JK ANATAMANI KUACHA MADARAKA.
Aona muda wake umekawia kuisha..................
RAIS Jakaya Kikwete amesema mfumo
unaotumika Tanzania ambako Rais
anatumikia nafasi ya uongozi kwa muhula
wa miaka mitano na si zaidi ya miaka 10 ni
mzuri na unaovutia kwa sababu unaiwezesha
nchi kupata fikra na mawazo mapya.
Aidha, Rais Kikwete amesema, anaamini
Tanzania itapata Rais bora zaidi kuliko yeye,
atayeiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa
kasi kubwa zaidi.
Rais Kikwete pia amesema, ana hamu
kumaliza muda wake wa uongozi ili arudi
kijijini kushughulika na wajuu wake na
mifugo yake. Rais Kikwete ametoa kauli hiyo
mjini Beijing, China, wakati akizungumza na
mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi
zao katika China.
Mkutano huo uliofanyika kwenye Nyumba ya
Kufikia Wageni wa Serikali ya China ya
Diaoyutai, ulikuwa shughuli ya kwanza ya
Rais Kikwete katika ziara yake rasmi ya siku
sita ya Jamhuri ya Watu wa China ambako
amealikwa na Rais Xi Jinping.
Wakati wa maswali na majibu, Balozi Sola
Onadipe, Naibu Balozi wa Nigeria katika
China, alishangazwa na kauli ya Rais
Kikwete kuwa anatamani amalize muda
wake wa uongozi ili astaafu na kusema kuwa
lingekuwa jambo la maana kwa Afrika kama
viongozi wengine wangekuwa na mawazo ya
namna hiyo ya kuheshimu Katiba za nchi
zao na kung’atuka kwenye uongozi muda
wao unapowadia.
Rais Kikwete amemwambia Balozi huyo:” Ni
kweli naona kama muda hauendi kwa kasi
ya kutosha ili niweze kuwa raia wa kawaida
na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na
mbuzi wangu na nilime mananasi yangu kwa
nafasi ya kutosha. Lakini Mheshimiwa Balozi
usishangazwe na utayari wangu kuondoka
katika uongozi.”
“Kwanza utaratibu huu wa miaka mitano
ama miaka 10 ni utaratibu wa Kikatiba, ni
jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna
kishawishi cha kulibadilisha. Pili, kazi hii ya
Urais ni kazi ngumu sana. Kwa hakika,
binafsi nawaonea gele sana wenye nguvu na
ubavu wa kutaka kubakia kwenye kazi hii
kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi
kuliko mimi,” amesema Rais Kikwete na
kuongeza:
“ Lakini pia kuna uzuri katika mfumo huu wa
kwetu kwa sababu kila baada ya miaka
mitano na hata kama ni baada ya kila miaka
kumi, anaingia mtu mwingine madarakani
akiwa na fikra mpya na mawazo mapya.”
“Mfumo huu ni mfumo unaoniridhisha sana
na wala hakuna kinachonishawishi nibakie
katika madaraka zaidi ya muda wangu
kikatiba. Nina hakika, nchi yetu itapata
kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi,
kuongoza vizuri nchi yetu.”
Rais Kikwete pia amesema kuwa si busara
pia kwa kiongozi kuwasikiliza wale
wanaoshauri wakisema kuwa akiondoka
madarakani nchi itavurugika.
“Kwa hakika, hawa wanatetea maslahi yao tu
wakisema kuwa ukiondoka wewe
madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi
ama mawaziri ama nafasi nyingine yoyote.”
0 comments :
Post a Comment