Dar es Salaam. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko zito
ikieleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kupinga
mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya
Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi Tume ya Mabadiliko
ya Katiba aliyoiteua.
Tamko hilo la CCT ni mwendelezo wa lawama ambazo Rais Kikwete amekuwa
akitupiwa na taasisi na watu mbalimbali kutokana na mchakato wa kuandika
Katiba Mpya kwenda mrama baada ya mkuu huyo wa nchi kueleza maoni yake
dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Serikali ya Muungano wakati
akilihutubia Bunge la Katiba.
Miongoni mwa watu waliojitokeza kuzungumzia kauli hiyo katika siku za
karibuni ni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, maaskofu
wa Kanisa Katoliki, katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa na Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad.
Jana, CCT iligongomea msumari juu ya lawama hizo ikifananisha kauli ya
kiongozi huyo aliyoitoa Machi 21, mwaka huu wakati akifungua Bunge
Maalumu la Katiba mjini Dodoma na mama anayeamua kubeba mimba na
kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza mtoto, badala ya kumfurahia.
Pia katika tamko lake (limechapishwa kwa ukamilifu Uk. 36 wa gazeti
hili), jumuiya hiyo imewataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu maoni ya
Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuacha kujadili maoni ya
vyama vyao vya siasa.
“Inashangaza jinsi chama kimoja cha siasa kinavyolazimisha wabunge na
wanachama wake kukubaliana na mapendekezo yake ambayo yanapingana wazi
na yaliyomo katika rasimu ya Katiba,” linaeleza tamko hilo lililotolewa
baada ya Mkutano wa 48 wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika
Julai 2 na 3 mjini Dodoma.
Tamko hilo pia limetaja mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.
Kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji
Joseph Warioba kutoa rasimu ya pili ya Katiba Desemba 30, CCM ilisambaza
waraka kuwaarifu wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM kuwa msimamo wa
chama hicho tawala ni Muungano wa serikali mbili, tofauti na mapendekezo
ya wananchi yaliyo kwenye rasimu hiyo ambayo yanataka serikali tatu.
Licha ya mara kadhaa Jaji Warioba kutetea kile kilichopendekezwa na Tume
yake, wajumbe hao kutoka CCM wameyapinga maoni hayo na kusisitiza kuwa
yanaweza kubadilishwa kadri Bunge la Katiba litakavyoona inafaa.
Kitendo hicho kilisababisha wajumbe kutoka vyama vingine kuunda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao Aprili 16 uliamua kususia vikao vya
Bunge hilo ukitoa masharti kuwa utarejea bungeni kama chombo hicho cha
kuandika Katiba kitajikita kujadili mapendekezo ya wananchi kama
yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Bunge hilo litaendelea na vikao vyake Agosti 5 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta anahaha kushawishi Ukawa walegeze msimamo wao.
Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la Katiba, Rais Kikwete aligusia
mambo kadhaa yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa
kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka, ikiwa ni
pamoja na muundo wa serikali tatu kwa maelezo kuwa idadi ya watu
waliotaka muundo huo ni ndogo.
0 comments :
Post a Comment