STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi hatakuwepo kabisa kwenye kambi ya timu
hiyo nchini Afrika Kusini kutokana na mechi mbili za timu yake ya Taifa
ya Uganda ndani ya kipindi kifupi.
Lakini hiyo ikaushie, ishu ni kwamba uongozi wa Simba umethibitisha
kwamba madaktari wameshauri mchezaji huyo asipande usafiri wowote wa
majini kama wanayapenda maisha yake. Wameshauri atumie nchi kavu na
angani tu.
Uchunguzi wa Mwanaspoti awali ulibaini kwamba Okwi tangu atue katika
kikosi hicho msimu huu akitokea Yanga hakuwahi kupanda boti kama
wachezaji wenzake wakati wakienda na kurudi kambini Zanzibar hali ambayo
ilianza kuzua maswali kwa baadhi ya wachezaji kwamba Okwi anadekezwa
zaidi na uongozi kwa kupewa huduma maalumu.
Habari
za ndani zinadai kwamba kumekuwa na minong’ono ya chini kwa chini baina
ya wachezaji wakihoji hali hiyo bila majibu ingawa baadhi ya wakongwe
waliwaridhisha kwamba labda suala la ndege ni makubaliano kwenye mkataba
wake wa kazi.
Wachezaji waliocheza naye siku za nyuma walidai kwamba tangu atue Simba
miaka ya nyuma usafiri wake ulikuwa ni ndege na aliwahi kujaribu maji
akapata matatizo.
“Hao wanaoshangaa hawajui, watakuwa wageni lakini hata kama wageni hivi
karibuni tuliwaambia kwamba siyo kipindi hiki tu hata huko nyuma Okwi
alikuwa hapandi boti kutokana na kwamba aliwahi kupata matatizo mara
moja alivyotumia usafiri huo,” alisema mmoja wa viongozi wakongwe na
mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba kwa sasa.
Bosi wa Simba Tanzania nzima, Rais Evans Aveva alithibitisha kwamba Okwi
hadekezwi ni hali halisi na ushauri wa daktari wanaufanyia kazi.
“Nikweli Okwi hatumii usafiri wa maji, hili si jambo geni ni la muda
mrefu na tumekuwa tukilazimika atumie usafiri wa ndege kila tunapoelekea
Zanzibar ikiwa ni sehemu ya ushauri wa madaktari ambao walitushauri,
hivyo baada ya kubaini matatizo fulani kwa mchezaji wetu,” alisisitiza
Aveva huku akiongeza kwamba hakuna mchezaji spesho Simba, wote ni sawa.
0 comments :
Post a Comment