-->

SIKU WANANCHI WAKICHOKA NA KIPIGO CHA ASKARI

Julius S. Mtatiro's photo.SIKU WANANCHI WAKICHOKA KIPIGO CHA ASKARI (1)?
Na. Julius Mtatiro,
Gazeti la Mwananchi - Jpili, 01 Februari 2015.
Matukio ya vyombo vya ulinzi na usalama kunyanyasa raia yamekithiri nchini kwetu. Raia wamekuwa wakinyanyaswa, wakiteswa, wakitishwa, wakiumizwa na mara nyingi tu kupoteza maisha kutokana na kipigo kutoka kwa vyombo vya dola au hata kupata ulemavu wa kudumu katika miili au akili kwa sababu ya kujeruhiwa vibaya na askari wetu.
Lengo la makala hii ni kuangazia tatizo hili linaloendelea kukua na kushauri hatua za kuchukua. Ni kweli kabisa kuwa nchi yoyote inakuwa na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kulinda mipaka ya nchi na hata hali ya amani ndani ya nchi yenyewe. Askari hawa huwa katika makundi tofauti na kazi tofauti kila mara.
Kwa mfano, askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) huwa na jukumu la kulinda mipaka ya nchi. Majeshi mengine kama vile Polisi, Magereza, JKT n.k huwa na kazi maalum ya kulinda amani ndani ya nchi. Wanajeshi mara zote hufunzwa mafunzo muhimu na hukanywa dhidi ya matumizi ya nguvu huku wakijulishwa kuwa siri ya mafanikio ya askari ni kuwa karibu na wananchi wa kawaida.
Kwa mfano, Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania yalipoingia Uganda kumfukuza Idd Amin Dada yalipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa kawaida ya yalifurahiwa sana na hivyo yalipewa kila taarifa muhimu za kupambana na adui. Askari wa jeshi lolote lile wanapokuwa hawana maelewano na raia huangukia mikononi mwa maadui kirahisi.
Kwa hiyo, majeshi yote duniani hivi sasa yanajenga mikakati na maboresho makubwa ya kuwa “rafiki wa raia” na yanafanya kila yawezalo ili kukubalika kwa raia kwa lengo la kurahisishiwa kazi ngumu ya kulinda na kufuatilia masuala ya usalama.
Vyombo vyetu vya dola vimekuwa mstari wa mbele kunyanyasa na kuonea raia, kuwapiga, kuwadhalilisha na kutweza utu wao, kuna matukio kadhaa yanathibitisha hali hii:
VURUGU ZA GESI MTWARA.
Mwezi Januari hadi Mei mwaka 2013 kulikuwa na sintofahamu mkoani Mtwara. Wananchi waliandamana wakitaka majibu kutoka kwa mamlaka husika juu ya masuala ya gesi inayochimbwa mkoani humo. Wananchi waliona kuwa, ahadi zote zilizotolewa na serikali hazijatekelezwa na badala yake serikali imeanzisha mpango wa kusafirisha gesi kupeleka Dar Es Saalam bila kuwajulisha wananchi uamuzi huo na una faida na hasara gani kwao.
Maandamano yale yalipoanza serikali ilituma askari jeshi wakatulize raia bila kuwekeza nguvu kwenye majadiliano na hatua za kistaarabu. Tulichokishuhudia Mtwara baada ya hapo ni wananchi kuchukuliwa kwa nguvu, kupelekwa kwenye kambi ya jeshi na kuteswa siku nzima, wiki nzima n.k. Ungeliwashuhudia wananchi waliopata mateso yale ungeliumia sana.
Sekeseke la gesi liliisha huku kuna raia wakiwa na vilema vya kudumu, watu karibia dazani moja kufariki na miundombinu mbalimbali kuharibiwa. Wananchi mara zote hupenda maswali yao yajibiwe kwa wakati hasa kama yanahusu jambo lenye maslahi, na serikali kwa kawaida huwa haitaki kutoa majibu hayo kwa wakati kuogopa kujichanganya kwa sababu haifanyi kazi kama timu.
Wananchi wanaponyimwa majibu huanza viashiria vya kuchukua hatua mkononi, na hata serikali za mikoa na serikali kuu zinapoona viashiria hivyo, mara zote hazichukui hatua ya kupeleka ujumbe mzito wa viongozi ili wakae na viongozi wa wananchi na hata wananchi wenyewe ilimradi jambo lifafanuliwe na makubaliano ya msingi yafanyike, la! Mara zote serikali ikiona viashiria tu vya wananchi kudai jambo lao tena kwa maandamano ya amani kinachofuatia ni kutuma jeshi ili wananchi wapigwe na kukamatwa, wateswe na wakomeshwe.
Njia hii ya serikali nyingi za kiafrika na hususani Tanzania ni “njia ya kipofu”, maana haisaidii kitu, inawafanya wananchi wawe sugu, wazoee kupigwa, wajenge uadui na serikali na vyombo vyake, wasiwe wazalendo na waaminifu kwa taifa lao na inawafanya wananchi waone kama viongozi ni madikteta wasio na huruma hata kidogo.
Wananchi wakijenga imani hii dhidi ya serikali na vyombo vyake na kisha ikaachwa iendelee kukomaa, tunajiandalia bomu zito siku za usoni ambalo likilipuka hakuna atakayejiokoa. Nasema hivi kwa sababu ni hatari sana kuwazoesha wananchi “usugu”, kuzoea mateso na kuonewa, kuichukia serikali na vyombo vyake n.k. maana wananchi ni wengi mno kila mahali na siku wakichoka hali hii ya kuonewa na kutwezwa, sote hatutakuwa salama.
