania Uliofanyika Jumamosi Tarehe 25 Oktoba 2014 katika Hoteli ya Vina Jijini Dar es Salaam

Kamati Kuu ya ACT-Tanzania ilifanya mkutano wake wa tatu siku ya Jumamosi tarehe 25 Oktoba 2014 katika Hoteli ya Vina Jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilijadili na kutoa maazimio kuhusu hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kama ifuatavyo:

1Kamati Kuu imejadili hitimisho la mchakato wa Katiba Mpya katika ngazi ya Bunge Maalumu la Katiba. Kamati Kuu imeendelea kusikitishwa na kushindikana kupatikana kwa maridhiano baina ya makundi mbalimbali ya kisiasa nchini kuhusu mchakato na maudhui ya Katiba Mpya. Kamati Kuu imesikitishwa zaidi na uamuzi wa Chama cha Mapinduzi na serikali yake wa kuteka na kuburuza mchakato wa katiba kwa kuegemea matakwa ya sheria bila kujali uhalali mpana wa kisiasa na kijamii nchini.
2.Kamati Kuu imezingatia kuwa mchakato wa katiba mpya umeitimishwa katika Bunge Maalumu la Katiba katika mtindo ambao umeacha mgawanyika na mpasuko mkubwa wa kisiasa na kijamii nchini badala ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa, ambalo ndilo lengo la msingi la mchakato wenyewe.
3.Kutokana maelezo ya hapo juu (1 & 2), bila kujali uzuri au ubaya wa maudhui yaliyomo katika Katiba Inayopendekezwa, Chama cha ACT-Tanzania kitawashawishi wananchi kuikataa katiba inayopendekezwa kwa kupiga KURA YA HAPANA katika kura ya maoni.
4.Kamati Kuu imesikitishwa na kuendelea kusuasua kwa kutolewa Ripoti kuhusu uchunguzi wa wizi wa fedha za umma uliofanyika kupitia akaunti ya Escrow iliyotokana na mgogoro baina ya TANESCO na IPTL. Kusuasua kutolewa kwa Ripoti ya Uchunguzu kumesababisha kukwamisha bajeti ya serikali kwa kuwa wafadhili wamesimamisha misaada muhimu kwa bajeti ya mwaka huu. Kamati Kuu inamtaka CAG atoe Ripoti yake kwa Kamati ya PAC kwa ratiba iliyopangwa. Aidha Kamati Kuu inawaunga mkono wabunge wote walio mbele katika kupigania sheria kuchukua mkondo wake katika sakata hili. Kwa kipekee, Kamati Kuu imempongeza Mhe David Kafulila kwa ujasiri wake katika kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa wote waliohusika na wizi wa fedha za umma kupitia kivuli cha akaunti ya Escrow. Tunawahimiza wabunge wazalendo wamuunge mkono mbunge mwenzao Mhe Kafulila katika kuhakikisha kwamba uwajibikaji unapatikana katika kashfa hii kubwa kabisa kuikumba nchi yetu.
5.Kamati Kuu imepokea taarifa ya kuhusu ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo. Kamati Kuu imesikitishwa na taarifa kwamba zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini hawatapata mikopo. Kamati Kuu haikubaliani na hali hii na imewahimiza wanafunzi, vijana na wadau wa elimu nchini kuungana na chama cha ACT-Tanzania katika kuishinikiza serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanapatiwa mikopo ili wawezi kujipatia elimu ya juu ambayo inahitajika sana kwa mustakabali wan chi yetu.
6.Uzinduzi rasmi wa chama utafanyika katika jiji la Dar es salaam mnamo tarehe 05 Desemba mwaka huu. Kwa mujibu wa katiba ya ACT TANZANIA kuna mkutano mkuu wa kidemokrasia (NATIONAL DEMOCRATIC CONGRESS). Mkutano wa kwanza wa namna hiyo utafanyika Desemba 5. Tunatoa wito kwa wanachama wote Tanzania kuanza maandalizi ya kushiriki mkutano huu.
7.Kutakuwa na mapokezi makubwa na mkutano mkubwa wa kwanza wa hadhara katika jiji la mwanza siku inayofuata tarehe 06 dec 2014. Wito kwa wakazi wa jiji kufanya maandalizi makubwa kukipokea chama mbadala
8.Mwisho Kamati kuu imeazimia kushiriki kwa nguvu zote uchaguzi serikali za mitaa na imeridhika na maandalizi ya kupata wagombea katika ngazi ya mitaa,vijiji na vitongoji.


Samson Mwigamba
Katibu Mkuu
Jumatatu, 27 Oktoba 2014
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment