-->

CAG YAFICHUO MADUDU KWENYE MAPATO NA MATUMIZI YA VYAMA VYA SIASA TANZANIA

 
NAPE NNAUYE.


SIKU chache baada ya kuanikwa kwa taarifa ya ukaguzi wa mahesabu uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikionesha dosari katika hesabu za mapato na matumizi ya karibu vyama vyote vya siasa nchini, baadhi ya vyama hivyo vimekiri udhaifu na kuahidi kufanya marekebisho kulingana na sheria za fedha zinavyoelekeza.


Aidha, vingine vimesema pamoja na ukweli huo, baadhi ya masharti ya CAG ni magumu na hayatekelezeki.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni miongoni mwa vyama 12 ambavyo vimepata hati yenye mashaka, kimesema baadhi ya masharti na maelekezo ya CAG hayatekelezeki likiwemo la kukitaka kuhesabu mali zake zote ambazo zimetapakaa nchi nzima.

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baadhi ya kasoro wanazirekebisha na kwamba zipo baadhi hazitekelezeki kwa kuwa na ugumu wa kuweza kuzipata hasa akaunti ambazo kwa masharti ya benki zinaeleza kuwa jukumu la kuendesha akaunti hizo ni la viongozi wa ngazi husika.

Vyama 12, vilivyokaguliwa ni pamoja na CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR- Mageuzi, TLP, NLD, UMD, ADC, APPT-Maendeleo, SAU na Chauma.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumzia suala hilo alisema, CCM tangu mwaka 1977 imekuwa ikikaguliwa na kwamba dosari zilizoonekana kupitia ripoti ya CAG, zimetokana na mgongano wa mambo kati ya sheria ya ukaguzi wa hesabu ya Serikali na taratibu za chama.

“Nikiri kwamba kuna kasoro, ila hizo zinatokana na uwepo wa mabadiliko, kuna vitu sheria ya ukaguzi ya serikali imebadilika, ila sisi chama hakijabadilisha, hivyo kwenye ukaguzi lazima mambo yanapishana, na huko kupishana ndiko kumeleta shida,’’ alisema.

Aliongeza kwa kutoa mfano kuwa, kuna kipengele katika sheria hiyo ya ukaguzi kinataka vyama vitaje mali za chama jambo ambalo alisema ili CCM iweze kutaja mali zake zote ni lazima wawe na Sh bilioni moja kwa ajili ya kufanya tathmini ya mali za chama hicho zilizotapakaa nchi mzima.

Alisema ili wamridhishe CAG kama alivyoagiza na akahoji "sasa hizo fedha tunazitoa wapi, ilhali ruzuku tunayopata ni chini ya bilioni moja?”

Alisema jambo kama hilo lina changamoto kutekelezeka ila dosari nyingine zinaweza kutekelezeka kwa chama kubadilisha taratibu zake na kufuata matakwa ya Sheria ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Serikali.

Aidha alisema pamoja na kasoro hizo wao CCM wamezikubali na wanajipanga kufanya marekebisho ili kufuata matakwa ya sheria husika na kwamba katika kutekeleza hayo kuna baadhi ya mambo ni magumu kutekelezeka.

"Ila sisi kama chama tunajipanga kuona mapungufu ni yapi na tunaondokaje hapo,” alisema Nape.

Kwa upande wa CUF, Mkurugenzi wa fedha na Uchumi Joram Bashange, alisema wamepokea ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu yao na kwamba wanakiri kuwepo kwa mapungufu hayo na wanayafanyia kazi, ili kuboresha hesabu zao.

Bashange alisema zipo kasoro kadhaa zilizoonekana kwenye hesabu zao ambazo ni pamoja na kufanyia maboresho kanuni za chama hicho ili kwenye masuala ya fedha kuwe na mpangilio mzuri zaidi wa utoaji fedha na nyaraka zake.

Pia kwenye kipengele cha manunuzi, wameagizwa kufanya maboresho ili wakati wa kulipa au kufanya manunuzi wawe na nyaraka zinazoonesha manunuzi hayo na bei badala ya kuambatanisha vitu vingi kwa pamoja bila nyaraka.

“Tumepewa maelekezo tunayafanyia kazi, kwa maana sheria ya ukaguzi inataka tufanye hivyo na sisi tunatii na tunaboresha kwa kuwa baadhi ya mambo kwenye sheria hiyo na taratibu zetu vilipishana, ila kwa maelekezo ya CAG , tunarekebisha,” alisema Bashange.

Akizungumzia ukaguzi wa hesabu za Chadema, Msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema Oktoba 5, mwaka huu, Chadema ilipokea taarifa rasmi ya ukaguzi wa hesabu zinazoishia Juni 30 mwaka 2012, na ile ya Juni 30 mwaka 2013 kutoka kwa CAG.

Katika ripoti hiyo ilibainisha chama hicho kina akaunti zaidi ya 200 zikihusishwa zile zinazoendeshwa na makao makuu, kanda, mikoa, wilaya, majimbo na hata ngazi za chini na kuainisha kasoro kadhaa zilizosababisha wapate hati yenye mashaka.

Alisema mashaka ya CAG, pia yamesimama katika salio la kufungia vitabu kutohusisha akaunti zote zenye jina la chama na kwamba, inawezekana akaunti hizo zilikuwa na fedha ambazo chama kinaweza kubadilisha kiasi kilichotajwa.

Kwa mujibu wa Makene, baadhi ya kasoro wanazirekebisha na kwamba zipo baadhi hazitekelezeki kwa kuwa na ugumu wa kuweza kuzipata kwa kile alichosema masharti ya benki yanaeleza kuwa, wenye jukumu la kuendesha akaunti hizo ni viongozi wa ngazi husika.

Hata hivyo alisema ripoti ya CAG, wameipokea kama sehemu muhimu ya kuboresha ujenzi wa chama kama taasisi ya kudumu na inayokua, na kwamba changamoto zote alizoziainisha watazifanyia kazi.

Hivi karibuni, Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi, akitoa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema vyama 12 vilivyokaguliwa hesabu zake na CAG, kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo vimepata hati zenye mashaka na hakuna chama kilichopata hati safi.

HABARILEO
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment