Nelson Rolihlahla
Mandela ni Rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini ya kidemokrasia. Ni mtu
aliyejijengea heshima kubwa duniani kutokana na jitihada zake kubwa
zilizofanikisha uhuru
wa nchi hiyo na nyinginezo katika Bara la Afrika.
Mzee Mandela
anayefahamika pia kwa jina la Mzee Madiba amelazwa hospitalini mjini Pretoria,
Afrika Kusini kwa zaidi ya mwezi sasa akiwa mahututi. Anasumbuliwa na ugonjwa
wa mapafu.
Kutokana na umaarufu
wa Rais huyo mstaafu wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 95, JAMHURI tumeona
vema kuchapisha historia fupi ya maisha yake kama ifuatavyo:
Nelson Mandela ni
mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati aliyepambana na sera za ubaguzi za makaburu
wa Afrika Kusini na hatimaye kuwa Rais wa kwanza Mwafrika nchini humo. Ni
mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel. Pia amepata kutunukiwa zaidi ya tuzo 250
katika miongo minne iliyopita.
Ni rais wa kwanza
aliyechaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini. Alikuwa mwanasheria na
mwanachama wa Chama cha African National Congress (ANC) aliyepinga utawala wa
ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
Nelson Mandela
alizaliwa Julai 18, 1918. Baba yake mzazi alifariki wakati Mandela akiwa na
umri wa miaka tisa. Tangu kipindi hicho alilelewa na Jonintaba hadi
alipoitoroka familia hiyo baada ya kutakiwa aoe mwanamke aliyepangiwa.
Mwaka 1943 Mandela
alijiunga ANC. Aliiongoza Afrika ya Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na kuibuka
kiongozi shujaa duniani.
Alipoanza mapambano
ya kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi na kutafuta usawa kwa wote, ilitegemewa
kuwa mke wake ndiye angekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mambo
yanakwenda sawa.
Mandela alipata kuoa
wake watatu katika historia ya maisha yake. Alimuoa mke wa mwisho siku
alipokuwa akiadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Madiba anatajwa kuwa
katika kipindi chote cha historia yake amekuwa akiwaunga mkono watoto na
upatikanaji wa elimu. Mfuko wa Nelson Mandela wa kusaidia watoto ni sehemu tu
ya ushahidi wa mafanikio ya Mandela kuwasaidia watoto.
Mandela ni baba wa
watoto sita. Watoto wanne aliwazaa na mke wake wa kwanza, Evelyn Mase na watoto
wawili aliwazaa na mke wake wa pili, Winnie Madikizela.
Inaelezwa kuwa
baadhi ya watoto wake hawakupata kwenda kumwona Madela alipokuwa gerezani.
Watoto wake wote
wawili wa kike aliowazaa na mke wa kwanza walikuwa wakitumia jina la Makazawie.
Mtoto wake wa kwanza
alifariki akiwa na umri wa miezi tisa na mtoto wa pili aliyejulikana kwa jina
la Madiba Thembikile (Thembi) alifariki katika ajali ya gari mwaka 1969 akiwa
na umri wa miaka 25. Mandela alikuwa gerezani na hakuruhusiwa kwenda kuhudhuria
mazishi ya mwanaye.
Mtoto mwingine,
Makgatho alifariki kwa ugonjwa wa Ukimwi mwaka 2005. Mandela amekuwa mstari wa
mbele kupiga vita virus vya Ukimwi na Ukimwi akitumia namba 46664 ambayo ni
namba yake alipokuwa gerezani kupiga kampeni.
Mandela na Evelyn
walidumu katika ndoa yao kwa miaka 13 kabla haijavunjika mwaka 1957. Evelyn
alikuwa muumini wa dhehebu la Mashahidi wa Yehova lililokuwa haliruhusu waumini
wake kushiriki kwenye siasa, hivyo muda wote hakujihusisha na siasa. Alifariki
mwaka 2004.
Mandela alimuoa
Winnie Madikizela mwaka 1958, ingawa muda mwingi hawakuishi pamoja kwa sababu
alikuwa kifungoni huku Winnie akijijengea umaarufu katika majukwaa ya siasa.
Kutokana na
misuguano iliyoibuka ndani ya umaarufu wa kisiasa ya Mandela na Winnie
walijikuta wakipeana talaka mwaka 1994. Mwaka 1998 Mandela alimuoa Graca Machel
ambaye alikuwa mke wa kwanza wa Rais wa Msumbiji, Samora Machel.
Rais wa sasa wa
Afrika Kusini, Jacob Zuma, ameendelea kutoa wito kwa wananchi wa nchi hiyo
wamwombee heri wakati huu anapougua. Maombi yamekuwa yakifanywa makanisani kote
nchini Afrika Kusini kumwombea Mandela apone maradhi yanayomsumbua.
Hata hivyo, Mandela
ameshaandika wosia wake na kuelekeza kwamba kama atakufa azikwe kwenye milima
iliyojitenga nyumbani kwa mababu zake huko Qunu, Afrika Kusini.
Mandela alikuwa Rais
wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 1994 hadi 1999. Alifungwa jela miaka 27 kuanzia
mwaka 1962 hadi mwaka 1990. Anaelezwa kuwa alikumbwa na ugonjwa wa mapafu
alipokuwa akifanyishwa kazi ngumu katika machimbo ya mawe akiwa gerezani.
Blogger Comment
Facebook Comment