-->

TAARIFA YA SAMSON MWIGAMBA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU WARAKA WA MKAKATI WA MABADILIKO 2013

Jumatano, 27 Novemba 2013
Jana katika taarifa kwa waandishi wa habari, Mhe. Tundu Lissu na Mhe. John Mnyika waliudanganya umma kuhusu waraka unaohusu Mkakati wa Mabadiliko 2013. Katika maelezo yao waheshimiwa hawa, pamoja na mambo mengine, walidai kuwa waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni feki. Ukweli ni kwamba:


  1. Ninathibitisha kwamba waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ni sahihi neno kwa neno kama nilivyousoma katika magazeti ya HabariLeo, Jamhuri na Rai, pamoja na nakala iliyopo Jamii Forum. Ili kuthibitisha kwamba waraka ule ndio wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta mpakato (laptop) yangu ambako ndiko ulikoibwa na viongozi wa chama baada ya kunipora kwa nguvu laptop yangu Oktoba 25 na kukaa nayo hadi jioni ya Oktoba 28. Naomba kila mtu asome neno kwa neno waraka ninaowapa leo halafu afananishe na ule uliopo kwenye magazeti na kwenye mtandao ili mjiridhishe kama kweli sio wenyewe. Kama Lissu na wenzake wana mpango wa kuuchakachua waraka huu wamekwama!
  2. Waraka huu si wa uhaini wala mapinduzi wala usaliti kama inavyodaiwa na akina Lissu. Huu ni waraka wa kusaka ushindi katika uchaguzi halali ndani ya chama ambao ulikuwa ufanyike Desemba 2013, na ambao sasa umesogezwa mbele.
  3. Napenda ijulikane kwamba wakati wa uchaguzi si jambo la ajabu kuwa kwa wanachama kuwaunga mkono wagombea tofauti. Nimekuwa karibu na Mwenyekiti Mbowe kwa miaka mingi na ninajua kwamba yeye naye anao mkakati tena unaohusisha mbinu haramu za kuhakikisha anammaliza Zitto na yeye kupita bila kupingwa kwenye uchaguzi huo. Wanaoshiriki mkakati wake ni pamoja na Lema, Lissu na wakurugenzi kadhaa waliopo makao makuu.
  4. Waraka huu ulipaswa kuwa siri ndani ya watu watatu tu (M1, M2 na M3) na haikutarajiwa kwamba ungevuja kwa jamii. Bahati mbaya viongozi wa chama baada ya kuunasa waraka huu kutoka kwenye komputa yangu mpakato (laptop), na baada ya kikao cha Kamati Kuu, waliamua, kwa jazba na bila kutumia busara ya kiuongozi, kuusambaza waraka huo kwenye vyombo vya habari kwa lengo la kuwakomoa na kuwadhalilisha waandaji. Sasa baaada ya kugundua madhara ya waraka huo machoni pa jamii wameamua kuukana. Ni ajabu kwamba wanaukana waraka ambao waliusambaza wenyewe.
  5. Nasisitiza kwamba mambo yaliyopo kwenye waraka ni bayana na dhahiri. Sibahatishi kwa sababu mimi nimefanya kazi makao makuu kama Mhasibu Mkuu hadi Mwezi Aprili 2012. Ni kwa kutambua uozo uliopo katika uongozi wa chama makao makuu niliona umuhimu wa kubadilisha uongozi kwa njia za kidemokrasia ili tukiokoe chama na hatukuwa na nia wala sababu za kuanika haya yote kwenye umma. Kwa sababu za chuki na kukosa busara za kiuongozi huyo anayeitwa Mwanasheria Mkuu akawashauri viongozi wetu kijinga wauanike waraka mbele ya macho ya watanzania. Wangekuwa na akili na busara baada ya yote haya kutokea wangejiuzulu au kuitisha uchaguzi mara moja.
  6. Tunatambua kwamba viongozi wetu wanamchukia Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa siku nyingi sana na wametamani kumfukuza siku nyingi. Hata hivyo, ninawashauri watafute sababu nzuri za kumfukuza uongozi na hata uanachama kwa sababu yeye hahusiki na waraka wetu wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 hata chembe, pamoja na kwamba yeye ndiye alikuwa na bado ndiye mlengwa mkuu, kama atakubali.



Samson Mwigamba (M3)
Arusha
Jumatano, 27 Novemba 2013.
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment