WINGA wa Yanga, Mrisho Ngassa, amekiri kwamba akiwa mikononi mwa Simba na Azam, klabu hizo zilitaka kumpa dili la maana lakini Yanga wakaingilia kati na kufanikiwa kutibua kwa matajiri wao kumpenyezea fungu ili atue Jangwani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngassa alisema kuwa anajuta kwanini alizikatalia klabu hizo zilizokuwa na malengo mazuri ya kumuuza kwenye klabu ya El Merreikh ya Sudan na badala yake akang’ang’ania kubaki Tanzania kisa ikiwa ni mapenzi yake kwa Yanga ambayo yamemnyima fursa kwenye maisha yake ya soka.
Ngassa alisema: “Nimekuwa nikikataa dili nyingi ninazopata kwa sababu ya mapenzi yangu kwa Yanga. Nakumbuka nilikuwa niende El Mereikh ya Sudan lakini nilikataa ili nibaki Yanga.
“Leo hii ninajuta, nakumbuka nafasi hiyo niliyoipata kupitia Simba na Azam ilikuwa ndiyo bahati yangu ya kutoka kisoka.
“Mapenzi yangu kwa Yanga yaliniponza na hivi sasa ninajuta kwani leo hii pengine ningekuwa mbali na ningekuwa nimepata mafanikio makubwa zaidi ya haya niliyoyapata Yanga.
“Sina wa kumlaumu kwani uamuzi wangu ndiyo wa kuujutia kwani nilipata ushauri kutoka kwa watu wengi wa karibu lakini nikapuuza wakati ningeikubalia Azam ningeweza kupata fedha nzuri ya usajili pamoja na kuichezea klabu hiyo huku nikiangalia sehemu nyingine ya kucheza soka nje ya Bara la Afrika.
“Hivi sasa nimebakiza mkataba wa miezi mitano na Yanga na sijajua iwapo nitaongeza mkataba au nitatimka zangu kwenda kutafuta klabu nyingine ya kucheza.”
Azam ambao walimpeleka kwa mkopo mchezaji huyo Simba, kwa pamoja walitaka kumuuza Ngassa, El Mereikh kwa dau la dola 100,000 (sawa na Sh 179 milioni) ambapo kwenye dau hilo Ngassa alikuwa apewe Dola 50,000 sawa na Sh 89.5 milioni) kama fedha ya usajili wa mkataba wa miaka miwili wakati Simba na Azam zingegawana Dola 50,000.
0 comments :
Post a Comment