KUUAWA KWA DAUDI MWANGOSI - IRINGA
Tabia ya vyombo vya dola kutumia nguvu bila sababu katika mambo ambayo yanahitaji busara na mazungumzo ya kawaida ilikuwa sababu kubwa ambayo baadaye ilipelekea matumizi makubwa ya nguvu na kuuawa kwa Mwangosi.
Daudi Mwangosi aliuawa mwezi Septemba mwaka 2012 akiwa katika majukumu yake ya uandishi wa habari. Eneo alilouawa huko mkoani Iringa lilikuwa na shughuli za kisiasa za CHADEMA. Pamoja na Mkuu wa Polisi wa Wilaya kuruhusu shughuli za CHADEMA ambazo zilikuwa ni pamoja na ufunguzi wa matawi, Mkuu wa Polisi wa Mkoa alizuia shughuli hizo zisiendelee (jambo ambalo ni kinyume na sheria na ni nje ya mipaka ya kazi yake “ultra vires”).
Wakati viongozi na wananchama wa CHADEMA wanatembelea vijiwe na ofisi kadhaa kufungua matawi yao, Polisi kwa maagizo ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa waliamua kutumia nguvu kuwatawanya na kuwakamata wananchi waliohusika katika tukio lile. Hapa ndipo Mwangosi alipolipuliwa na bomu ambalo mpaka leo halijulikani ni la aina gani.
Mwili wa mwandishi huyu kijana ulisambaratika vipandevipande, baada ya hapo serikali ilianza kutoa taarifa za kila namna za kujitetea na kuwasukumia waandamanaji makosa. Kuna wakati serikali ilidai haijui bomu lile lilitoka wapi, mara ikasema lilirushwa na CHADEMA na mwisho wa siku ikakiri kuwa lilimponyoka askari mmoja.
Tukio la Daudi Mwangosi liliacha simanzi kuu miongoni mwa raia wa Tanzania. Kila mtu alijiuliza matumizi ya nguvu ya namna hii yalikuwa ya nini? Yalikuwa na faida gani? Kwa nini nguvu itumike kuwashughulikia watu ambao kwa mujibu wa sheria walilijulisha jeshi la polisi juu ya shughuli zao? Je, shughuli za CHADEMA zilizuiliwa ghafla na RPC kwa sababu gani na kwa nini OCD aliziruhusu kabla ya hapo?
Jambo la kusikitisha ni kuwa, kamanda wa polisi wa mkoa ambaye alichukua madaraka nje ya mamlaka yake na kuingilia mkutano wa CHADEMA na kusababisha mauaji hayo, hakufukuzwa kazi wala kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu hata baada ya ripoti mbalimbali kuonesha kuwa alikuwa chanzo cha mauaji yale na hadi sasa serikali inamlinda kwa udi na uvumba. Wananchi wanayajua haya na yanawaumiza sana.
KUUAWA KWA WANANCHI NYAMONGO – TARIME
Mgodi wa dhahabu wa Nyamongo umekuwa ni uthibitisho mwingine wa matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya Raia. Tatizo la Nyamongo linajulikana tangu zamani, awali huu ulikuwa ni mgodi wa wachimbaji wadogowadogo, baadaye serikali iliamua kuuchukua ili kuwakabidhi wachimbaji wakubwa. Uchukuaji huo ulifanyika kiholela na ni kama wananchi waliporwa mgodi wao, baadhi yao walifidiwa kidogo na wengine hawajafidiwa hadi leo na huku maeneo yao yalichukuliwa.
Baada ya utaifishaji huo, serikali haikuweka kinga yoyote ya kiuchumi kwa wananchi. Serikali ilifikiria kuwapa wawekezaji wa kigeni maeneo yote ya mgodi bila kufikiri kuwa wachimbaji wadogo ni lazima watengewe maeneo yao ili na wao waendelee na uchimbaji. Serikali haikufanya hivyo na haitaki, mwisho wa siku wananchi wanachoshwa na wanaamua kufanya maandamano kwenda mgodini na serikali hutafsiri kitendo hicho kama “uvamizi wa mgodi” na wananchi hao huishia kupigwa risasi na polisi na kuuawa, serikali haioni shida jambo hili likitokea tena na tena.
Mauaji ya wananchi Nyamongo ni tatizo kubwa sana na yanaendelea kila uchwao na hakuna hatua thabiti ambazo zimechukuliwa kuzuia mauaji haya na machafuko siku za usoni. Kila mara mauaji yakitokea, utasikia serikali inasema “wananchi walivamia mgodi na kutaka kupora dhahabu hivyo polisi wamewapiga risasi na kuwaua”. Je ni serikali gani inayofurahia wananchi wake waendelee kuuawa kwa sababu wamevamia mgodi? Kwa nini wanavamia mgodi huo?
Je, serikali bado inashindwa kufanya uamuzi wa kuwapa maeneo maalumu waendeleze uchimbaji? Ama serikali inataka wananchi hawa wakafanye kazi gani wakati kazi waliyoizoea tangu wamezaliwa ilikuwa ni kuchimba dhahabu. Kwa nini pia migodi hii isiwaajili wananchi hawa wenye uzoefu ili watoe mchango wao? Tunadhani suluhisho ni kuwapiga risasi tu? Na tutawapiga risasi hadi lini ikiwa hatutaki kutatua mgogoro uliopo?
Tutaendelea na sehemu ya pili ya makala hii.
(Mwandishi ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi wa kisiasa ndani ya Tanzania. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment