Ndugu zangu,
Si wengi
wenye kufahamu, kuwa Yoweri Museveni alianza masomo yake ya Chuo Kikuu,
Dar es Salaam, mwaka 1967. Kijana Museveni alitoka Uganda kuja Dar es
Salaam kwa garimoshi ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya Uganda.
Kwenye
kitabu chake, ' Sowing The Mustard Seed', Museveni anasimulia, kuwa pale
Railway Station , Dar es Salaam, alipokewa na Mganda mwenzake Martin
Mwesigwa aliyemwonyesha njia ya kufika Ubungo na Chuo Kikuu.
Uhanarakati
wa Museveni ulianza kujitokeza hapo Mlimani. Akiwa hapo, Museveni na
baadhi ya wanafunzi wenzake walianzisha jumuiya ya USARF- University
Student's African Revolutionary Front. Uanachama wake ulikuwa ni wa
PanAfricanism. Kulikuwamo na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.
Alikuwamo pia marehemu Andrew Shija.
Museveni
akiwa Mlimani, alipangiwa kuishi hall lililoitwa ' Biafra'. Maana,
lilijitenga kidogo na mengine. Na wakati huo ndio kulikuwa na vuguvugu
la Biafra kujitenga kutoka Serikali ya Shirikisho, Nigeria, na Julius
Nyerere, alianza kwa kuitambua Biafra kabla ya kubadili mtazamo baadae.
Pale
Mlimani Museveni alisoma Political Science. Uhanarakati wa Museveni
unathibitishwa pia na ndugu yangu BAP-' Born Again Pagan'. Hili si jina
lake halisi. Huyu ni mmoja wa ' wanakijiji wa Mjengwablog' wa miaka
mingi. Naye alisoma Chuo Kikuu enzi hizo. Anamkumbuka Yoweri Museveni
aliyekuwa mbele yake mwaka mmoja. Kuwa alikuwa ni mtu mwenye msimamo, na
kuwa , alikuwa akiingia kwenye lectures za wahadhiri aliowakubali tu
kimisimamo.(P.T)
Kwenye '
Sowing The Mustard Seed', Museveni anaelezea jinsi jumuiya yao ya USARF,
ambaye yeye ndiye alikuwa Rais wake, ilivyojipambanua kwenye masuala
yenye kuhusiana na itikadi na mapambano ya ukombozi. Waliunda kikundi
chao wenyewe cha kujisomea na kujadiliana. USARF ilikuwa na akina Eriya
Katageya, James Waphakhabulo, Andrew Shija na hata John Garang,
aliyekuja kuwa kiongozi wa SPLM ya Sudan.
Waliawaalika
pia baadhi ya wahadhiri kujadiliana nao. Walter Rodney, alikuwa mmoja
wa wahadhiri hao. Wakati huo, Walter Rodney, mwandishi wa kitabu cha '
How Europe Underdeveloped Africa' alikuwa kwenye harakati ya kukusanya
materials za kitabu chake.
Kikundi
cha USARF kilifikia hata kuwaalika wageni mbali mbali waliopita hapo
chuoni kwa mijadala. Ikiwamo viongozi wa mataifa ya nje.
USARF ya
Museveni na wenzake ilifika mahali wakawashambulia hata vijana wa TANU,
tawi la Chuo Kikuu kwa kuacha harakati za kiuanafunzi na badala yake
kujipendekeza kwa viongozi wa TANU mjini, ili waje wapewe vyeo baadae.
Jambo
hilo lilifanya USARF na akina Museveni watengenezewe ' zengwe' ama
fitina kutoka viongozi wa TANU- Youth League Mlimani kwenda kwa viongozi
wa TANU Lumumba. Kosa la USARF? Kwamba wanaeneza kampeni dhidi ya sera
za TANU.
Na TANU Youth League wakaenda mbali zaidi, wakawachongea USARF na akina Museveni kwa Julius Nyerere mwenyewe.
Kikatoka
kivumbi. Nyerere akaamua ashuke mwenyewe Mlimani kukutana na hao
wanaojiita USARF. Museveni akawapanga watu wake, na akawa tayari
kuongoza mapambano. Nini kilitokea kwenye mpambano wa hoja kati ya
Nyerere na Museveni pale Mlimani?
Tukutane kesho, panapo majaliwa.
Maggid,
Iringa.
Iringa.
0 comments :
Post a Comment