Arusha. Polisi, kwa kushirikiana na maofisa wa Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya, imekamata magunia 267 ya bangi katika vijiji vya Olkokola na Kisimiri Juu wilayani Arumeru.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa licha ya kukamata bangi hiyo yenye uzito wa kilo 9,102, wameteketeza ekari moja na robo tatu ya shamba la miche hiyo.
Alisema bangi hiyo ilikamatwa katika operesheni iliyofanyika kwenye vijiji hivyo, Oktoba 28 na 29. Alisema magunia hayo ya bangi, yalikutwa kwenye nyumba za watu na kwenye makorongo, tayari kusafirishwa ndani na nje ya nchi. Alisema wamiliki wa magunia hayo walikimbia .
“Msako bado unaendelea...wananchi na viongozi wa serikali za vijiji hivi waache kilimo hiki kwa kuwa ni kosa,” alisema.
Kamanda Sabasc alitoa wito kwa maofisa kilimo kwenda katika vijiji hivyo, kutoa elimu ya kilimo cha mazao mbadala kwani kila mwaka mamia ya magunia ya bangi yamekuwa yakikamatwa.
Maeneo ya vijiji vya Kisimili juu na Olkokola katika kata za King’ori na Mukulati yamekuwa yakiongoza kwa kilimo cha bangi nchini ambapo nusu ya wakazi wakiwepo viongozi wa serikali za vijiji wanatajwa kuhusika na kilimo hicho haramu.MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment