-->

KINYANG'ANYIRO CHA NAFASI YA URAISI CCM CHAPAMBA MOTO,NI BAADA YA KUHUSISHWA KWA MIZENGO PINDA


LOWASSA.


UJIO wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umetibua mipango ya kada wenzake, Edward Lowassa na kubadili kabisa upepo wa kiasiasa, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.


Lowassa kwa muda mrefu sasa kambi yake ilimeonekana kujiimaisha zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, na hivyo kuwanyima usingizi makada wenzake walionesha nia, licha ya kwamba bado anatumikia kifungo cha mwaka mmoja baada ya chama kumtia hatiani kwa tuhuma za kuanza kampeni kabla ya wakati.

Kambi ya Lowassa inatajwa kuwa na mtandao mrefu hususani kwenye vikao vya juu vya uteuzi vya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC), lakini baada ya Pinda kuonesha nia ya kuutaka urais, inaelezwa kuwa ametokea mpasuko mkubwa.

Pinda inatajwa kuvuruga mipango ya ngome za Lowassa baada ya kutangaza nia akiwa mkoani Mwanza na kutamba kuungwa mkono na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa dini zote huku akiainisha watu watano ambayo alisema majina yao ndiyo yatakwenda NEC.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu ndani ya CCM, kambi hizo sasa zinatuhumiana kwa rushwa, ambapo kila moja inadai mwenzake anagawa fedha kwa wajumbe wa NEC na CC ili kujaribu kujenga mazingira ya ushawishi wa kuweza kupenya katika uteuzi.

Hatua hiyo, imesababisha vikao vya NEC vilivyomalizika mjini Dodoma juzi, kutawaliwa na tuhuma za rushwa kwa wajumbe wanaojiondoa kwenye makundi ya Lowassa na kwenda kwa Pinda.

Mazingira ya rushwa
Wapambe wa Pinda wanadai kuwa mtandao wa Lowassa unatembeza rushwa ya kati sh. 700,000 kwa wajumbe waliojiondoa huko na kuhamia ili kuwashawishi wasiondoke.

“Sasa hivi hawa jamaa wamejipanga, wamegawana majukumu ya kuwanunua wajumbe wa NEC kwa mtindo wa kanda ili kurahisisha azma ya kuwafikia wajumbe wengi,” kilieleza chanzo chetu.

Wafuasi wa makundi yote wapo mjini Dodoma wakati wote wa vikao vikuu vya CCM, ambapo kwa nyakati tofauti walionekana wakikutana na wajumbe hao wakijaribu kuwashawishi wawaunge mkono.

Nalo kundi la Lowassa linadai kuwa kambi ya Pinda ilifika mjini Dodoma Jumapili usiku wiki iliyopita na kuweka kambi katika vitoa viwili vya mjini na nje ya mji wakikutana na wajumbe wa NEC na kuwashawishi wamuunge mkono katika mbio za urais.

Chanzo hicho kinaongeza kuwa siku za Jumatatu na Jumatano zilikuwa za kukutana na makatibu wa CCM wilaya na ambapo kila mjumbe alitengewa sh.150,000 kama posho ya kikao.

Ndani ya NEC
Akiwasilisha taarifa ya maadili ndani ya kikao cha NEC, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philipo Mangula alisema kuwa licha ya kwamba wapo makada walipewa adhabu kwa kuanza kampeni za urais mapema bado kumezuka ATM mpya ambayo kwa sasa inaonekana kutoa fedha kwa kasi.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mangula alitaja maeno mawili ambayo alidai fedha hizo zinatolewa huku akijigamba kwamba wahusika wanawafahamu lakini akaonya kuwa hata kama hawatawapa adhabu leo, nyendo zao zinafuatiliwa.

Kwamba, mjumbe Christopher ole Sendeka, alisimama katika kikao hicho na kudai kuwa chama chao kinachafuliwa na ufisadi wa IPTL na fedha hizo zinatumika Dodoma kwenye kampeni za urais.

Madai ya Sendeka, yalizimwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, akisema kuwa la IPTL waliache kwanza maana wanasubiri ripoti ya uchunguzi, kwamba baada ya hapo watajua ni uamuzi gani ambao utachukuliwa.

Kamanda ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma, Emma Kuhanga, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa hajapata taarifa hizo za kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa wajumbe.

Emma, alisema hata hivyo kuwa taarifa inayohusiana na madai ya kuwapo kwa vitendo hivyo itafanyiwa kazi na ofisi yake.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chama hicho hakina taarifa za kuwapo kwa makundi ya makada wanaogawa rushwa, kwamba zikiwafikia watazifanyia kazi.

“Kama wanapeana rushwa usiku huko hotelini wakati wengine tumelala, hatuwezi kujua, lakini kama chama tutachukua hatua zinazostahili, tunaomba muendelee kutupatia taarifa mnazozipata,” alisema.

Mnyukano wa urais ndani ya CCM unaonekana kukiweka njia panda, kwani pamoja na kuwaadhibu makada sita kwa kuwafungia mwaka mmoja kutogombea uongozi wowote ndani ya chama, kutokana na kuanza kampeni mapema, baadhi yao wamekiuka adhabu hiyo na kuendelea kutangaza nia.

Waliofungiwa tangu Februari mwaka huu, ni Lowassa, Bernard Membe, Stephen Wassira, January Makamba, William Ngeleja na Fredrick Sumaye.

Wengine waliotangaza nia ya kutaka kiti hicho ni Dk. Hamis Kigwangalla na Mwigulu Nchemba ingawa pia wapo Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. John Magufuli na Dk. Asha-Rose Migiro ambao bado hawajatangaza rasmi.

Jaji Warioba kusulubiwa
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye pia ni kada mkongwe wa CCM, Jaji Joseph Warioba, amekalia kuti kavu ndani ya chama hicho.

Kuti kavu hilo litanatokana na umuazi wa NEC, iliyomaliza kikao chake juzi kuiagiza kamati ya maadili inayoongozwa na Philip Mangula, kumhoji kada huyo na wenzake kwa kwenda kinyume na taratibu na kanuni za chama.

Wajumbe wengine wanaunda kamani ya Maadili ni Dk. Maua Daftari, William Lukuvi, Abdulrahman Kinana, ambapo NEC vile vile iliamua makada wengine wa chama hicho akiwemo Joseph Butiku wahojiwe kwa tuhuma za kupingana na serikali na chama katika mchakato wa katiba mpya.

Warioba, Butiku na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wanadaiwa kuendesha mapambano ya kupinga katiba inayopendekezwa iliyotungwa na Bunge Maalum la Katika.

Makada hao wanadaiwa kuuhamasisha umma kuamini kuwa Bunge Maalum halikuwa na mamlaka ya kuondoa maoni yao yaliyokuwamo ndani ya rasimu ya katiba iliyotolewa na tume yao.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa katika kikao hicho cha NEC, Kilumbe Ng’enda na John Komba waliibua sakata hilo baada ya Mangula kuwasilisha mada kuhusu maadili na taratibu zinazotakiwa kufuatwa hasa katika chaguzi zijazo.

Katika kikao hicho, Ng’enda alilaumu chama kujenga madaraja ya kuwaadhibu, kuwaonya na kuwahoji makada wake wanaotuhumiwa kwenda kinyume na taratibu na kanuni za chama.

Ng’enda inadaiwa alisema anaamini anachokifanya Warioba na wenzake kingefanywa na mtu mwingine, CCM ingashachukua hatua muda mrefu.

Mjumbe huyo indaiwa alisema Warioba na wenzake inaonekana wanaogopwa ndiyo maana nao wanaendelea kukidhoofisha chama kwa matamko ya kupinga katiba inayopendekezwa itakayopigiwa kura mwaka 2016.

Naye Komba, inadaiwa kuwa alisema ni heri chama kikamuondoa Warioba kama hatoacha mashambulizi yake kuliko kuendelea kuwa naye.

Alisema Warioba amekuwa akijitapa mwanachama mwadilifu na hai wa CCM lakini matendo na kauli anazozitoa zinakwenda kinyume.

Mjumbe huyo alisema kama Warioba ataondoka hatokuwa wa kwanza na chama hakitakufa kwa kuwa walishafanya hivyo baadhi ya makada waliokuwa na nguvu zaidi na chama kilizidi kuimarika.

Tanzania Daima Jumapili, mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho lilimuuliza Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, kuhusu makada hao kupelekwa kwenye kamati ya maadili lakini hakuwa tayari kuweka wazi jambo hilo huku akisisitiza vikao vya chama hicho vilijadili mambo mengi ya msingi yanayogusa masilahi ya wananchi ikiwemo uchumi pamoja na chama kujitegemea.

“Hilo la watu kupelekwa kwenye kamati ya maadili Mwenyekiti wake ndiye atakayelizungumzia muda ukifika, lakini kimsingi tumejadili mambo mengi yenye masilahi kwa wananchi,”alisema.TANZANIA
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment