Risasi zarindima ofisi ya mbunge, zazua taharuki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul
TAHARUKI imetokea kwenye ofisi ya Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Lucy Nkya (CCM) baada ya risasi mbili kufyatuka kutoka kwenye bastola ya mtoto wake, Jonas Nkya.
Milio ya risasi iliwashitua wananchi waliokuwa karibu na ofisi za taasisi isiyo ya kiserikali ya Faraja Trust, inayoshughulika na elimu ya Ukimwi na ushauri nasaha inayomilikiwa na mbunge huyo iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Hali hiyo iliwafanya wananchi kukimbia huku na kule na baadaye kujazana nje ya ofisi hizo. Dk Nkya aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii. Kwa sasa ni Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro.
Watu waliokuwa eneo la tukio hilo, walidai kuwa Jonas alikuwa na mzozo na mama yake kwenye geti la ofisi hizo na ndipo alipofyatua risasi mbili hewani.
Hata hivyo, walidai hawakufahamu mzozo wao ulihusu nini zaidi ya kuwaona wakijibishana. Inadaiwa baada ya risasi kufyatuka, mama yake alikimbilia Polisi kutoa maelezo.
Hata hivyo, Jonas na mama yake, Lucy Nkya, wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, jana, walikanusha kuwa na mzozo wowote.
Jonas alieleza kuwa risasi zilifyatuka zenyewe baada ya bastola yake kuanguka chini. Jonas aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Morogoro.
Kwa sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM kupitia Kundi la Vijana. Jonas alisema bastola yake ilikuwa kwenye mfuko wa suruali na ilidondoka chini na kujifyatua risasi mbili, ambazo zilileta taharuki eneo la ofisi na kwa majirani.
“Sikuishika bastola hiyo mkononi mwangu, ila nikiwa kwenye geti la ofisi ya Faraja ili kuiacha gari ndogo na kuchukua gari kubwa kwa ajili ya kwenda shamba, ndipo bastola ilidondoka kutoka kwenye mfuko wa suruali na kujifyatua,” alisema.
Alisema ni kawaida yake kila Jumamosi anakwenda shamba na kuchukua silaha hiyo, ambayo ina uwezo wa kuhifadhi risasi 15. Alisisitiza hakuwa na ugomvi wa kifamilia na mama yake, ambaye anaishi naye eneo moja kwa ajili ya kumuuguza baba yake ambaye ni mgonjwa.
“Sina ugomvi na mama yangu wala mtu mwingine, siwezi kufikia hapo kwa kumdhuru mama yangu, wala sikurushiana risasi na mama yangu na kungekuwa na ugomvi tungemalizia nyumbani.
“Wakati nashuka pale ofisini, ghafla bastola ilijifyatua na kutoa risasi mbili...majirani waliposikia milio hiyo walitaharuki na kufikiri ni majambazi na mimi sikujua kama ndani ya ofisi yupo mama yangu akiwa na watu wake (wageni),” alisema Jonas.
Alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, alibakia hapo kwa muda wa dakika 15 kusubiri Polisi, lakini baadaye alitoka kwenda shamba. Polisi walifika baadaye kuchukua maelezo kuhusu jambo hilo.
Alisema hakukimbia tukio hilo kama watu wanavyosema na kwamba silaha aliyonayo, anaimiliki kihalali baada ya kuisajili jijini Dar es Salaam. Kwa upande wake, Lucy Nkya aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa wakati wa tukio hilo, hakuwepo eneo hilo.
Alisema alikuwa katika zanahati moja (hakuitaja) akiwahudumia wagonjwa baada ya muuguzi aliyepo kupata matatizo. Alisema baada ya kufika ofisini hapo, alikuta watu wakielezea tukio hilo la kufyatuliwa kwa risasi mbili kutoka katika silaha ya mwanawe.
Alisema hana ugomvi kati yake na mwanawe huyo, kwani kwa sasa anaishi nyumbani kwake kwa ajili ya kumuuguza baba yake , hivyo kama kungekuwepo na ugomvi, wangeumaliza nyumbani na si ofisini.
Alisema mwanawe alikwenda ofisini, kuchukua gari kwenda shamba na ndipo ilielezwa bastola yake ilidondoka na kufyatua risasi mbili hewani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alithibitisha kwa njia ya simu akiwa nje ya mkoa, kuhusu kutokea kwa tukio la kufyatuliwa kwa risasi hizo. Alisema polisi wake walikwenda eneo la tukio na kupata maelezo ya Lucy Nkya.
“Nipo safarini kwenda Mlandizi , timu ya Polisi ‘inacheza’ hapo, ila tukio hili limetokea na nimearifiwa na wasaidizi wangu, tutalitolea maelezo ya kina baada ya kufanyika kwa uchugunzi na kujiridhisha vya kutosha,” alisema Kamanda huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo , tukio hilo ni la jana saa 5:00 asubuhi. Alisisitiza kwamba Polisi inafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama rirasi hizo, zilijifyatua zenyewe kwa bahati mbaya, ama zilifyatuliwa na mhusika. Alisema baada ya uchunguzi huo, taarifa kamili zitatolewa na hatua zitachukuliwa.HABARILEO
0 comments :
Post a Comment