Rais wa chama cha walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu msimamo wa chama hicho kuunga mkono na kushiriki mgomo uliotishwa na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania(TUCTA, baada ya serikli kushindwa kuteleleza madai ya wafanyakazi.Picha na Michael Jamson Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametangaza Aprili 30 kuwa ni siku ya kupiga Kura ya Maoni, lakini Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinataka kuitumia kwa malengo tofauti; imepanga kuanza mgomo nchi nzima wa kudai stahiki zao. Chama hicho, ambacho kinaongoza walimu shule za msingiu na sekondari wapatao 206,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2010, kimeeleza kuwa iwapo Serikali itakuwa haijatekeleza maazimio yao matano ifikapo tarehe hiyo, walimu watachukua uamuzi mgumu kama ule wa mwaka 2012.
Uamuzi huo uliofikiwa kwenye mkutano wa Baraza la CWT uliomalizika Morogoro wiki mbili zilizopita, umekuja katika kipindi ambacho wadau wengi wana shaka na utayari wa Serikali kufanikisha mchakato wa Kura ya Maoni kutokana na viashiria vingi vya vikwazo, hasa muda wa kutosha kutekeleza masuala yote yanayohitajika kama Sheria ya Kura ya Maoni inavyotaka.
Ingawa Tume ya Uchaguzi (Nec) imeeleza kuwa mambo yote yako sawa kufanikisha Kura ya Maoni, zikiwamo fedha za kuendeshea mchakato huo, tamko hilo la CWT linaonekana litakuwa kizingiti kingine kikubwa kwa Serikali, hasa kutokana na ukweli kuwa walimu ndio hutumika sana kwenye shughuli za upigaji kura.
Akizungumza na gazeti hili jana, rais wa CWT, Gratian Mukoba alitaja maazimio hayo kuwa ni kuitaka Serikali kulipa Sh16 bilioni ambazo ni madeni ya walimu, kupandisha walimu wanaostahili, kulipwa mishahara waliokuwa wanadai tangu mwaka 2012, mwalimu kuwa na mwajiri mmoja kati ya Wizara ya Elimu na Tamisemi na kubadilishwa kwa kanuni za viinua mgongo kwa wastaafu. “Yote haya yanatakiwa kutekelezwa ifikapo Aprili 30 mwaka huu la sivyo Baraza litawataka walimu kuchukua uamuzi mgumu. Fedha za kumlipa mwalimu zipo, lakini wanaozifaidi ni wachache,” alisema Mukoba, ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta).
“Ukisikiliza mijadala bungeni ni wizi na ufisadi. Mara mishahara hewa... mara (sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta) Escrow, lakini walimu hawalipwi wala kutatuliwa matatizo yao. Hii ni kwa sababu Serikali iliyopo imeshindwa na umefika wakati sasa kuiondoa madarakani.”
Mwaka 2012 CWT ilitikisa nchi baada ya kufanya mgomo nchi nzima ulioungwa mkono na walimu wa shule za msingi, sekondari na vyuo na ambao ulisambaa hadi kwa wanafunzi walioamua kuandamana ili kuishinikiza Serikali kuwalipa walimu wao.
Mwaka huo, Julai 27 CWT iliandika notisi ya saa 48 kuhusu mgomo huo, lakini Serikali ikautangaza kuwa si halali kwa maelezo kuwa unakiuka taratibu za kimahakama baada ya pande hizo mbili kufikishana Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi kujaribu kutatua tatizo hilo.
Jana, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa alisema hawajayapokea maazimio hayo.
“Wao wamefikia maazimio hayo, lakini sisi bado hatujayapata na kama tukiyapata tutawaita na tutazungumza nao,” alisema Waziri Majaliwa
“Mfano suala la madeni wao watakuwa wamelizungumza kwa ujumla hivyo tukikutana tutaweza kuwaeleza tumefikia wapi katika utekelezaji wa kila eneo.”
Lakini Mukoba alipofuatwa kuzungumzia kauli hiyo ya Waziri Majaliwa, alisema: “Kama anasema hawajayapata, basi wasubiri Aprili 30 kuyapata. Serikali ina ubabaishaji na kama ndiyo hivyo mwambie asubiri Aprili 30 atayapata maazimio hayo.”
Aliongeza kusema:”Kama anasema hawajui mbona watumishi kutoka Tamisemi walikuwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wanafuatilia madeni ya walimu kama hawajui wanachokifuatilia huko ni nini, wasubiri wataona?”
Nec ilikuwa imependekeza kutumia wanajeshi katika mchakato wa Kura ya Maoni, lakini pendekezo hilo limepingwa na wadau, hasa wanasiasa na wanaharaka ambao wamesema matumizi ya chombo hicho cha dola yatatisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura na pia siku ya kuhitimisha mchakato huo ambayo ni Aprili 30.
Kwa hali hiyo, Nec italazimika kutumia walimu kwenye mchakato huo mkubwa na unaohitaji nguvu kazi kubwa hasa wakati wa upigaji kura.
Tayari vyama vya upinzani vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimetangaza kujitoa kwenye mchakato huo wa Kura ya Maoni, ambao utahusisha uandikishaji wa wananchi kwenye Daftari la Wapigakura, utoaji wa elimu kuhusu yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa, upigaji wa kampeni za kutaka wananchi waikubali au waikatae na kuhitimishwa kwa kupiga kura.
Mchakato wa Kura ya Maoni imekuwa na vikwazo vingi tangu wakati wa Bunge Maalum la Katiba wakati vyama vya upinzani vilipodai kuwa chombo hicho kilikuwa kinapoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na badala yake kujadili rasimu iliyokuwa na utashi wa CCM.
Baadaye vyama hivyo vikaunda Ukawa na mwezi Aprili vikasusia vikao vya Bunge la Katiba, na juhudi za kuwarejesha bungeni zilkishindikana.MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment