Mshauri
na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akitoa
mada inayohusu mchango wa vyombo vya habari katika kuhamasisha matumizi
rafiki ya huduma za kuzuia VVU na Huduma za Afya ya Uzazi kwa Vijana
wakati warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu
udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU iliyofanyika hivi karibu katika
kituo cha Habari na Mawasiliano Sengerema, Mwanza chini ya mradi wa
SHUGA unaoendeshwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa UNICEF na
UNESCO kwa kuzishirikisha redio jamii nchini.
Na Mwandishi wetu Sengerema
Licha
ya jitihada za serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kupambana
na mambukizi ya Virusi Vya Ukimwi hapa nchini, baadhi ya madhehebu ya
dini nchini yameelezwa kuchangia kukwamisha juhudi hizo kutokana na
imani zao .
Hayo
yameelezwa na washiriki wa mafunzo ya siku tatu kwa vyombo vya habari
vya jamii Tanzania juu ya kuendesha mradi mpya wa SHUGA unaolenga
kutumia vyombo vya habari kutoa elimu na hamasa kwa vijana kukabiliana
na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Washiriki
hao kutoka redio mbalimbali za jamii hapa nchini wamesema kuwa kumekuwa
na baadhi ya viongozi wa dini ambao kwa namna moja au nyingine
hawakubaliani na matumizi ya kondomu kama njia sahihi ya kuzuia sio tu
maambukizi ya VVU bali pia magonjwa ya ngono na kama njia ya mpango wa
uzazi kutokana na itikadi zao kidini kwa kile wanachokiita kuzuia mimba
ni dhambi.
Pichani
juu na chini ni Baadhi ya waandishi wa Habari na Mameneja kutoka vituo
mbalimbali vya redio za jamii walioshiriki warsha hiyo wakifuatilia mada
zilizokuwa zikiwasishwa kwenye warsha hiyo.
Yamekuwepo
pia madhehebu mengine ambayo yamediriki kuzuia watu wanaoishi na VVU
kuachana na matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU na badala yake
maombi ndio njia pekee ya uponyaji jambo ambalo linaonekana kuwa imani
potofu kwa sababu ya kuchanganya imani na utaalamu wa kisayansi
uliofanyiwa utafiti wa kina na sahihi.
Matokeo
yaliyotajwa na washiriki baada ya ushawishi huo wa imani za kidini kwa
watu wanaoishi na VVU kuacha matumizi ya dawa zenye kupunguza makali ya
virusi ni kudhoofika kwa haraka, kushambuliwa na magonjwa nyemelezi
yanayosababishwa na ukosefu wa kinga mwilini na hatimaye kufa.
“Dini
ina nguvu kubwa katika kukuza maadili ya kawaida hasa juu ya heshima na
utakatifu wa maisha ya binadamu, upendo, huruma na uvumilivu na ina
mengi ya kuchangia katika mapambano dhidi ya VVU / UKIMWI hususan huduma
za kujitolea na kutoa sadaka kuwasaidia waliopatwa na maambukizi na
walioathirika, kuhamasisha watu na makundi mbalimbali kwa kutumia maeneo
ya maombi na kuchangisha rasilimali kwa ajili ya kuwajengea vituo vya
malezi watoto, wagane na wajane ni muhimu kwa waandishi wa habari
kuzitangaza na kuzipa umuhimu wake”.
Majadiliano hayo yalitokea baada ya mwezeshaji Bi Rose Haji Mwalimu kuwasilisha mada yake iliyohusu ‘Mchango Wa Vyombo Vya Habari Katika Kuhamasisha Matumizi Rafiki Ya Huduma Za Kuzuia Maambukiziya VVU,’
na kusisitiza kwamba hadi sasa bado hakuna chanjo wala tiba sahihi
kutibu VVU na UKIMWI. Njia sahihi ni kuzingatia na kufuata maagizo ya
kitaalam katika kuthibiti na kupunguza maambukizi mapya hasa kwa vijana
hususan matumizi ya kondomu.
Wakati
huo huo waandishi wa habari wamehimizwa kuzingatia maadili na lugha
mahsusi katika kuandika habari zinazohusiana na VVU pamoja na watu
wanaoishi na VVU na kuacha kuandika habari ambazo zina mwanga mdogo, ni
za mfumodume, kejeli, na zinakosa ujumbe mpya.
Mshauri
na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu
akiendelea kuwapiga msasa Mameneja na waandishi wa Habari kutoka redio
za jamii zinazoshiriki mradi mpya wa SHUGA.
“Kuna
changamoto kubwa katika kuandika na kutayarisha vipindi vya VVU kwa
sababu mara nyingi lugha zinazotumika katika taarifa au zinanyanyapaa,
kubagua, kuhukumu na kulaumu, vyombo vya habari havitendi haki”, alisema
Bi Rose Haji Mwalimu ambaye ni Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii
nchini kutoka UNESCO katika warsha hiyo.
Warsha
hiyo ya siku tatu imefanyika katika kituo cha Habari na Mawasiliano
Sengerema, Mwanza chini ya mradi wa SHUGA unaoendeshwa kwa pamoja na
mashirika ya Umoja wa Mataifa UNICEF na UNESCO kwa kuzishirikisha redio
jamii nchini.
Mshiriki
wa warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti
wa Maambukizi mapya ya VVU ujulikanao kama SHUGA kutoka Sengerema FM
Redio, Peter Marlesa (kushoto) na Mshauri na Mkufunzi wa
Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu wakifutilia kwa umakini
kazi zilizokuwa zikiwasilishwa na vikundi kazi.
Mmoja
wa washiriki kutoka redio ya jamii FADECO ya wilayani Karagwe mkoani
Kagera akiwasilisha kazi ya kikundi chake ya kutengeneza jedwali la
Message Matrix mbele ya washiriki wenzake.
Afisa Mipango VVU/UKIMWI kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumbe akifuatilia jambo kwa umakini wakati wa warsha hiyo.
Meneja wa kituo cha Kahama FM Redio, Marco Mipawa (kulia) akimshukuru Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu kwa kuwapiga msasa kupitia mradi wa SHUGA unaolenga kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU mara baada ya warsha hiyo ya siku tatu.
0 comments :
Post a Comment