PROFESA AUAWA KWA KUCHINJWA NA KUWEKWA KWENYE FRIJI
Matukio ya ukatili wa kutisha yanazidi kushika kasi kila kona ya nchi, safari hii hofu imetanda kwa baadhi ya wakazi wa Dar es salaam ambapo Profesa maarufu aliyefahamika kwa jina la Joseph Minja, mkazi wa Makonde eneo la Mbezi-Beach anadaiwa kuuawa kwa kuchinjwa kinyama kisha mwili wake kukutwa kwenye friji.
Profesa maarufu anayefahamika kwa jina la Joseph Minja, mkazi wa Makonde eneo la Mbezi-Beach anadaiwa kuuawa kwa kuchinjwa.
Tukio hilo la kutisha lilijiri Februari 3, mwaka huu nyumbani kwake maeneo hayo alikokuwa akiishi na wafanyakazi wake ambapo watekelezaji wa mauaji hayo walitimkia kusikojulikana.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, kutokana na kutapaka kwa damu katika nyumba hiyo, kulionesha ni jinsi gani Profesa Minja alivyokuwa akijitetea kunusuru roho yake.
CHANZO KINAFAFANUA
Kwa mujibu wa majirani wa eneo hilo ambao hawakutaka majina yao yawekwe kwenye gazeti, kitendo hicho ni cha kikatili na kuliomba jeshi la polisi kuwasaka wauaji popote walipo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Chumba cha mauaji.
Mmoja wa majirani hao ambaye amepanga karibu na kwa marehemu aliliambia gazeti hili kuwa alishangaa kuona kuku na nguruwe wakipiga kelele huku nyumba ikiwa na giza ndipo mauaji hayo yalipogunduliwa na majirani.
“Ilikuwa majira ya usiku wa kuelekea saa 3:00, nyumba hiyo ilikuwa na watu watatu, mmoja ni mmiliki wa nyumba na Baa inayofahamika kwa jina la Kunontze Center ni Profesa Minja.
“Pia kulikuwa na huduma nyingine za mitandao ya simu na walikuwa wakiuza ving’amuzi.
“Lakini katika hali ya sintofahamu, wafanyakazi wa Baa hiyo walitokomea kusikojulikana baada ya tukio hilo na kuweka kitendawili kisichokuwa na majibu.
“Polisi walipofika eneo la tukio waliukuta mwili wa marehemu ukiwa ndani ya friji huku damu zikiwa zimetapakaa.
“Usoni na mikononi alikutwa amekatwakatwa na kitu chenye ncha kali,” alisimulia shuhuda.
Baada ya kuchinjwa kinyama kisha mwili wake kukutwa kwenye friji hili.
MJOMBA, MTOTO WANASIMULIA
Mjomba wa marehemu, William Mambali alilisimulia gazeti hili kwamba, alipokea simu saa 6:30 usiku kutoka kwa mmoja wa majirani hao akimtaarifu kuhusiana na tukio hilo la kinyama.
Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo mbaya masikioni mwake, naye alianza kuwataarifu ndugu mbalimbali ambapo asubuhi na mapema walifika nyumbani hapo na kushuhudia damu zikiwa zimetapakaa chapachapa huku mwili ukiwa tayari umeshachukuliwa na polisi na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu wa Kinondoni ya Mwananyamala, Dar.
“Huu ni zaidi ya unyama, hata kama angekuwa kakosea jambo gani, hakustahili kuchinjwa na kuwekwa kwenye friji tena ndani yake kukiwa na kuku.
“Damu ya mtu haiendi bure, lazima wahusika watakamatwa tu.
“Tunafanya taratibu za mazishi. Mazishi yatafanyika kijijini kwao, Lysongo-Marangu mkoani Kilimanjaro baada ya kukutana kwa wanandugu na kukamilisha mambo mengine,” alisema mjomba kwa uchungu.
Kwa upande wake, mtoto wa kwanza wa marehemu, Jane alisema anamwachia Mungu kwani ndiye atakayefichua wabaya wote waliohusika.
Marehemu ameacha watoto saba na hadi umauti unamfika alikuwa akifundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitengo cha Computing Center (UCC).
Hata hivyo, tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kawe na kupewa jalada la kesi namba KW/RB/1162/2015 -MAUJI ambapo polisi wanaendelea na uchunguzi.
Binti wa marehemu akiwa na polisi.
WASIFU WA MAREHEMU
Profesa Minja alikuwa mwanaharakati na mwanzilishi wa siasa za vyama vingi nchini. Aliwahi kuingia kwenye harakati za kugombea nafasi ya ubunge kupitia kwenye Jimbo la Kawe kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi mwaka 1995. Baadaye alianzisha na kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Peoples Democratic Movement (PDM).
Ni Mtaalam Mstaafu wa Kimataifa wa Ndege aliyewahi kuwa Mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi Mawasiliano ya Anga. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen.
SOURCE:TZNEXT
0 comments :
Post a Comment