-->

NDEGE YA MALAYSIA YAANGUSHWA KWA MITAMBO MAALUMU UKRAINE

Image
Wafanyakazi wa dharura wameonekana mahala ilipoanguka ndege hiyo ya abiria ya Malaysia yenye nambari ya usajili MH17, wakiweka utepe mweupe kuzunguka eneo ilipotapakaa miili ya watu walioangamia kwenye ajali hiyo mbaya kabisa.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777 iliyokuwa ikitoka Uholanzi kuelekea Kuala Lumpur, ilianguka Mashariki mwa Ukraine katika eneo ambalo linadhibitiwa na waasi wanaotaka kujitenga.
Watu wote 298 waliokuwamo kwenye ndege hiyo wamepoteza maisha, huku Marekani ikisisitiza kuwa ndege hiyo imeshambuliwa na kombora lililorushwa na mitambo maalum kutoka ardhini.
Kwa upande wake, Ukraine imewashutumu moja kwa moja waasi wanaoiunga mkono Urusi kwa kufanya kile ilichokiita "mashambulizi ya kigaidi", huku viongozi kadhaa duniani wakitaka uchunguzi wa kina kufanyika.
Wengi wa waliouwawa ni raia wa Uholanzi
Aidha Waziri wa Usafiri wa Malaysia Liow Tiong Lai, amesema miongoni mwa walioangamia ni wafanyakazi 15 wa Shirika la Ndege la Malaysia.
Waziri Tiong Lai, ameongeza kuwa wengine waliouwawa ni raia 173 kutoka Uholanzi, 43 kutoka Malaysia, Waindonesia 12, Wajerumani wanne na Waaustralia 28.
Wengi wa waliouwawa ni wajumbe waliokuwa wakielekea Australia kushiriki mkutano wa Maradhi ya Ukimwi unaofanyika wiki hii mjini Sydney.
Huku hayo yakiarifiwa viongozi mbalimbali duniani wameendelea kutoa hiasia zao juu ya madai kuangushwa kwa ndege hiyo ya Malaysia na waasi wa Ukraine.
Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott, amelitaja tukio hili kuwa ni uhalifu wala sio ajali, huku Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier akisikitishwa na mkasa huo na kutoa salamu za rambirambi kwa familia za waathiriwa.
"Nimeshtushwa na habari kutoka Mashariki mwa Ukraine watu wasiohusika na mzozo wameuwawa kwa njia hii, hili linamuacha mtu akiwa hana la kusema. Nataka kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia za abiria. Tunatarajia kila kitu kitafanyika kusawazisha hili haraka iwezekanavyo." Alisema Frank-Walter Steinmeier.
Naye Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametaka uchunguzi ufanyike haraka kujua hasa kile kilichotokea, huku akitoa wito wa kusimamishwa kwa mapigano kutoa nafasi ya wahusika kuingia katika eneo la ajali.
Vikao vya dharura vyaitishwa juu ya mkasa wa ndege
Kwa sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao ch dharura kuzungumzia mkasa huo, huku Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akiitisha mkutano mwengine wa maafisa wakuu kuzungumzia suala hilo hilo.
Wakati hayo yakiarifiwa, familia za abiria walioangamia bado wana matumaini ya kuwapata wapendwa wao wakiwa hai.
Baba ya mfanyakazi mmoja wa ndege hiyo amesema licha ya kufahamu kuwa wengi wameangamia katika tukio hilo ana matumaini kuwa mwanawe Nur Shazana Salleh yuko salama na atarejea nyumbani karibuni.
Enny Nuraheni amesema dada yake, Ninik Yuriani, raia wa Uholanzi aliye na asili ya Kiindonesia, alikuwa akielekea nyumbani kusherehekea sikukuu ya Idd ul Fitri, na sasa familia imekusanyika pamoja kwa maombolezo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment