Polisi
wakishusha mwili wa marehemu mmoja na watu watatu waliofariki dunia
katika mapigano ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa, Morogoro juzi.
Picha na Juma Mtanda
Na Juma Mtanda, Mwananchi.
Mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi
kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro, yanazidi kutikisa baada
ya watu wengine watatu kuuawa kwenye Kijiji cha Mbiligi, Kata ya Magole
wilayani Kilosa.
Tukio hilo,
ambalo limetokea mwezi mmoja tu baada ya mkulima mmoja kuuawa kwenye
Bonde la Mgongola wilayani humo, ni kati ya matukio mengi ya mapigano
baina ya jamii hizo mbili na ambayo yalijadiliwa kwa kina kwenye mkutano
uliopita wa Bunge la Muungano.
Habari kutoka eneo la tukio
zinaeleza kuwa, juzi saa 2.00 asubuhi wakulima wapatao 15 walikwenda
eneo la Matembele na Ming’oni, jirani na Kijiji cha Mbigili ili kupanda
mpunga, lakini saa nne baadaye vijana wawili wa Kimasai walifika na
kuhoji sababu za kutumia eneo hilo kwa kilimo wakati ni mali ya Kijiji
cha Mabwegela na kuwaamuru waondoke.
Lakini wakulima hao walikaidi na ndipo muda mfupi baadaye likaibuka kundi la wafugaji wapatao 50 na kurejea swali hilo.
Habari
hizo zilisema kuwa, baada ya wakulima kuona wamevamiwa, walianza
kuwarushia Wamasai mapande ya udongo na walipozidiwa ndipo waliporudi
nyuma, lakini ghafla wakajikuta wamezingirwa.
Kwa mujibu wa
habari hizo, wakulima waliamua kutoroka, ndipo baadhi yao
waliposhambuliwa kwa mikuki, virungu, mishale na visu na kusababisha
vifo vya watu hao watatu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias
Tarimo alisema watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wamelazwa katika
Kituo cha Afya cha St Joseph cha Dumila, Kilosa.
Alisema
waliouawa ni Joseph Lawama, ambaye ni mkulima wa Mbigili (26), Rajabu
Kigongo, mkulima wa Mbigili ambaye alichomwa mshale mgongoni na kuchanwa
na shingoni na Kandura Kashu (30) mfugaji wa Mabwegere.
Alisema
mtu mmoja alifariki dunia katika maeneo ya tukio na wengine wawili
wakati wakitibiwa katika kituo cha afya. Pia aliwataja majeruhi kuwa ni
Binzi Dotto (42), Juma Someke (35) na Mohamed Selemani (36).
“Mgogoro
huu unatunyima usingizi viongozi katika jitihada zetu za kuutatua na
kuepusha umwagaji damu. Tumekuwa tukijitahidi kuitisha vikao vya
upatanishi kati ya vijiji vya Mbiligili na Mabwegere, lakini hakujawa na
mafanikio,” alisema Tarimo.
Alisema tatizo hilo linatokana na baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Mabwegere kukataa kuhudhuria vikao vya upatanishi.
Muuguzi
wa zamu katika Kituo cha Afya cha St Joseph, Melania Shayo alisema
walianza kuwapokea majeruhi saa 10.30 jioni na kwamba wakati
wakiwahudumia, wawili walifariki dunia.
Shayo alisema watu
hao ni Joseph Lawaza na Rajabu Kigongo ambaye alipoteza maisha saa 4.28
usiku wakati akifanyiwa mpango wa kusafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
“Awali tuliwapokea
majeruhi saba na maiti moja, lakini baadaye vifo viliongezeka baada ya
majeruhi wawili kufariki dunia hapahapa hospitalini wakati wakipatiwa
huduma,” alisema Shayo.
Shayo alisema vurugu nusura zitokee
kwenye kituo hicho baada ya wananchi kupata taarifa kuwa kulikuwa na mtu
mmoja kutoka jamii ya Wamasai aliyefikishwa akiwa majeruhi na hivyo
kutaka kuvamia ili wammalizie, lakini polisi walidhibiti hali hiyo.
Mmoja
wa majeruhi, Mohammed Athuman alisema vurugu kati yao na wafugaji
zilianza saa 6.00 mchana wakati wakipanda mpunga shambani.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Marambo alisema hadi sasa
hakuna mtu aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.MWANANCHI
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment