Ndugu zangu,
Katika siku kama hii ya kusheherekea siku ya kuzaliwa kwa mke wangu mpenzi nitasimulia kwa mara ya kwanza kisa cha mimi kuingilia msafara wa Mheshimiwa Rais ili kumwahisha mwanangu aliyekuwa mgonjwa sana.
Ilikuwaje? Jumamosi ya Januari 2, 2009, tukiwa mapumzikoni Bagamoyo, kamanda wangu Manfred alizidiwa kwa malaria na kutapika sana. Alionekana kupungukiwa nguvu kwa haraka. Niliwasiliana na daktari Dar es Salaam na aliniambia, kuwa pamoja na kuwa ilikuwa ni Jumamosi mchana, angetusubiri ili amwudumie mgonjwa.
Basi, tulipofika Tegeta Wazo, na mimi nikiwa ni dereva huku mtoto akiendelea kutapika na homa kali, magari yote kutokea Bagamoyo yalisimamishwa kupisha msafara wa viongozi waliokuwa wakitoka kumzika Mheshimiwa Rashid Kawawa, nyumbani kwake Madale.
Kwa kuangalia afya ya mwanangu, nikalazimika nitafute njia za pembeni pale Tegeta na hata kutokea mahali ambapo kulikuwa na upenyo tena wa kuingia barabara kuu. Trafiki aliyepaswa kunizuia hakuwa mahali pake, nami nikawasha taa zote za gari yangu na nikaingia barabara kuu baada ya msafara wa JK kupita na nikiunganisha katikati ya magari mengine yaliyokuwa yakifuata nyuma yake. Trafiki aliyeniona nikiingia kwenye msafara naye alipigwa na butwaa na bila shaka aliamini huenda nasi tulikuwa kwenye msafara lakini tulipotea njia!
Kutoka hapo ikawa spidi ya zaidi ya 140 kwa saa kwa kasi ya msafara wa JK! Ndani ya dakika 25 tukawa tumeshafika hospitalini. Daktari alionekana kushangaa sana kutuona, mimi, mke wangu na watoto katika muda huo mfupi tangu tupigiane simu tukiwa Bagamoyo. Sikutaka atuulize ilikuwaje, na hakuuliza , bali alianza kuhangaika na mgonjwa.
Na kwa kuyaandika haya sitarajii kuwa nitaitwa trafiki nikaandikishe maelezo kwa kosa la kuingilia msafara wa JK, Jumamosi, Januari 2, 2009!
Usiku Mwema.
Maggid,
Iringa.
0 comments :
Post a Comment